31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Uhaba wa samaki walikumba soko la Feri

AVELINE KITOMARY Na RAHMA SWAI (TSJ)-DAR ES SALAAM     

SOKO la Samaki la Kimataifa la Feri jijini Dar es Salaam limekumbwa na uhaba wa samaki kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanasababisha bei ya bidhaa hiyo kupanda.

Akizungumza na MTANZANIA jana Dar es Salaam, Ofisa Uvuvi wa soko hilo, Ahmed Mbaruku alisema kwa kipindi hiki kumekuwa na uhaba wa dagaa kutokana na mbalamwezi huku samaki wakubwa wakipatikana kwa mshipi.

“Asilimia 90 ya dagaa mchele wanapatikana usiku kwa sababu ya kiangazi, samaki wakubwa tunawapata wachache na wanapatikana kwa mishipi,” alisema.

Mbaruku alisema bei ya samaki imepanda, kwa sasa ndoo ya dagaa mchele inauzwa Sh 8,000 wakati mwanzo ilikuwa Sh 5,000 huku nguru kilo moja ikiuzwa Sh 15,000 kutoka Sh 8,000.

“Kwa upande wa samaki changu kwa sasa anauzwa kwa kilo moja Sh 9,000 kutoka Sh 4,500 hivyo bado kuna uhitaji mkubwa wa samaki,” alisema.

 Mbaruku alisema kumekuwa na uhaba licha ya kupokea samaki kutoka sehemu mbalimbali ikiwamo Kilwa, Mafia, Mtwara, Lindi pamoja na mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo huleta sangara na sato.

Alisema uhaba wa vifaa vya kisasa unachangia uwapo wa uvuvi duni nchini, hivyo aliiomba Serikali iangalie sekta hiyo kwa kuwapatia wavuvi zana bora za kisasa.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa wavuvi wadogo wadogo, Amiri Nsoko aliunga mkono suala la uhaba wa zana za kisasa akisema linachangia upatikanaji mdogo wa samaki kwani wavuvi wengi wanatumia mitumbwi na boti ndogo.

“Licha ya mabadiliko ya hali ya hewa, lakini pia zana zisizoendana na teknolojia ya kisasa zinachangia samaki kuvuliwa wachache.

“Samaki waliopo Bahari ya Hindi wakivuliwa vizuri wanaweza hata kutumika kwa nchi nzima,” alieleza Nsoko.

Naye mmoja wafanyabiashara sokoni hapo, Jafari Miraji, alisema kuwa kwa sasa hali ya biashara si nzuri kutokana na uhaba wa samaki jambo linalochangia kutokuwapo kwa bei maalumu.

 “Wakati mwingine wavuvi wanapokwenda wanarudi hawana kitu, hakuna bei maalumu ya samaki kwa sasa, bei  iko juu. Lakini samaki hawapatikani, hivyo kusababisha biashara kuwa ya kusuasua,” alisema Miraji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles