23.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

UHURU AMSHAWISHI KALONZO AACHANE NA RAILA

MAKUENI, KENYA


RAIS Uhuru Kenyatta ameendelea kumshawishi mgombea mwenza wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), Kalonzo Musyoka, aungane naye serikalini wakuze taifa.

Kiongozi huyo wa taifa, akikiongoza Chama cha Jubilee kunadi sera zake jana katika Kaunti ya Makueni, ameeleza imani yake kuwa atambwaga kinara wa Nasa, Raila Odinga kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumanne ijayo.

“Nawaambia wazi huyu mtu wa kitendawili (Raila) mara hii ataenda nyumbani saa tatu za asubuhi siku ya kupiga kura. Ndiyo maana namwambia ndugu yangu Kalonzo njoo serikalini tukuze taifa hili, huyo mtu wa vitendawili hakuna mahali anakupeleka,” alisema Rais Uhuru.

Akaongeza: “Namwambia yale ambayo Kalonzo aliniambia mwenyewe hapo awali kuwa Raila hakuna mahali anaenda.”

Uhuru amekuwa akimshawishi Kalonzo ajiunge na Serikali yake akimweleza atakuwa mgombea mwenza wa Naibu wake William Ruto akiwania urais mwaka 2022.

Awali Rais Uhuru alidai kuliona jina la Kalonzo likiwasilishwa katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na Chama cha Wiper awe seneta maalumu endapo Nasa itabwagwa na Jubilee.

Hata hivyo, Kalonzo amekana madai hayo.

Akiwashawishi wapigakura kumchagua kwa wingi, Rais Uhuru amemsuta tena Raila akisema kuwa hadithi zake hazitalisha wananchi.

“Sisi tunaongea kwa macho na vitendo, kila mara mnaelezwa stori nyingi ambazo hamtazila. Aache kupiga stori zake kwa vyombo vya habari kuwa ataibiwa kura, auze sera zake kwa amani. Aeleze watu wa magazeti tu na sisi tunachapa kazi,” alisema.

Uhuru aliwaahidi wananchi wa Makueni miradi mingi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jiji la kisasa maarufu kama Konza City.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles