NA ISIJI DOMINIC
SAKATA la aina yake lilishuhudiwa katika Bunge la Taifa nchini Kenya wiki iliyopita kwenye kikao maalumu ambacho kilipitisha mapendekezo ya Rais Uhuru Kenyatta ya Muswada wa Fedha 2018.
Awali Rais Uhuru alikataa kutia saini utekelezaji wa muswada huo uliopendekeza ushuru wa kodi asilimia 16 ya bidhaa inayotokana na mafuta baada ya wabunge kupitisha muswada huo uahirishwe kwa miaka miwili zaidi ili waufanyie marekebisho.
Kama angesaini Rais, hii ingekuwa mara ya tatu muswada huo unaahirishwa kwa sababu mwaka 2013, wabunge walipitisha muswada huo kuahirishwa kwa miaka miwili na mwaka 2016 ambapo ingeanza kutekelezwa, wabunge tena wakapitisha uahirishwe kwa miaka mingine miwili.
Septemba Mosi mwaka huu, Waziri wa Fedha Henry Rotich alianza kutekeleza kutozwa kwa kodi ya asilimia 16 akiwa na lengo la kukusanya fedha ili kusaidia Serikali kutekeleza miradi yake na hususani ajenda nne kuu alizojiwekea Rais baada ya kula kiapo kuwatumikia wananchi kwa awamu yake ya pili.
Waziri Rotich alisimamia utozaji ushuru wa asilimia 16 akisubiri Rais kama atatia saini Muswada wa Fedha 2018 itakayozuia Wakenya kutozwa kodi ya asilimia 16 ya mafuta. Hata hivyo Rais Uhuru alirudisha muswada huo bungeni huku akipendekeza kushusha kwa asilimia 50 ushuru ulioanza kutekelezwa.
Ni agizo ambalo lilimlazimu Spika wa Bunge, Justine Muturi, kuitisha kikao cha siku mbili ili wabunge wajadili mapendekezo ya Rais ambapo kama wangemkubalia basi Wakenya wangeanza kutozwa kodi ya asilimia nane ya bidhaa zitokanazo na mafuta na endapo wangemkatalia, Muswada wa Fedha 2018 inakuwa sheria na utozaji huo wa ushuru ungesitishwa kwa miaka miwili zaidi.
Macho ya Wakenya wengi yalikuwa kwa wabunge ambao walitarajia watatupilia mbali mapendekezo ya Rais ambayo yangeongeza gharama ya maisha. Kilichohitajika ni robo tatu au takribani wabunge 233 kati ya 349 kupiga kura kupinga mapendekezo hayo ya Rais.
Kwa mara nyingine tena tangu Rais Uhuru na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kukutana Machi 9, mwaka huu na kuahidi kufanya kazi pamoja, tulishuhudia viongozi hao wakizungumza lugha moja.
Rais Uhuru alikutana na wabunge wa Chama cha Jubilee Ikulu jijini Nairobi wakati Raila alikutana na wabunge wanaounda Muungano wa NASA katika Jumba la Orange, Nairobi na wote wakawashawishi wabunge hao kupiga kura kuunga mkono mapendekezo ya Rais ya kushusha kodi kutoka asilimia 16 hadi nane.
Swali likabaki, Je, wabunge watasimama na viongozi wao wa chama au Wakenya? Katika kile kinachoonekana hali ya kushangaza, sauti za wabunge waliokataa mapendekezo ya Rais ndiyo iliyokuwa kubwa lakini waliotangazwa washindi ni wale waliyoikubali na hivyo basi muswada huo kupita ambapo Rais Uhuru aliutia saini siku iliyofuata na kuwa sheria.
Wachambuzi wa siasa wanasema kupita kwa muswada huo ni ushindi wa Uhuru na Raila na kikubwa matunda ya ‘handshake’ lakini wanahoji, kama wabunge walidai wapo na wananchi, kwanini walikataa muswada huo kupigiwa kura kwa njia ya elektroniki na kuukubali ule utaratibu wa NDIO/HAPANA?
Ni dhahiri wabunge walitaka kuuwa ndege wawili kwa jiwe moja. Hawakutaka kuonekana wakaidi mbele ya viongozi wao wa chama ambao walikutana nao kuwashawishi kupitisha mapendekezo ya Rais. Vile vile, kitendo chao cha kuzungumza na vyombo vya habari baada ya kutoka bungeni wakionesha kusikitishwa maamuzi ya Spika kupitisha mapendekezo ya Rais waliyoikataa ungewafanya waonekana mashujaa mbele ya wananchi wa kawaida.
Kuna kila dalili wabunge walihofia kura ya kielektroniki ambapo wangetakiwa kila moja aliyekuwa bungeni kuhesabiwa na kisha kusema kama anaunga mkono au anakataa mapendekezo ya Rais.
Siku moja baada ya Rais Uhuru kutia saini muswada huo na kuwa sheria, Raila aliwapongeza wabunge wa NASA waliopitisha mapendekezo ya Rais huku akisisitiza anaunga hatua hizo mpya za kodi akiitaka serikali ndani ya mwaka moja kutumia vyema fedha zitakazokusanywa.
Aidha Raila ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani ameitaka serikali kupunguza matumizi yasiyokuwa na ulazima kwa ajili ya kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo na kuionya wakishindwa ataongoza wananchi kutupiliwa mbali kwa muswada huo na kufanya kampeni ya kodi ya asilimia sifuri kwa mafuta.
“Asilimia nane ya ushuru kwa mafuta haitafanya Wakenya kuumia mbali itaongeza uchumi wa nchi na tumeiambia Serikali pamoja na Bunge kupunguza matumizi yasiyo na ulazima,” alisema Raila.
Miongoni mwa matumizi yasiyo na ulazima ambayo yanastahili kupunguzwa ni serikali kutumia magari makubwa, kamati za bunge kufanya vikao vya Mombasa badala ya Nairobi na safari za nje ya nchi kwa kutumia usafiri wa daraja la juu.
Raila alisema kama nchi ina pengo la Bajeti kubwa, mtu hawezi kuendesha uchumi wa nchi kwa njia mwafaka labda matumizi yapunguzwe au kodi iongezwe.
“Kama tunapunguza kodi basi matumizi hayana budi kupunguzwa na hiyo itamaanisha Bajeti inalenga sekta muhimu kama afya,” alisema kiongozo huyo wa upinzani na kubainisha Rais alipunguza kodi na kufikia asilimia nane ikiwamo kupunguza matumizi ya serikali.
Matumaini ya Wakenya wengi ni kwamba serikali itatumia vyema fedha zitakazokusanywa kutokana na ushuru wanaotozwa. Pia Wakenya wana matumaini makubaliano ambayo serikali iliafikiana na Serikali za Uingereza na Uswisi kurudishwa fedha zilizofichwa nje ya nchi zitatumika vyema.