Na Bakari Kimwanga,
MTO Nile ni miongoni mwa mito mikubwa iliyopo upande wa Mashariki wa Bara la Afrika na duniani kote ukiwa na urefu wa kilomita 6,695. Bonde la Mto Nile hukusanya maji kwa ujazo ambao ni asilimia 10 ya ujazo unaokusanywa na mabonde yote ya Afrika.
Kwa muonekano wa juu Mto Nile unaonekana kama pembetatu huku upande wa chini wa eneo hilo, yaani kaskazini na upande wa juu kusini kuna mimea mbalimbali iliyostawi kwa wingi.
Na katika kipindi cha mwisho wa mwaka eneo la Mto Nile huwa linakuwa na wekundu kimwonekano kutokana na kushamiri maua aina ya ‘lotus.’
Japokuwa mimea hii haioti kwa wingi wakati huu kama ilivyokuwa hapo awali, mimea mingine inayostawi zaidi katika eneo la Mto Nile kwa upande wa chini ni ile inayoitwa Egyptian lotus na kwa upande wa juu ni ile inayoitwa Cyperus papyrus.
Chanzo cha Mto Nile ni pamoja na mito yote inayopeleka maji kwenda Ziwa Victoria kutoka nchi za Tanzania, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na Kenya.
Aidha, upande mwingine wa Mto Nile unaanzia Ethiopia ukijulikana kama Abbai au Nile ya Buluu, ambao unatoka katika Ziwa Tana. Katika vyanzo hivi vyote imebainika kwamba chanzo cha mbali kabisa cha Mto Nile ni Mto Luvironza huko Burundi unaoingia katika Mto Kagera na kufika hadi Ziwa Victoria.
Mto Nile ambao unaanzia Ziwa Victoria nchini Tanzania ni chanzo kikubwa cha maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwandani, kilimo cha umwagiliaji na kuzalisha umeme kwa wakazi wa nchi za bonde hilo.
Kutokana na nchi nyingi kuzungukwa na Mto Nile, suala la ushirikiano katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za bonde la mto huo limepewa kipaumbele ili kuzuia migogoro inayoweza kuzuka baina ya nchi zinazoutumia.
Pamoja na ushirikiano uliopo, hali ya uchafuzi wa mazingira imekuwa changamoto kubwa katika Ziwa Victoria ambalo limekuwa tegemeo kubwa kwa nchi wanachama wanaotumia maji kupitia Mto Nile.
Changamoto zilizopo katika Bonde la Ziwa Victoria ni pamoja na uchafuzi wa mazingira kutokana na ongezeko la shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi, usafirishaji, uzalishaji viwandani, uchimbaji madini na utiririshaji wa maji machafu.
Mbali na hayo, ziwa hilo limekuwa likikabiliwa na magugu maji na uvuvi usio endelevu ambao unatumia zana hatari zisizoruhusiwa kisheria.
Hali hiyo imekuwa ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na usimamizi dhaifu wa mfumo wa pamoja wa kudhibiti utiririshaji wa maji kutoka viwandani na shughuli nyingine za kibinadamu zinazotokana na mahitaji mbalimbali kwa nchi husika.
Kuna juhudi za uhifadhi mazingira ya Bonde la Ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na vyanzo vyote vya maji, ardhi oevu na madakio yake ikiwamo kuwapa elimu jamii zinazoishi maeneo kuzunguka eneo hilo ili kuwapo mazingira endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Lakini bado kuna hali inayotishia uhai wa chanzo hiki cha mkusanyiko wa maji ya Mto Nile.
Ni vema taasisi zenye jukumu la ulinzi na usimamizi wa rasilimali na faida zitokanazo na ziwa hususan maji, samaki na usafiri zioanishe sera, sheria na taratibu baina ya nchi wanachama.
Lakini pia kunahitajika upimaji na ufuatiliaji wa hali ya Ikolojia za ziwa na utafiti ili kuweza kudhibiti na kuzuia uchafuzi toka kwenye vyanzo mahususi kwa kuboresha mifumo ya maji safi na maji taka kwenye miji na maeneo yanayozunguka ziwa.
Pia kuendeleza njia za uzailishaji viwandani zisizochafua mazingira kama njia ya kupunguza Nyanja za uchafuzi zinazotokana na usafirishaji ziwani na usalama.
Kwa mujibu wa Sera ya Maji Tanzania inatambua kwamba, maji ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Hivyo, binadamu anahitaji maji kwa matumizi ya nyumbani na kwa ajili ya matumizi yake mengine ya kiuchumi na kijamii, kwa kuwa maji ni uhai.
Aidha, kwa ujumla na umuhimu wake upo dhahiri kwamba maji yanahitajika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile uzalishaji viwandani, umwagiliaji mashamba, ufugaji, usafishaji wa madini, uzalishaji wa umeme, usafiri na uchukuzi, burudani na utalii.
Tanzania inashirikiana na nchi nyingine katika umiliki, utunzaji na matumizi ya rasilimali za maji ya kimataifa.
Katika matumizi makubwa ya maji shirikishi kunahitaji maelewano na makubaliano baina ya nchi husika zinazotumia Mto Nile. Mchakato huu unaendelea kutekelezwa na nchi husika za Bonde la Mto Nile.
Kimsingi ipo changamoto ya kubaini mahitaji halisi ya matumizi ya maji shirikishi kwa mabonde yote ikiwamo bonde la Mto Nile na mikakati mahususi ya kuyatumia maji hayo.
Maandalizi ya pamoja na changamoto hizo, nchi husika katika Bonde la Mto Nile zimeendelea kutumia teknolojia na utaalamu kuaninishwa changamoto hizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayosimamia shughuli za uendelezaji wa Bonde la Mto Nile (NBI), Innocent Ntabana anasema azma ya kusimamia na kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto Nile imepewa kipaumbele na nchi zote zinazozungukwa na mto huo, jambo hilo ndiyo kiini cha kuanzishwa kwa sekretarieti ya NBI mwaka 1999.
NBI ina jukumu la kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la Mto Nile kwa niaba ya nchi wanachama zipatazo 10 ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Misri
Kwa upande wa Mratibu wa Kanda wa Kitengo cha Uratibu cha Bonde la Mto Nile (NELSAP-CU), Elicad Nyabeeya anasema kuwa mto huo una manufaa makubwa kwa nchi wanachama kwani muunganiko wa nchi hizo umeleta mawasiliano mazuri ambayo yanasaidia kuinua uchumi wa nchi hizo katika usimamizi na uzalishaji.