31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

UHURU ASHUTUMIWA KWA KUUA DEMOKRASIA VYUONI

NAIROBI, KENYA


Rais Uhuru KenyattaWANAFUNZI wa vyuo vikuu juzi walimshutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kuidhinisha sheria inayopiga marufuku viongozi wa wanafunzi vyuoni kuongoza kwa zaidi ya miaka miwili.

Wakiongozwa na kiongozi wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Were Sam na mwenzake wa Chuo Kikuu cha Moi, Towett Ng’etich, walisema kuwa sheria hiyo inalenga kukandamiza demokrasia vyuoni.

“Sheria hiyo inalenga kutatiza demokrasia ya wanafunzi katika vyuo vikuu nchini,” Sam aliwaambia wanahabari mjini hapa.

Sheria mpya pia hairuhusu wanafunzi kuchagua viongozi wao moja kwa moja kutokana na kubuniwa kwa mfumo wa baraza la wajumbe litakalokuwa na usemi wa mwisho katika uchaguzi vyuoni.

“Uchaguzi vyuoni sasa utapitia mikononi mwa wajumbe wachache ambao wataketi chumbani na kuamulia maelfu ya wanafunzi viongozi wao,” alisema Sam.

Viongozi hao wa wanafunzi pia walikosoa kifungu kingine cha sheria kinachozuia kiongozi wa zamani katika chuo kimoja kuhamia chuo kingine na kuwania uongozi.

“Mbona tunafungia nje wanafunzi walio na kipaji cha uongozi kutowania uongozi katika chuo kingine wanapoenda kuendeleza masomo yao? Wabunge waliopitisha muswada huo, mbona wao hawajajiwekea ukomo wa miaka wanayofaa kuhudumu?” alihoji Ngetich.

Wanafunzi hao walisema sheria hiyo inakinzana na katiba na wakatishia kwenda mahakamani ili itupiliwe mbali.

“Tutapigana dhidi ya sheria hii mahakamani. Hatutaruhusu sheria inayokandamiza haki ya wanafunzi,” alisema Sam.

Walisema wanafunzi ambao ni wadai wakuu, hawakushauriwa kabla ya kupitishwa kwa muswada huo, kinyume na matakwa ya katiba inayotaka wananchi kuhusishwa katika uamuzi.

Wanafunzi pia walimshutumu vikali Kiongozi wa Wengi Bungeni, Aden Duale aliyewasilisha mswada huo kwa lengo la kukandamiza haki ya wanafunzi vyuoni.

Sheria hiyo inaonekana kumlenga Paul Ongili maarufu kama Babu Owino, ambaye amekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi (Sonu) tangu mwaka 2010.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles