WATAALAMU wa afya wanaonya kwamba wagonjwa wa kisukari au moyo wakae majumbani nyakati ambazo kuna vyombo vingi vya moto barabarani.
Wanasema utitiri wa vyombo vya moto hasa vile chakavu barabarani husababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira ulio hatari kwa afya zao.
Kwa sababu hiyo, watu wanene na wale wanaougua maradhi ya moyo au kisukari hawapaswi kuwapo barabarani nyakati zenye foleni kali ili kuukwepa moshi huo wa magari.
Onyo la madaktari hao linakuja miaka mitatu tu tangu utafiti wa kimataifa uonye kuwa hewa chafu huathiri mioyo dhaifu na hata kusababisha kifo.
Utafiti huo uliofadhiliwa na Mfuko wa Maradhi ya Moyo wa Uingereza na kuchapishwa katika Jarida la Sayansi la Lancet, ulitokana na tafiti 35 zilizokuwa na takwimu za maelfu ya wagonjwa katika mataifa 12 yakiwamo ya Uingereza, Marekani na China.
Katika utafiti huo wagonjwa pamoja na mambo mengine walisimulia jinsi uchafuzi wa hewa ulivyozidi kudhoofisha hali zao za moyo.
Uchafuzi huo ulitokana na hewa zenye sumu kama vile za carbon monoxide na nitrogen dioxide, pamoja na zile zinazodaiwa kuwa safi yaani moshi kutokana na mabasi, teksi, pikipiki na malori.
Moshi aina hiyo unaweza kupenya mbali mapafuni na kutokea hapo huingia kwenye mkondo wa damu.
Wataalamu hao kutoka Chama cha Maradhi ya Moyo barani Ulaya hivi karibuni pia walitoa mwito wa upunguzaji wa matumizi ya mafuta ya ardhini (fossil fuels).
Walionya, uchafuzi wa hewa si tu unadhoofisha hali duni zilizopo sasa kiafya bali pia huchangia kuibua maradhi hayo.
Hiyo ni kwa sababu uchafuzi wa hewa hudhoofisha maendeleo ya shinikizo la juu la damu na kuharibu utendaji wa insulini, ambazo zote ni visababishi hatarishi kwa unene na kisukari.
Wataalamu hao pia walipendekeza watu wenye pumu, watoto wachanga na wazee waepuke maeneo hatarishi kwa uchafuzi wa hewa.
Madaktari wanapaswa kuanza mara moja kuwashauri watu waliopo katika makundi hatarishi waepuke maeneo yenye uchafuzi wa hewa, walisema.
Professa Robert Storey, kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza alisema; “Vifo vya watu zaidi ya milioni tatu duniani kila mwaka husababishwa na uchafuzi wa hewa.
“Uchafuzi wa hewa unashika nafasi ya tisa miongoni mwa visababishi hatari vya maradhi vinavyorekebishika (modifiable disease risk factors), ukitanguliwa na ukosefu wa mazoezi, mlo wenye sodium kwa wingi, wenye mafuta mengi kwenye damu (cholesterol) na matumizi ya dawa.”
Sasa kuna ushahidi wa kutosha kuwa uchafuzi wa hewa husababisha kuugua kwa muda mrefu na vifo kutokana na maradhi ya moyo, alisema.
Aliongeza; “Si tu inafanya hali iliyopo ya maradhi ya moyo kuwa mbaya zaidi bali pia kuchangia kuibuka kwa maradhi hayo.
“Kuepuka uchafuzi wa hewa kwa kadiri inavyowezekana kunasaidia kupunguza hatari ya maradhi ya moyo na wataalamu wa maradhi ya moyo wanapaswa kuzingatia hilo wakati wa utoaji ushauri kuhusu staili ya maisha kwa wagonjwa wao.
Alisema; “Pia tunahitaji kuongeza shinikizo kwa watengeneza sera kupunguza viwango vya uchafuzi wa hewa.
“Uchafuzi wa hewa unapaswa kuhesabika kama moja ya visababishi vikuu vinavyorekebishika vya maradhi ili kuzuia na kudhibiti maradhi ya moyo.
“Mtu mmoja mmoja hasa wale wenye au walio katika hatari ya kukumbwa na maradhi ya moyo, wanaweza kuchukua hatua kupunguza uwezekano wa kukaribia hatari na madaktari wanapaswa wazingatie hilo wakati wanapotoa ushauri kwa wagonjwa wao kuhusu staili za maisha.
“Watengeneza sera wanapaswa wapunguze viwango vya uchafuzi wa hewa na hilo linapaswa kutungiwa sheria.”
Theluthi moja ya watu wa Ulaya wanaoishi katika maeneo ya mjini wako hatarini kuvuta hewa iliyochafuka kwa kiwango cha juu ya kile cha Umoja wa Ulaya, wataalamu walionya.
Lakini Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema karibu watu tisa kati ya 10 wa Ulaya wako hatarini kukumbwa na kiwango cha uchaguzi wa hewa kinachochafua afya zao.
Watoto wachanga, wazee na watu wenye matatizo ya upumuaji wanapaswa waepuke kutembea au kuendesha chombo katika barabara zenye shughuli nyingi.
Hali kadhalika wanashauriwa kufanya mazoezi au kupita mbali na sehemu hizo na kuziepuka zile nyakati za shughuli nyingi.
Walio hatarini wanapaswa wahakikishe kwamba daima wamebeba dawa zao popote pale waendako.
Lakini uchafuzi wa hewa nje ya nyumba unaoingia majumbani bado ni tatizo, walionya.
Matatizo mengi ya uchafuzi hutokea ndani ya nyumba, hivyo wataalamu wanapendekeza uwekaji wa mifumo ya uingizaji na uchujaji hewa majumbani katika maeneo yenye uchafuzi mkubwa wa hewa.
Profesa Storey aliongeza; “Watunga sera wana jukumu muhimu la kupunguza uchafuzi wa hewa nje ili kuzuia uchafuzi wa mazingira ya ndani ambako sehemu kubwa ya athari za kukumbana nao hutokea.
“Mbali ya kupunguza mchango wao binafsi kwa uchafuzi wa hewa mitaani, kunatakiwa pia liangaliwe suala hili la uchafuzi wa hewa majumbani kwa kuweka mifumo ya kuchuja hewa ili kuvuta hewa safi.
“Kuondokana na matumizi ya mafuta ya ardhini kwa ajili ya uzalishaji nishati kutasababisha manufaa makubwa kwa afya ya mwanadamu, kutokana na upunguzaji wa hewa chafu na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Nchini India utafiti uliofanywa na Global Burden of Disease (GBD), umeonesha hewa chafu nje ya majumba inayotokana na moshi wa magari, uvutaji sigara ni chanzo cha vifo vya mapema vya watoto 700 kila mwaka nchini humo.
GBD pia iliorodhesha moshi huo kama mmoja wa wauaji bora 10 duniani na wa sita kwa uuaji Kusini mwa Asia.
Aidha utafiti mwingine nchini Marekani unasema kwamba wanawake wenye kisukari ambao wanakabiliana na uchafuzi wa hewa kwa kipindi kirefu wanakaribisha hatari ya kukumbwa na maradhi ya moyo.
“Utafiti wetu ni moja ya ile ya kwanza inayoonesha hatari kubwa ya maradhi ya moyo miongoni mwa wale wanaokabiliwa na moshi wenye sumu kwa kipindi kirefu,” alisema kiongozi wa utafiti huo Jaime Hart kutoka Shule ya Tiba ya Harvard mjini Boston.
Wakati watafiti wa kimataifa wakija na matokeo hayo, ambayo hakuna shaka shaka yatafanyiwa kazi, changamoto inabakia katika mataifa yetu ya dunia ya tatu kama Tanzania.
Nchini Tanzania wagonjwa wa maradhi ya moyo na kisukari wanazidi kuongezeka sambamba na uchafuzi wa hali ya hewa unaosababishwa na ongezeko kubwa la magari.
Mbaya zaidi magari mengi barabarani ni chakavu na hatuna vifaa maalumu vya kuchuja hewa chafu kama wanavyoshauri wataalamu.
Katika hilo unapata picha wagonjwa wangapi wanaathirika au kuibuka kutokana na uchafuzi huo? Kazi kwetu!