23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Uhusiano wa ndugu wa karibu na matukio ya ubakaji

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo Bisimba.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo Bisimba.

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

DAI (si jina lake halisi) ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule moja ya sekondari iliyoko mkoani Kilimanjaro.

Mwanafunzi huyo alijikuta akiingia katika ulimwengu mpya baada ya kubakwa na mtoto wa jirani yao wakati akiwa darasa la tano.

Kulingana na mwanafunzi huyo, mara kwa mara kijana huyo ambaye kwa wakati huo alikuwa amemzidi umri kwa miaka sita, alikuwa akimuita katika nyumba ambayo ilikuwa haijamalizika ujenzi wake kisha kumlaghai kwa kutaka kufanya naye mapenzi.

“Alikuwa akiniambia nilale chini halafu ananivua nguo na kujaribu kuingiza uume wake kwangu…lakini nilikuwa naumia hivyo akawa anashindwa.

“Siku aliyofanikiwa kunibaka alinipa Sh 500…sikuwahi kumwambia mama nilikuwa naogopa kwa sababu alinitishia kuwa nikisema ataniua,” anasema mwanafunzi huyo.

Mama wa binti huyo aligundua kuwa mwanawe amebakwa siku ya pili baada ya kutokea tukio hilo.

“Aliamka akaniambia kuwa huku chini (sehemu za siri) kunatoka usaha, nilishtuka sana nikaamua kumpeleka hospitali. Lakini cha kusikitisha nilipofika hospitali daktari alimuangalia na kuniambia mama huyu mwanao haumwi ila watu wameshamaliza yao.

“Awali sikumwelewa nikamuuliza daktari una maana gani, akaniambia hizi ni shahawa na si usaha,” anasema mama huyo.

Hata hivyo tofauti na matarajio ya wengi kwamba pengine kijana huyo angechukuliwa hatua za kisheria lakini haikuwa hivyo.

“Wazazi wake walikuja wakaniomba wakaniletea Sh 20,000 na kitenge cha wax basi nikaamua kusamehe, unajua tena tumeishi hapa kama ndugu na hatukuwahi kugombana hata siku moja,” anasema mama huyo.

KISA KINGINE

Mwaka jana gazeti hili pia liliwahi kuripoti tukio la kusikitisha la mtoto wa kiume (15) aliyelawitiwa na mjomba wake.

Mtoto huyo ni yatima na wazazi wake walifariki dunia wakati akiwa bado ni mdogo hivyo mjomba wake alimchukua ili amlee.

Kulingana na mtoto huyo, mjomba wake huyo mwenye mke na watoto wawili, alianza kumfanyia vitendo hivyo vya kinyama akiwa darasa la tano wakati huo akiwa na umri wa miaka 12.

“Ilikuwa ni kawaida yetu mimi na wenzangu yaani watoto wa mjomba tukioga pamoja lakini baadaye mjomba alituamuru kuwa kila mtu awe anaoga peke yake.

“Siku ya kwanza nilipoingia bafuni kuoga peke yangu mjomba alikuja na kuanza kuingiza vidole vyake sehemu zangu za siri, huku akinitishia kuwa nisimwambie mtu.

“Aliendelea hivyo kila mara na baadaye alinifanyia vibaya zaidi kwa kuuviringisha uume wangu huku akiniingilia sehemu ya haja kubwa jambo lililonifanya nipige kelele kwa sababu ya maumivu makali.

“Baada ya kelele hizo alikuja shangazi yaani mke wake, akahoji kinachoendelea, lakini mjomba alimwambia mambo ya wanaume hayakuhusu na kwamba tupo bafuni tunaoga hivyo aondoke.

“Kila anaponifanyia hivyo amekuwa akinitishia kuniua huku akiwa amenishikia kisu hivyo nilikuwa naogopa kumwambia mtu yeyote kwa sababu najua angeniua nikaona niendelee kuvumilia tu,” anaeleza mtoto huyo.

Hata hivyo baadaye mjomba huyo alikamatwa na kabla ya kufikishwa katika vyombo vya sheria aliomba suala hilo limalizwe kindugu lakini nduguze walikataa na kumpeleka kwenye vyombo vya dola.

Tukio lingine la kusikitisha ni lile la askari polisi aliyebaka na kumlawiti mtoto wa miaka 13.

Askari huyo mwenye namba G 9762 PC Daniel (24) alihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Ilala baada ya kupatikana na makosa ya kubaka na kumlawiti mtoto huyo wa miaka 13.

Visa hivi ni mfano tu wa matukio mengi yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini huku mengine yakihusisha ndugu wa karibu waliopewa jukumu la ulezi kwa watoto husika.

Matukio mengi yanayohusisha ndugu humalizwa bila kuchukuliwa hatua zozote za kisheria ili kumlinda mbakaji au mlawiti.

Matokeo ya haya yote ni kuendelea kuongezeka kwa matokeo ya ulawiti na ubakaji hasa kwa watoto, kwani ndugu husika hata kama atafukuzwa huenda akarudia kufanya tukio kama hilo mahali kwingine kwa sababu atakuwa hana hofu yoyote.

HALI ILIVYO

Takwimu za matukio ya ubakaji zilizotolewa na Jeshi la Polisi kati ya Januari na Julai mwaka huu, zinaonyesha watoto wa kike na kiume 2,571 walibakwa na kulawitiwa hapa nchini.

Kulingana na takwimu hizo, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni ndio unaongoza kwa kuwa na matukio 187 ya watoto waliobakwa katika kipindi hicho, Mbeya 177, Morogoro 160, Pwani 159, Temeke 139 na Ilala 109.

Mbaya zaidi ni kwamba ndugu na jamaa wa karibu ndio wanaoongoza kwa kufanya matendo hayo ya kinyama.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambacho wiki iliyopita kiliadhimisha miaka 21 tangu kuanzishwa kwake, kilitumia maadhimisho hayo kupaza sauti juu ya unyanyasaji kijinsia hasa matukio ya ubakaji na ulawiti watoto.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk. Hellen Kijo Bisimba, anasema idadi ya watoto wa kiume kulawitiwa inaongezeka kwa kasi ya ajabu.

“Matukio ya watoto wa kiume kulawitiwa yameendelea kuongezeka kwa kasi ya ajabu huku wahusika wakirandaranda bila kuchukuliwa hatua za msingi kwa hoja ya uhusiano wa karibu kati ya mtoto na aliyemlawiti.

“Ripoti inaonyesha asilimia 49 ya vitendo hivyo hufanyika nyumbani, asilimia 23 hufanyika njiani wakati wa kwenda au kurudi shuleni na asilimia 15 hufanyika shuleni,” anasema Dk. Bisimba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Edda Sanga, anasema kuna ucheleweshwaji na upotoshwaji ushahidi wa kesi za vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ubakaji na ulawiti katika ngazi ya mahakama, polisi na baadhi ya madaktari hospitalini.

Anasema baadhi ya madaktari wamekuwa wakiwaomba walalamikaji (waathirika) fedha ili fomu zao zinazojulikana kama fomu namba 3 (PF3) zijazwe ukweli vinginevyo zijazwe uongo.

“Kuna baadhi ya viongozi wanapokea rushwa ili kuzima kesi za watoto wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia, pia baadhi ya polisi wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano kwa mlalamikaji ambapo wanatoa maneno ya vitisho na kusababisha mlalamikaji kukosa ujasiri wa kuhifadhi na kutetea kesi yake.

“Kwa mfano kesi ya ubakaji kwa mtoto wa miaka 9, fomu yake ilipotoshwa ikaandikwa kuwa mtoto aliyebakwa alikuwa na umri wa miaka 19, ikaambatanishwa kwenye jalada lililokwenda kwa mwanasheria wa serikali, kesi hiyo haikupelekwa mahakamani kwani illikosa ushahidi.

“Madaktari wengine wamelalamikiwa kupokea rushwa kutoka kwa watuhumiwa ama ndugu na jamaa za watuhumiwa ili fomu hizo zijazwe kwa kupotosha ukweli,” anasema Sanga.

Kamishna wa Dawati la Jinsia na Watoto katika Jeshi la Polisi, Adolphina Chialo, anasema unyanyasaji wa aina zote upo na bado ni tishio kwa Watanzania.

MANISPAA YA ILALA

Katika Manispaa hiyo kati ya Januari hadi Agosti mwaka huu, watoto 302 walifanyiwa ukatili wa kingono.

Ofisa Uhusiano wa Manispaa hiyo, Tabu Shaibu, anasema vitendo hivyo  huanzia majumbani  na ndiko  kunakoongoza  kwa sababu kwa wakati huo  walimu huwa hawapo  katika nafasi  ya kujua  nini  wafanyacho  watoto nje ya shule.

“Uchunguzi wetu umebaini kwamba baadhi ya watoto waliripoti kuanza kufanyiana na wenzao na wengine walifanyiwa majumbani au wakati wakirudi nyumbani kutoka shule.

“Mazingira mengi yanayowazunguka watoto hayapo salama hivyo wazazi na walezi wachukue tahadhari dhidi ya mazingira yanayowazunguka watoto hasa katika kuchangamana na watu waliowazidi umri,” anasema Shaibu.

WAZAZI

Ines Urio ni mama mwenye watoto wawili ambao wanasoma katika shule za msingi tofauti zilizoko Kata ya Buza, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Anasema watoto wake wote ni wa kike na mmoja anasoma darasa la pili huku mwingine akiwa darasa la awali.

“Kwakweli mimi huwa nazungumza sana na wanangu nawaeleza ukweli kwamba wakipewa chipsi au juisi wasikubali kwa sababu wanaweza kubakwa. Huyu mtoto wangu aliyeko awali alikuwa hajui maana ya kubakwa nikamuelewesha wazi kabisa bila kutafuna maneno.

“Nashukuru Mungu pamoja na udogo wao lakini wanangu sasa wanaelewa hatari ya kubakwa au kulawitiwa. Nawashauri wazazi wasisubiri hadi watoto wawe wakubwa ndio waanze kuwaaambia, siku hizi watu wengi hawana hofu ya Mungu wanabaka hadi watoto wachanga hivyo tuwafundishe kujilinda mapema,” anasema Urio.

ATHARI KWA WATOTO

Mtaalamu wa Saikolojia ambaye pia ni Mhadhiri wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (Mwecau), Christian Bwaya, anasema vitendo vya ubakaji na ulawiti vina athari kubwa katika ustawi wa watoto.

Anasema ubakaji una athari za kimwili na kisaikolojia ambapo kisaikolojia mtoto husononeka na kukosa furaha wakati wote, pia huingiwa na hofu na kudhani kwamba atabakwa au kulawitiwa tena.

USHAURI

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anawashauri wazazi na walezi wasikubali kuwalaza chumba kimoja watoto wa kike na ndugu wa kiume kwani tabia hizo chafu zimekuwa zikifanywa na watu wa familia.

Naye Mkurugenzi wa LHRC, Dk. Bisimba, anasema Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inaeleza wazi juu ya mtu aliyeaminiwa kumlea mtoto na baadaye akamfanyia unyama kwa aina yoyote kwamba atapata adhabu zaidi kuliko kawaida.

“Mtu aliyeaminiwa awe ndugu, kiongozi wa dini au yeyote yule na baadaye akamfanyia mtoto unyanyasaji au unyama, sheria hiyo inampa adhabu zaidi tofauti na mtu wa kawaida aliyefanya hivyo.

“Wazazi na walezi wasimamie vyema wajibu wao kuhakikisha watoto wanakua katika malezi yenye maadili salama kwa kuwathamini na kuwalinda katika matukio mbalimbali ambayo yanaweza kuwanyima haki stahiki,” anasema Dk. Bisimba.

Anawashauri viongozi wa dini kuhubiri haki za watoto na kutahadharisha wanajamii wanaowaongoza kuwa na hofu ya Mungu ili kuepuka kutenda dhambi ikiwemo uvunjaji wa haki za watoto.

 

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Kituo cha One Stop Centre kinachoshughulikia masuala ya watoto katika Hospitali ya Amana, Suphian Mndolwa, anasema suala la elimu bado ni tatizo kwani wako wazazi au walezi ambao huwapeleka watoto wao katika vituo hivyo wakiwa wameogeshwa na kuwabadilisha nguo jambo linalopoteza ushahidi wa kidaktari.

“Daktari anapaswa kuandika kile anachokiona siku hiyo, hivyo wazazi waripoti mapema matukio ya unyanyasaji dhidhi ya watoto kwa kupiga namba 116 (Child Help Line) na kuhakikisha hazizidi saa 72 ili kupata ushahidi.

Naye Askofu wa Makanisa ya Ufunuo nchini, Paul Bendera, anasema ongezeko la matukio ya kikatili kwa watoto linatokana na watu kutokuwa na hofu ya Mungu, kukosa maarifa ya malezi na kujali kwani matukio mengi yanatokea hata kwa wanafamilia wenyewe.

“Unakuta mtu kafanyiwa nayeye anataka kulipiza, umasikini kwa wazazi na walezi kuwaozesha binti zao katika umri mdogo, kuokosa maadili pia ni sababu mojawapo,” anasema Askofu Bendera.

0768 745725

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,636FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles