MOJA ya habari zilizokuwapo katika ukurasa wa pili wa toleo la jana la gazeti hili, ilizungumzia kitendo cha Idara ya Uhamiaji kukamata mitambo ya kughushi nyaraka mbalimbali za idara hiyo pamoja na mashine za kielektroniki (EFDs).
Habari hiyo ilitolewa na Kamishna wa Usimamizi wa Mipaka wa Idara ya Uhamiaji, Samwel Magweiga na alisema nyaraka hizo zilimilikiwa kinyume cha sheria na kuikosesha Serikali mapato.
Kwa mujibu wa Magweiga, watu watano ndio waliokamatwa baada ya kujifanya ni mawakala wa idara hiyo na walikuwa wakiwatapeli wananchi kwa kujifanya ni maofisa wao, wakati ni matapeli.
Alisema hadi sasa upelelezi umekamilika na watu hao watafikishwa mahakamani ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Pia alisema kwamba, watu hao wamekuwa wakitumia mitambo mbalimbali kughushi kazi zinazofanywa na idara hiyo, huku wakijua ni kinyume cha sheria.
Licha ya mitambo hiyo, alisema watu hao wamekutwa na nyaraka za shughuli za Serikali, zikiwamo miradi ya maendeleo na EFDs zinazorekodi kodi za Serikali.
Kutokana na hali hiyo, alisema idara hiyo imepiga marufuku watu wote wanaojifanya mawakala wao na kufanya kazi zinazofanana na uhamiaji kinyume cha sheria na kuonya kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Awali ya yote, sisi wa MTANZANIA Jumamosi tunaipongeza idara hiyo kwa kung’amua utapeli unaofanywa na watu hao kisha wakawakamata.
Lakini tunawashangaa kwa kuchelewa kuwakamata, kwamba siku zote walikuwa wapi kuwakamata wao na mitambo hiyo, ama walikosa taarifa za intelijensia za utapeli unaofanywa na watu hao.
Kwa sababu tunaamini hadi sasa watakuwa wameshawatapeli watu wengi na kuwasababishia wananchi usumbufu na kuikosesha Serikali mamilioni ya fedha.
Pia kwa mujibu wa habari aliyoitoa Magweiga mwenyewe, ni kwamba hadi sasa wamepata taarifa ya kuwapo kwa magenge ya wahalifu wanaotumia jina la idara hiyo kwa ajili ya kuwatapeli wananchi.
Kama hivyo ndivyo, tunaishauri idara hiyo isiishie kuwaomba wananchi kushirikiana nao kwa kutoa taarifa kwenye mamlaka husika juu ya watu wanaojifanya mawakala waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, ili kupunguza au kudhibiti utapeli huo, bali wanatakiwa kujua chanzo cha tatizo hilo ni nini?
Kwa sababu sisi tunaamini labda chanzo cha magenge ya matapeli hao ni mtandao mpana wanaoshirikiana nao kufanya vitendo hivyo na pengine baadhi yao, wakiwamo watumishi wa idara hiyo.
Kwamba baadhi ya watumishi hao ambao si waaminifu wanashirikiana na matapeli hao na pengine ndio wanaothibitisha matumizi ya nyaraka hizo idarani hapo.
Kwa hiyo, tunaishauri idara hiyo kwamba wakati ikiwa katika mchakato wa kukomesha utapeli huo, pia ianze kumulika watumishi wake ili kubaini kama kuna baadhi wanaoshirikiana na matapeli hao.