24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Uhuru ampa mamlaka zaidi Waziri Matiang’i

NAIROBI, KENYA                    

RAIS Uhuru Kenyatta juzi alimwongezea Waziri wa Usalama wa Ndani, Dk. Fred Matiang’i, mamlaka makubwa zaidi kwa kumteua kusimamia kamati ya maendeleo, utekelezaji na mawasiliano katika baraza la mawaziri ambao wote watakuwa chini yake.

Hatua hii inampa Matiang’i, anayesifika kwa uchapa kazi na usimamizi mzuri uwezo wa kumulika utendaji wa wizara zote za serikali na hivyo kumfanya kinara wa wenzake.

Anakuwa jicho la rais katika utekelezaji wake wa ajenda nne kuu za maendeleo, msimamizi wa usalama wa taifa pamoja na utawala wa serikali kuu mikoani na kauntini.

Kwenye agizo kuu la kwanza la Rais mwaka huu, Dk. Matiang’i atakuwa akiripoti kwa Rais Kenyatta moja kwa moja kuhusu utendakazi wa kila waziri serikalini.

Kamati hiyo itakayojulikana kama Kamati ya Taifa ya Utekelezaji wa Maendeleo na Mawasiliano ya Baraza la Mawaziri, pia itashirikisha Mwanasheria Mkuu na Katibu wa Baraza la Mawaziri.

Itakuwa na ofisi na wafanyakazi ambao watakuwa chini ya Matiang’i.

Mamlaka haya mapya yanamfanya Matiang’i kufuatilia kwa makini na kikamilifu yanayotendeka katika wizara nyingine za serikali kama alivyofanya mwaka jana alipoidhinisha sheria za usalama barabarani na kusimamia mitihani ya taifa.

“Ni muhimu kutoa agizo kuu la rais kueleza mfumo wa kusimamia kikamilifu, kushirikisha na kutekeleza miradi ya maendeleo ya serikali,” alisema Rais Kenyatta.

Aidha, jukumu la kamati hiyo litakuwa ni kuhakikisha fedha zinazotengewa miradi ya maendeleo zinatumiwa ipasavyo na kwamba mawasiliano ya serikali yatakuwa yakiwafikia umma na wadau ipasavyo.

Naibu wa Matiang’i katika kamati hiyo atakuwa ni Waziri wa Fedha Henry Rotich.

Uteuzi huo ulijiri saa chache baada ya Rais Kenyatta kuwapatia wakuu wa kanda, ambao wako chini ya Matiang’i nguvu za kushirikisha maendeleo na usalama katika maeneo yao.

Rais Kenyatta pia alihamisha Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama wa Taifa (NTSA) kutoka kwa Wizara ya Uchukuzi hadi Wizara ya Usalama wa Ndani inayosimamiwa na Matiang’i.

Hii inamaanisha shughuli za usalama barabarani sasa ziko chini ya waziri huyo anayetambulika kama mchapa kazi hodari katika kila idara anayosimamia.

Wizara yake pia inasimamia usalama wa taifa na idara ya polisi, ujasusi na usalama. Makamanda wote wa polisi wako chini yake na ni mwanachama wa baraza la usalama la taifa. Pia makamishna wote wa kanda wamo chini yake.

Wakenya walimpongeza Rais kwa hatua hiyo wakisema Matiang’i ni mchapa kazi na atamaliza ufisadi ambao umekuwa kikwazo cha maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles