Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema mawakala kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji wanashirikiana kuorodhesha wakulima hewa na hivyo kusababisha Serikali kudaiwa deni kubwa la Shilingi bilioni 65.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Devotha Minja (Chadema) katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu bungeni jana.
Minja alitaka kujua ni lini Serikali itawalipa mawakala waliosambaza pembejeo za kilimo kwa njia ya vocha katika msimu wa kilimo wa mwaka 2014/2015 na 2015/2016.
Katika swali la nyongeza Devotha aliitaka Serikali kuharakisha mchakato wa kuwalipa mawakala hao kutokana na madhara yaliyoanza kuwapata ikiwamo kuuziwa nyumba zao na mabenki.
Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema ni kweli mawakala hao bado wanaidai Serikali lakini akasema madeni hayo yametokana na mawakala na watendaji wasiokuwa waaminifu ambao wameibambikia Serikali deni kubwa lililofikia Sh bilioni 65.
“Tulijikuta tuna deni la shilingi bilioni 65, nilipokutana na mawakala wiki mbili zilizopita, niliwaahidi kwamba tutawalipa lakini ni lazima watupe muda tufanye uhakiki ili kubaini kama kweli pembejeo zilifika.
“Kati ya Sh bilioni 35 za madeni ya awali, imebainika kuwa Sh bilioni 6 tu ndiyo deni halali na bado kuna Sh bilioni 30 nyingine zinafanyiwa uhakiki,” alisema Waziri Mkuu.
Hata hivyo Majaliwa alisema kutokana na Serikali kubaini kuwapo kwa watendaji wasiokuwa waaminifu, deni hilo halitalipwa mpaka hapo Serikali itakapofanya uhakiki ili kupata deni halisi.
“Tukianza kulipa bila kufanya uhakiki, itaigharimu Serikali kulipa fedha nyingi ambazo kimsingi zingeweza kufanya shughuli nyingine za maendeleo, lazima tujiridhishe kwenda kwenye maeneo husika na kufanya uhakiki ili tujue Serikali inadaiwa kiasi gani cha fedha,’’ alisema.
Katika swali jingine Mbunge wa Viti Maalum, Amina Molel (CCM) alitaka kujua Serikali inatoa kauli gani juu ya kuwapatia watumishi wenye ulemavu hususan walimu vifaa vya kujifunzia na kufundishia ikiwamo nukta nundu ili watumishi hao waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu. .
Akijibu swali hilo Waziri Mkuu alisema hivi sasa Serikali inafanya uratibu mzuri kwa watumishi wenye mahitaji maalum na itahakikisha vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinaendelea kupatikana.