31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

UHAKIKI MWINGINE MALI ZA CCM WAJA

 

PATRICIA KIMELEMETA, Dar es Salaam


JUMUIYA ya Wanawake ya Chama Cha Mapinduzi (UWT), inatarajia kuunda kamati maalumu ya kufanya uhakiki wa mali za jumuiya hiyo kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa.

UWT imechukua hatua hiyo ikiwa ni miezi michache tangu Mwenyekiti wa     CCM, Dk. John Magufuli, kuunda tume iliyochunguza mali za chama hicho nchi nzima.

Tume hiyo ya Rais ambayo iliongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ali, ilibaini upotevu mkubwa wa mali za chama hicho na jumuiya zake, ikiwamo Umoja wa Vijana (UVCCM), Jumuiya ya Wazee na UWT yenyewe.

Jana, Katibu Mkuu wa UWT, Mwalimu Queen Mlozi, alisema kamati hiyo itasaidia kubaini mali za jumuiya hiyo ambazo   zilifichwa au hazikutajwa wakati wa kamati ya Dk Bashiru.

“Tunaamini kuna mali nyingi za chama ambazo hazijaorodheshwa kwenye kamati ya Dk. Bashiru kutokana na sababu mbalimbali, hivyo basi kama jumuiya tuna kila sababu ya kuhakiki mali zetu tuweze kuzitambua,”alisema Mlozi.

Alisema mpaka sasa jumuiya hiyo ina mali nyingi ambazo nyingine hazijulikani zilipo na hata waliouziwa hawakufuata taratibu.

Alisema wakati umefika kwa jumuiya hiyo kupita kwa wananchi kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa   kubaini mali hizo na kuziorodhesha.

Aliwataka makatibu wa jumuiya katika ngazi za mikoa na wilaya kushirikiana na watu watakaopita kwenye maeneo yao.

“Hatuna haraka katika hili, kama kuna mali imefichwa tutajua  kwa sababu tutafuatilia hatua moja hadi nyingine  i tuweze kujua.

“Ninachowaomba makatibu wa jumuiya wa mikoa na wilaya kutoa ushirikiano kwa watu ambao watapita kwenye maeneo yao na kufuatilia suala hilo,”alisema.

Alisema baada ya kumalizika  uhakiki huo, kamati hiyo itawasilisha ripoti kwa viongozi wa juu wa jumuiya ambao nao   wataiwasilisha kwa Mwenyekiti wa CCM Rais Magufuli na Katibu Mkuu waweze kuipitia na kutoa uamuzi.

Alisema kwa wale ambao wamechukua mali hizo bila  kufuata utaratibu, uamuzi wao utatolewa  baada ya viongozi hao kupitia ripoti hiyo.

Alisema tayari imeundwa bodi ya wadhamini ambayo pamoja na mambo mengine, itaweza kusimamia mali hizo kwa utaratibu maalumu   baada ya kuhakikiwa.

Mlozi alisema  mkakati wa jumuiya hiyo ni kufanya uwekezaji kwenye mali hizo ikiwamo viwanja, maduka na mashamba hali ambayo inaweza kuwasaidia kupata mapato.

Wakati umefika wa mali hizo kusimamiwa kwa umakini na jumuiya zake  ziweze kuwanufaisha wanachama wa CCM kuanzia ngazi mbalimbali nchini, alisema.

Alisema jumuiya hiyo imekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wanawake   na kuikumbusha serikali kuteua nafasi za uongozi wa jinsia hizo   waweze kufikia malengo ya asilimia 50 kwa 50.

Alisema mpaka sasa nafasi za uongozi za wanawake ni asilimia 36, hivyo basi bado wanahitaji nafasi zaidi za uteuzi  kufikia malengo waliyokusudia.

Mlozi alisema jumuiya hiyo itaendelea kuwajengea uwezo wanawake   waweze kujikwamua katika uchumi na kujiondoa kwenye utegemezi jambo ambalo linaweza kupunguza umaskini.

Alisema wanawake popote walipo bila ya kuangalia tofauti zao za rangi, chama au kabila, wanapaswa kupaza sauti  wanapoona wenzao wanaonewa na kukemea uovu unaojitokeza kwenye maeneo yao.

Kwa mujibu wa Mlozi  jumuiya hiyo imekwisha kuanzisha dawati la jinsia ambalo pamoja na mambo mengine, litajitika kusikiliza kero za wanawake na kutoa elimu ya jinsi ya kujikomboa.

Aliwataka wanawake kujitokeza kwenye uchaguzi mbalimbali ukiwamo wa siasa na jamii ili kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles