24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

UHURU: NIMEWATIMIZIA WAKENYA AHADI ZOTE

NAIROBI, KENYA


RAIS Uhuru Kenyatta ameeleza kuridhika kwake na kile alichotaja ufanisi mkubwa chini ya utawala wake, akisema historia itamkumbuka kwa kuleta mageuzi muhimu nchini hapa, hasa ugatuzi.

Kwenye taarifa ya kuadhimisha miaka minne ya utawala wake, Kenyatta alisema kumekuwa na mafanikio mengi kuliko yaliyofanywa tangu Kenya ipate uhuru.

“Ninajivunia kwa ugatuzi ambao umetekelezwa kikamilifu. Ninaamini historia itakumbuka wajibu wa utawala katika kipindi hiki cha mageuzi kwa nchi yetu,” alisema huku akikumbuka Aprili 9 kama siku muhimu kwake alipoapishwa kama rais.

“Juhudi zetu ziliongozwa na utekelezaji wa kiapo changu kuheshimu, kulinda na kutetea Katiba yetu, na pia kwa sababu ninaamini ugatuzi kama muundo bora wa uongozi.”

Hata hivo, viongozi wa upinzani walipuuzilia mbali mafanikio yaliyotajwa wakisema wananchi wamezidi kutaabika chini ya utawala wake.

Naibu Kiongozi wa Wachache Bungeni, Jakoyo Midiwo, alisema utawala huu utakumbukwa tu kwa ufisadi na ubaguzi wa kikabila katika utoaji wa vyeo serikalini.

“Kuanzia kwa masuala ya uporaji ardhi hadi sakata kubwa za kiuchumi, na jinsi rais mwenyewe alivyokiri hajui la kufanya kukabiliana na ufisadi, hii Serikali imeshindwa kabisa,” alisema.

Rais Uhuru alisema kuwa amejitahidi kuimarisha usalama, kwa kuongeza idadi ya polisi na kuimarisha mikataba yao ya utendaji kazi.

Pia amekuwa akikashifiwa kwa kukopa kiwango kikubwa cha fedha kutoka kwa mataifa na mashirika ya kigeni ilhali hakuna maendeleo mengi yanayoonekana.

Katika taarifa yake, aliusifu mradi wa ujenzi wa reli ambao ni miongoni mwa ile iliyotumia kiwango kikubwa zaidi cha mikopo, akisema utawaondoa Wakenya kutoka umasikini kwa kutoa nafasi za ajira.

“Ni teknolojia ya kisasa, iliyojengwa kuleta mageuzi kwa kilimo na biashara, kwa kujali wanyama pori wetu,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuwa kuna mengi zaidi ya kufanya akieleza kuwa kubadilisha nchi, uchumi na mifumo ya uongozi huchukua muda.

“Tumefanya mengi zaidi katika muda wa miaka minne iliyopita kuliko nchi nyingi zilivyofanya. Tumeweka msingi, tumeonyesha kuwa Kenya inaweza kufanya mambo kulingana na ratiba na pia bajeti,” alieleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles