22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Uhamiaji: Tangu 2013 tunamchunguza mwanahabari Kabendera

Andrew Msechu -Dar es salaam

IDARA ya Uhamiaji imesema imekuwa ikimfuatilia mwandishi wa habari za uchunguzi, Eric Kabendera tangu mwaka 2013, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakilalamika kuwa si raia wa Tanzania.

Wakati hayo yakiendelea, leo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam itatoa uamuzi wa maombi ya mawakili wa Kabendera wanaoiomba iamuru Jamhuri imfikishe mahakamani.

Akitoa ufafanuzi katika mahojiano na MTANZANIA jana, Kamishna wa Uraia na Pasipoti wa idara hiyo, Gerald Kihinga, alisema uchunguzi huo ulianza muda mrefu, lakini yeye alikaidi alipoitwa kutoa maelezo ya upande wake.

“Ni kwamba uchunguzi ulianza kufanyika muda mrefu na tulikuwa tukimuita kuhojiwa akawa hataki kuja, yaani kama angetupa ushirikiano akaja tukamuhoji tukamaliza, tukapata tunavyohitaji, tungemalizana naye tukaendelea na taratibu nyingine,” alisema.

Kihinga alisema watu wanaohojiwa na idara hiyo kuhusu masuala ya uraia ni wengi na wanapotoa ushirikiano ndipo wanawarahisishia kazi yao, kwa sababu uchunguzi unaweza kuanza na kupata taarifa za awali.

Alisema kwa Kabendera, tayari hatua ya taarifa za awali ilishamalizika na ilifikia hatua sasa walikuwa wanataka kumuhoji ili kulinganisha taarifa walizonazo.

“Tatizo yeye alikuwa hataki kuja, kwa hiyo tukaona tumkamate tumuhoji kwa nguvu na kupata vile tulivyokuwa tunavitaka kwa nguvu, angekubali mapema sisi tungekuwa hatuna shida,” alisema.

Alisema kuhusu suala la kumaliza utata wa uraia wake mwaka 2013 si sahihi, kwa kuwa hawajawahi kumuona wala kumsafisha, ndiyo maana waliamua kumhoji.

“Hatujawahi ‘kum-clear’ (kumsafisha) sisi, na tungekuwa ‘tumem-clear’ (tumemsafisha) tusingekuwa tunaendelea naye, hajawahi hata kuhojiwa hapa kwetu sisi,” alisema.

Awali, katika mkutano wake na wanahabari Dar es Salaam, Kamishna Kihinga alisema waliamua kumkamata Kabendera baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusu utata wa uraia wake.

Alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kupata taarifa hizo, hivyo kulazimika kuzifanyia kazi.

“Hata hivyo, Kabendera alikuwa hajawahi kuhojiwa kuhusiana na uraia wake, kwa kuwa hakufika ofisini, japokuwa aliwahi kutumiwa wito mara kadhaa wa kumtaka afike ofisini kwa mahojiano.

“Na ndiyo maana sasa Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imemtafuta na kumkamata ili ahojiwe kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi kuhusu uraia wake. Uchunguzi utakapokamilika matokeo yake yatatolewa,” alisema.

Alifafanua kuwa uchunguzi wa utata wa uraia umekuwa ukifanyika kwa watu kadhaa wakiwemo watu mashuhuri katika jamii, hivyo suala hilo limeibua hisia kwa kuwa muhusika ni mwanahabari.

Kihinga alisema Idara ya Uhamiaji imekuwa ikishirikiana na vyombo vingine ya ulinzi na usalama, katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo suala hilo si geni.

“Idara inatoa wito kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano na taarifa kwa masuala yahusuyo uhamiaji ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama,” alisema.

Alieleza kuwa Idara ya Uhamiaji ambayo ni chombo kilichopewa dhamana ya kusimamia na kutekeleza Sheria ya Uraia ya Tanzania Sura ya 357 rejeo la 2002, ina mamlaka ya kuchunguza na kuthibitisha uraia wa mtu yeyote anayetiliwa shaka, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa vyanzo vyake.

Alisema jukumu hilo la utambuzi wa uraia limekuwa likitekelezwa kwa mtu yeyote kwa mujibu wa sheria bila kujali dini, rangi, kabila wala wadhifa wa muhusika katika jamii.

Kabendera ambaye anaandikia magazeti ya ndani na nje ya Tanzania, alichukuliwa kwa nguvu jioni ya Jumatatu iliyopita nyumbani kwake Mbweni, Dar es Salaam na watu waliojitambulisha ni polisi.

Juzi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliwaeleza waandishi kwamba wanamshikilia mwandishi huyo kwa mahojiano kuhusu uraia wake.

Mambosasa alisema walimkamata Kabendera nyumbani kwake baada ya kupelekewa wito wa kufika kuhojiwa, lakini alikaidi.

Jana, Kamishna Kihinga alisema baada ya kumwita kwa muda mrefu na kukaidi waliamua kutumia Jeshi la Polisi kufanikisha kumkamata.

Alisema walipata taarifa kuwa Kabendera si rai wa Tanzania na wiki mbili zilizopita walianza uchunguzi kuhusiana na taarifa hizo.

“Tulianza uchunguzi kila tukitaka kumuhoji hataki, tulimpigia simu, tulimwita, lakini hakutaka kuja, na kwa vile polisi tunashirikiana, tuliwaomba watusaidie kumkamata,” alisema Kihinga.

Alisema tayari wanaye na wameshafanya mahojiano ya awali na kama ataonyesha ushirikiano wataangalia suala la kumpa dhamana.

Kuhusu uraia wa ndugu zake, Kihinga alisema watakapomaliza naye mahojiano watakachobaini ndiyo kitakachowafanya kuanza uchunguzi kwa ndugu zake.

Kutokana na kuibuka kwa utata wa kukamatwa kwa mwanahabari huyo kuhusu uraia wake, Mei 2013, yalifanyika mahojiano ya mwisho kuhusu suala hilo.

Hatua hiyo ilijumuisha matukio ya kuhojiwa kwa wazazi wake kijijini kwao, jambo ambalo lilizua taharuki na manung’uniko.

Kutokana na hali hiyo kwa wakati huo, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliunda kamati iliyofanya kazi ya kuchunguza uraia wa Kabendera.

Kwa mujibu wa kumbukumbu hizo, Dk. Nchimbi, aliwaagiza  maofisa wa uhamiaji kutowasumbua wazazi wa Kabendera kuhusiana na uraia wao, agizo ambalo alilitoa baada ya mwanahabari huyo kuandika barua ya malalamiko kwa waziri mwenye dhamana.

Hata hivyo, ikiwa imepita miaka sita baadaye, suala hilo sasa limeibuka tena huku likizua utata kuhusu kukamatwa kwa mwanahabari huyo.

TAMKO LA MCT

Baraza la Habari Tanzania (MCT), limeoliomba Jeshi la Polisi kumwachia huru mara moja Kabendera wanayemshikilia kuanzia Jumatatu.

Taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na Katibu Mtendaji wa  baraza hilo, Kajubi Mukajanga, ilieleza kuwa kosa analotuhumiwa mwandishi huyo lina haki kisheria ya kupata dhamana.

“Kuhusu suala la uraia wa mwandishi huyo, tamko hilo limeeleza kuwa ni la tangu 2013, ambalo Idara ya Uhamiaji ilishughulikia suala hilo na kuthibitisha uraia wake.

 “Kabendera ni mwandishi anayejulikana kitaifa na kimataifa, kuendelea kumshikilia kwa sababu zilizotolewa kunaleta picha isiyo nzuri kwa Tanzania, lakini pia kunaleta hofu kwa waandishi wa habari, wanataaluma na wananchi kwa ujumla,” alisema Kajubi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles