23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

UHABA WA SUKARI WAIKUMBA MBEYA

 

 

Na PENDO FUNDISHA -MBEYA

WANANCHI wa Mkoa wa Mbeya wameiomba Serikali kuingilia kati mfumuko wa bei ya sukari kutokana na kupanda kutoka Sh 2,500 kwa kilo hadi kufikia Sh 3,000.

Mfuko wa kilo 20 za sukari ukiwa unapatikana kwa Sh 56,000 kutoka Sh 44,000 na kilo 50 ikipatikana kwa Sh 120,000 kutoka Sh 100,000.

Wakizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa nyakati tofauti juzi, watumiaji na wauuzaji wa bidhaa hiyo jijini Mbeya, walisema wanashagazwa na ongezeko la ghafla la bei ya sukari licha ya Serikali kupiga marufuku.

Walisema ni vema Serikali ikadhibiti tatizo hilo kutokana na wananchi wengi wa kipato cha chini kupata shida wakiwamo wa maeneo ya vijijini ambako sukari inauzwa kati ya Sh 3,000 hadi Sh 3,500 kwa kilo moja.

“Serikali inapaswa kuliangalia na kulidhibiti suala la kupanda kwa bei ya sukari kwa sababu wanaoumia ni wananchi wasio na uwezo wa kuinunua, huku wafanyabiashara wakiendelea kuneemeka,” alisema Judith Peter, mkazi wa Soweto.

Nao Anamary Chikota, Joseph Mwakasungura na Sauda Buja wakazi wa jijini hapa, walisema hali imekuwa mbaya na Serikali inapaswa kuingilia kati kwa sababu bei ya kikombe cha chai kwa sasa ni Sh 1,000 badala ya Sh 500 ya awali.

“Ukiangalia mzunguko wa fedha hakuna, maisha ni magumu na bidhaa hii ambayo ni muhimu, nayo bei ndiyo haikamatiki,” alisema Chikota.

Akizungumzia kupanda kwa bei ya sukari, muuza duka la rejareja, mkazi wa Itiji jijini hapa, Rashidi Malusu, alisema wao wanalazimika kupandisha bei ya bidhaa hiyo kutokana na upatikanaji wake kuwa mgumu na kwa gharama kubwa tofauti na kipindi cha nyuma.

“Awali mfuko wa sukari wa kilo 20 tulikuwa tunanunua kwa Sh 44,000 lakini sasa ni Sh 56,000 nao haupatikani kwa mawakala, mfuko wa kilo 50 ndiyo unapatikana lakini kwa bei ya Sh 120,000 badala ya 100,000 na hii ni ile ya kutoka nchi ya jirani ya Malawi, ya Kilombero haipatikani kabisa,” alisema.

Pia alisema ongezeko la bei ya sukari linasababishwa na bidhaa hiyo kuadimika.

Alisema wafanyabiashara wa maduka wanalazimika kupanga foleni kwa kuandika majina kwa mawakala tofauti na kipindi cha nyuma walipokuwa wanachukua kiasi wanachokitaka na kuondoka.

“Mimi leo (juzi) nina siku ya nne bado sijapata sukari kutoka kwa wakala Tughimbe, hata hivyo pindi nitakapoipata itanilazimu kuiuza kwa bei ya juu,” alisema mfanyabiashara wa duka la rejareja wa eneo la Mwanjelwa, Saimon Sanga.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, alisema Serikali imepokea taarifa za kuadimika kwa sukari na inazifanyia kazi na itazitolea ufafanuzi pindi zitakapokamilika baada ya ofisi yake kujiridhisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles