UHURU AONGOZA KURA YA MAONI KENYA

0
525

NAIROBI, KENYA


IWAPO uchaguzi ungefanyika leo, asilimia 47 ya Wakenya wangekipigia kura chama tawala cha Jubilee kulinganisha na asilimia 42, ambao wangeuchagua muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), kura mpya za maoni zilizoendeshwa na taasisi maarufu ya Ipsos zimeonesha

Lakini kwa kulinganisha na kura ya maoni ya taasisi hiyo iliyochapishwa Januari mwaka huu, mchakato wa sasa unaonesha viongozi wa NASA, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wanakuja kwa kasi dhidi ya Uhuru Kenyatta na William Ruto wa Jubilee.

Nasa imejipatia asilimia zaidi ya 10 ya kura kutoka asilimia 30 ilizokuwa nazo Januari 2017 hadi asilimia 42 Mei mwaka huu huku Jubilee ikiendelea kuwa na asilimia zake 47 ilizokuwa nazo kipindi hicho.

Namna umma unavyowaamini wagombea urais, Rais Uhuru Kenyatta anaongoza kwa kuwa na asilimia 40, William Ruto wa pili akiwa na asilimia 31, Raila Odinga ana asilimia 25 na Kalonzo Musyoka asilimia 12.

Kuhusu mwelekeo wa taifa, asilimia 71 ya Wakenya waliohojiwa na Ipsos katika utafiti huo wa robo ya pili wanasema Kenya iko katika mwelekeo usio sahihi.

Wafuasi wa Nasa wanazungumzia picha mbaya zaidi kwa vile asilima 91 miongoni mwao wanasema taifa hilo linaelekea shimoni wakati wafuasi wa Jubilee wenye mtazamo kama huo wakiwa asilimia 52 ya waliohojiwa.

Kati ya wale wanaosema kwamba taifa hilo linaendeshwa kuelekea kusiko, asilimia 68 wanaeleza gharama ya maisha kuwa sababu.                      

Utafiti huo wa Ipsos uliendeshwa kati ya Mei 11 na 23 ukihusisha Wakenya 2,026 waliohojiwa ana kwa ana na 5,484 kwa njia ya simu katika kaunti 46.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here