25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

UHURU, TRUMP WAKUTANA IKULU YA MAREKANI

Marekani


Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amehitimisha ziara yake ya siku tatu nchini Marekani jana kwa kukutana na Rais Donald Trump, katika Ikulu ya Marekani kwenye kikao cha wajumbe wa pande zote mbili  na kutia saini makubaliano ya ushirikiano katika nyanja mabalimbali.

Ilikuwa ni ziara rasmi ya kwanza nchini Marekani kwa Rais Kenyatta tangu aingie madarakani ambapo yeye na mkewe Margaret walipokewa na Rais Trump na mkewe Melania kabla ya kikao ambapo masuala kadhaa yalijadiliwa, yakiwemo uwekezaji, biashara na usalama.

Trump, akizungumzia baadhi ya Nyanja za ushirikiano, alisema Marekani itashiriki katika ujenzi wa barabara kubwa nchini Kenya.

“Tunafanya mipango ya mradi mkubwa wa ujenzi wa Barabara kubwa ambayo itakuwa kielelezo na mfano wa kuigwa. Tuko na wajumbe waliofuatana na Rais Kenyatta na tutatia saini makubaliano kadhaa ya kuzinufaisha nchi zote mbili na ni heshima kubwa kwa rais na mkewe kuzuru ikulu ya Marekani,” amesema rais Trump.

Kenyatta amesema kwamba ili kufanikisha azma nne kuu ambazo ameahidi kuzipa kipaumbele katika muhula wake wa pili na wa mwisho kama rais, zikiwamo afya kwa wote, makazi nafuu, lishe ya kutosha na utengenezaji wa bidhaa na vifaa, ni muhimu kwa Kenya kuwa na mazingira mema ya kuwavuta wawekezaji kutoka nchi kama Marekani.

Kenyatta alimweleza Trump jinsi Kenya inavyothamini ushirikiano wake na Marekani.

“Kenya na Marekani zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na imara tangu tulipopata Uhuru. Tuko hapa kuuimarisha uhusiano huo. Na tuna ushirikiano mwema hususan katika kupambana na ugaidi na hasa kwa sababu ya ujirani wetu.

“Tunaendelea kupambana na Al-Shabab, ambapo Marekani imekuwa mshirika mkubwa na wa karibu. Cha muhimu Zaidi ni kuimarisha ushirikiano wetu wa kibiashara ambao tayari uko imara. Tuna makampuni mengi ya Marekani nchini Kenya. Tunataka kuona jinsi ya kuimarisha ushirikiano huo kwa faida ya nchi zote mbili,” amesema Rais Kenyatta.

Baada ya mkutano wa ikulu, Serikali ya Kenya ilitia saini makubaliano ya zaidi ya shilingi bilioni 25 na kampuni mbalimbali za Marekani, ambayo yameanzisha au yataanzisha miradi kadhaa ya uwekezaji katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Kiasi kikubwa cha uwekezaji huo kikiwa ni katika nyanja ya umeme na kilimo.

Kenyatta amekuwa rais wa pili Afrika chini ya jangwa la Sahara kualikwa na Trump Ikulu ya Marekani, tangu Trump achaguliwe kuwa rais ambapo wa kwanza alikuwa Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria.

Rais Kenyatta aliongozana na wajumbe wakiwemo mawaziri, maseneta, wabunge na wafanya biashara katika sekta mbalimbali.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles