Na AHMED MAKONGO, BUNDA
KERO ya ukosefu wa maji katika mitaa ya Kata ya Bunda Stoo, wilayani Bunda, mkoani Mara, imesababisha migogoro mingi kwa baadhi ya familia na ndoa zao kuingia matatani kutokana na wanawake kuamka alfajiri kutafuta maji na kukaa huko muda mrefu.
Baadhi ya wanawake wanaoishi eneo hilo walisema kero hiyo imekuwa ikisababisha migogoro mingi katika familia zao, ikiwa ni pamoja na kupewa vipigo na kujeruhiwa na waume zao wakiwatuhumu kuwa na wapenzi wengine.
Walisema mbali ya kupigwa na waume zao, wamekuwa wakitembea mitaa mbalimbali kusaka maji ambapo ndoo moja hununua kati ya Sh 300 hadi 500.
Kilio hicho walikitoa juzi kwa Diwani wa Kata hiyo, Daud Chiruma, aliyetembelea mradi wa uchimbaji wa mitaro kwa ajili ya kulaza mabomba ya maji ili wananchi wa kata hiyo waweze kuondokana na kero hiyo.
Regani Mahindi, ambaye ni balozi nyumba kumi katika Kitongoji cha Kilimani, alisema amekuwa akisuluhisha migogoro mingi ya ndoa eneo lake kutokana na wanawake wengi kupigwa na waume zao.
Alisema baadhi ya kesi anazozisuluhisha ni tuhuma za baadhi ya wanawake kwenda kwa waume wengine wakisingizia walikuwa wanatafuta maji, ambapo aliongeza kuwa, ujio wa maji mtaani kwao ni suluhisho la ndoa nyingi.
“Mimi ni balozi na mwenyekiti wa wana Nzengo, nasuluhisha ndoa nyingi, kwetu utakuta wanawake wamepigwa na wamepewa ngeo na kutolewa meno kwa sababu ya kero ya maji…ndoa zao ziko mashakani,” alisema Mahindi.
Alisema kero hiyo ni ya muda mrefu zaidi ya miaka 10 na kwamba wanamshukuru Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Esther Bulaya, kwa kuwaletea mradi huo.
“Tunaona ni furaha kubwa, ndiyo maana tumeamua kuchimba wenyewe mitaro ili kuondokana na kero hii, tunaamka mapema asubuhi tunashinda huko kwa sababu ya kero hii. Tunamshukuru diwani wetu pamoja na mbunge wetu,” alisema Rosemary Lucas, mkazi wa mtaa huo.
Naye Diwani wa Kata ya Bunda Stoo, Daud Chiruma, alisema wameamua kutekeleza mradi huo kwa sababu waliahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana.