25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

UHURU AMEPANGA KUGOMEA MATOKEO – RAILA

NAIROBI, KENYA



MGOMBEA urais wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, amedai kuwa Rais Uhuru Kenyatta amepanga kung’ang’ania madaraka atakaposhindwa katika uchaguzi wa Agosti 8.

Raila alidai Uhuru anaendesha harakati za kuunda vikosi vinavyopatiwa mafunzo vikihusisha maofisa kutoka polisi, wanyamapori, misitu na jeshi kwa namna inayoashiria udikteta.

Aidha alimtaka Rais Uhuru na naibu wake, William Ruto kuacha kueneza uongo kuwa NASA haijajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu na inataka Serikali ya ‘nusu mkate’, yaani ya ushirika, akisisitiza wamejiandaa ‘tangu jana’.

“Rais Uhuru anaonekana kujiandaa kukataa matokeo kwa sababu anafahamu fika atashindwa,” alidai Raila.
Aliongeza: “Tumeshuhudia kipindi cha miaka ya karibuni ongezeko linaloifanya Kenya kuwa taifa la kijeshi, huku rais akienda huku na kule katika mavazi ya kijeshi.

Wakati huu tuzungumzao, Uhuru anashinikiza majeshi kushughulikia changamoto ambazo ni yeye pekee azijuaye.”

Raila alisisitiza hitaji la uchaguzi huru, halali na wa haki, ambao alisema utapatikana tu katika zoezi huru na la amani.
“Wakenya wanataka chaguzi za wazi na hawatakubali zaidi ya hilo. Nimesema mara nyingi kuwa nitakubali matokeo iwapo yatafanyika kwa namna halali.

“Lakini kutumia vyombo vya Serikali ikiwamo vya usalama kutasababisha hujuma dhidi ya uchaguzi,” alionya Raila.
Aidha alimshutumu Rais Uhuru kwa kudai kuwa NASA inataka uchaguzi uahirishwe na kuwa wanapendelea Serikali ya ushirika.

“Uongo huu unaenda sambamba na maandalizi makubwa ya kijeshi kwa askari kumiminwa maeneo maalumu,” alisema Raila.

Aidha aliitaka Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutatua kasoro zilizopo katika daftari la wapigakura, ambalo lina wapigakura hewa wakiwamo wafu.

Daftari hilo linahusisha wapigakura 400,685 wanaodaiwa walijiandisha zaidi ya mara moja.
Hivi majuzi IEBC iliondoa majina ya watu 88,000 kutoka katika daftari hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles