UHALALI WA NDOA BURUNDI UNAPOTUMIKA KUFUNIKA KOMBE

0
703

NI suala la maridhiano ya kimahaba yanayofikia kwenye kuoana na kuishi kinyumba linalowahusu waliopendana na kushibana, linalosimamiwa na sheria za nchi husika wanayoishi wanandoa lakini nchini Burundi muunganiko wa ndoa umegubikwa muktadha wa shinikizo la kimamlaka kutokana na tangazo la hivi karibuni la Serikali ya Rais Pierre Nkurunzinza, kwamba wanaoishi kwenye ndoa za dhana zisizohalalishwa wamepewa hadi mwishoni mwa mwaka kuhalalisha ndoa zao ukiwa ni mkakati wa kukarabati maadili mema katika wigo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 


Kampeni hiyo mahususi iliyozinduliwa na Rais Nkurunzinza inayohanikizwa na Wizara ya Mambo ya Ndani, imedhamiria kudhibiti ongezeko la idadi ya watu nchini humo kutokana na ndoa hobela, mitala, wanafunzi kupata mimba ovyo na ‘ndoa mtambuka’ kwa walio kwenye ndoa kuingia kwenye ndoa nyingine wakati ndoa zao za kwanza zingalipo bado. 


Kwamba Serikali na taasisi za kiimani zimepania kuhakikisha ndoa zinakuwa halali ili kuendeleza uzalendo kwa taifa kwa maadili mema.
Rais Nkurunzinza ameenda mbali zaidi kwa kuwa ‘somo’ na ‘nyekanga’ wa Warundi kwa kuwaambia raia wake wanaoneshane ‘mahabat’ ya dhati kwa kuoana kihalali na kuionesha mapenzi nchi yao. 


Katika kudhihirisha kuwa hatanii kampeni imepamba moto kwa wenza wote wanaoishi kinyumba wasio na ndoa kushinikizwa kujisajili ifikapo Juni 22, watakaokiuka na kukwepa utaratibu huo watawekewa vikwazo ikiwemo watoto watakaowazaa kutojumuishwa katika mpango wa Serikali wa elimu na matibabu bure. 


Ili kutimiza agizo la Serikali, tayari maafisa waandamizi wanaosimamia ndoa nchini humo wameanza utaratibu wa kuandaa ndoa za jopo, ingawa wanapingwa na wanaharakati wanaodai kuwa huo ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu kwani Serikali haina mamlaka ya kuwasukasuka wenza wawili waliopendana walioamua kuishi pamoja. 


Wanaharakati hao wanadai kuwa ndoa hizo za shuruti ni mkakati wa udikteta wa kificho uliogubikwa mashiko ya kiimani kutoka kwa Rais Nkurunzinza na mkewe ambao wote wawili ni Wakristo wa Kilokole. 


Ukiangalia suala zima unaweza kuhisi kama halina mkanganyiko wa kisiasa lakini ni sawa na kombe linalofunikwa ili mwanaharamu apite, kutokana na siasa zinazoligubika taifa hilo katika miaka ya hivi karibuni kila upande baina ya Serikali na wapinzani wanaoshirikiana na wanaharakati ukivutia ngozi kwake katika kuwamba ngoma hiyo.


Serikali inadai inatekeleza sera zake kwa mujibu wa sheria zilizopo kwa kila Mrundi kuwajibika kwa maisha yake kimaadili, kwamba mkakati huu ni mahususi kwa kuhuisha uzalendo ambao kimsingi uliasisiswa mwaka 2013 lakini kisichobainishwa ni sababu za kuleta hoja mpya inayowafanya Warundi kusahau madhila ya kisiasa.


Kutokana na fukuto lililosababishwa na mgogoro wa muhula wa kutawala ambapo kwa miaka miwili sasa hamkani si shwari katika taifa hilo kutokana na Rais Nkurunzinza kulazimisha kugombea muhula wa tatu wenye utata mnamo mwaka 2015. 
Tangu vurumai hilo liliposababisha mkanganyiko walau watu 500 wameuawa katika vurugu za kisiasa zilizoibuka na takriban wengine laki nne wamekimbilia mataifa jirani kuomba hifadhi ya ukimbizi.


Uchumi wa taifa hilo ukiathirika mno kutokana na vurumai hizo ambazo majaribio kadhaa ya kusuluhisha hayajafanikiwa kujikita katika kiini ingawa kwa sasa kuna utulivu kiasi kulinganisha na jinsi hali ilivyokuwa muda mfupi baada ya Rais Nkurunzinza kulazimisha kusalia madarakani, hususan baada ya kunusurika katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa na kuongeza uhasama si tu ndani ya nchi lakini pia na nchi jirani, kwa baadhi ya mataifa ikiwemo Rwanda kushutumiwa kuchochea mzozo huo kwa siri. 


Serikali ya Burundi inajikanganya zaidi inapocheza turufu ya kutaka ndoa halali kwa kutoa sababu zinazojikanganya kwamba inarekebisha maadili, pili inakuza uzalendo lakini inathibiti uongezeko la watu. Lakini kuhalalisha ndoa si kudhibiti ongezeko la watu kwani ndani ya ndoa halali wenza wanaweza kuamua kuzaa idadi ya watoto sawa na timu ya kandanda!
Ukitathimini msingi wa kinachojaribu kurekebishwa ni kwamba Burundi imezidiwa na muelemeo wake kiuchumi hauko sawia kutokana na machafuko yaliyorindima na kutatanisha mifumo mingi ya tija.


Kwa hiyo udhibiti wa ongezeko la watu inaweza kuwa sababu ya kujiweka sawa hususan ikizingatiwa kuwa katika kujikubalisha Serikali ya Rais Nkurunzinza imeweka vivutio vya sera zake ikiwemo elimu na matibabu ya bure kwa watoto. 
Lakini katika turufu hii ya ndoa halali kwa Warundi iwe za kiserikali au kiimani sheria ya ndoa ya taifa hilo inabainisha kuwa umri wa kuingia kwenye ndoa ni miaka 18, mwenza mmoja kati ya wanaotaka kuoana lazima awe raia.


Taarifa za kugushi wakati wa mchakato wa ndoa zinaweza kupelekea kushitakiwa, nyaraka zote za ndoa lazima zitafsiriwe katika lugha ya Kifaransa, wageni lazima waombe idhini ya Serikali ili kuoana na raia, wanaooana wawe na tabia njema, wasiwe na ndoa nyingine lakini pia kwa mujibu wa sheria hiyo posa ikishapokelewa lazima mahari iwasilishwe ndani ya miezi sita ili kuhalalisha ufungaji ndoa. 
Ni mkanganyiko wa siasa zenye muktadha wa ‘kimahaba’ kwa amri ya Serikali inayohanikiza mkakati wake wa kimaadili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here