Mgombea urais wa Chama cha Jubilee nchini Kenya, Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya kutoruhusu uchaguzi kuwagawa kwa sababu Kenya itaendelea kuwepo hata baada ya uchaguzi.
Akizungumza baada ya kupiga kura Kaunti ya Gitundu, Kenyatta amesema kulikuwa na kampeni za amani na anaamini Wakenya wana hamu ya kuendelea na amani hiyo baada ya uchaguzi.
“Uchaguzi usitugawe sisi ni ndugu hata bila uchaguzi na baada ya uchaguzi, nawaambia amani, amani, amani… kila Mkenya apige kura aende nyumbani asubiri matokeo tutakuwa na Kenya baada ya uchaguzi na tutaendelea kuwa ndugu, dada, kaka na jirani hata baada ya uchaguzi.
“Nimetumia saa mbili katika foleni ya kupiga kura naona amani imetawala, fujo na vurugu zinaharibu Kenya yetu,” amesema.
Aidha, amesema endapo mpinzani wake atashinda katika uchaguzi huo ataheshimu maamuzi ya Wakenya na atashirikiana naye kuongoza pamoja kuipeleka Kenya mbele kwa maslahi na faida ya Wakenya.