LONDON, UINGEREZA
BARAZA la Mawaziri la Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, limekubali kuwa raia wa Umoja wa Ulaya hawatapewa upendeleo maalumu wa kufanya kazi nchini hapa kama ilivyokuwa kabla wakati taifa hilo litakapoondoka katika umoja huo (Brexit).
Mawaziri hao waliokutana juzi kwa pamoja waliunga mkono mfumo unaozingatia taaluma na uwezo na si uraia.
Taarifa hizo ambazo haijajulikana chanzo chake, zimeripotiwa katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na magazeti ya The Times na The Guardian ya hapa.
Kwa hivi sasa raia kutoka nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya wako huru kuishi na kufanya kazi Uingereza kwa mujibu wa sheria ya umoja huo inayoruhusu raia wake kufanya kazi katika nchi wanachama bila pingamizi.
Lakini uhuru huo utakwisha baada ya Brexit, ikiwataka badala yake wafuate sheria ya uhamiaji sawa na nchi nyingine zisizotoka eneo hilo huku wenye ujuzi kitaalamu wakipewa kipaumbele.