Na ARODIA PETER
-DODOMA
UKISIKILIZA mijadala katika Bunge la bajeti linaloendelea jijini Dodoma utabaini jambo moja, kwamba Serikali ina kazi kubwa kuhakikisha zinapatikana fedha za kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Licha ya baadhi ya wabunge, hususani wa chama tawala (CCM) kusifu utekelezaji wa miradi inayoendelea au iliyotekelezwa na Serikali, bado hairidhishi kwa mujibu wa taarifa za kamati na wabunge wenyewe.
Kwa mfano, taarifa za kamati za kudumu za Bunge kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na ile ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, zinaonesha wazi kwamba kuna changamoto kadhaa zinazosababishwa na ukosefu au upungufu wa rasilimali fedha jambo ambalo limechangia kukwama au kutokukamilika kwa wakati baadhi ya miradi.
MTANZANIA Jumapili limefanya uchambuzi wa michango ya wabunge, kamati pamoja na majibu ya wabunge na mawaziri kwa upande mwingine.
WIZARA YA AFYA
Tukianza na hotuba ya Wizara ya Afya, wabunge wanashauri iongeze vitendea kazi katika hospitali na vituo vya afya nchini ili kuboresha huduma kwa wananchi, hususani wa vijijini.
Mathalani, maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge kwa wizara hiyo yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Peter Serukamba ilisema miradi yote ya maendeleo iliyokuwa imetengewa fedha kwa mwaka 2018/2019 na ambayo waliikagua haikupelekewa fedha yoyote.
Changamoto nyingine iliyoainishwa na kamati hiyo ni upungufu wa watumishi katika sekta ya afya, huku ikitolea mifano hospitali za rufaa za mikoa kwamba karibu zote zinakabiliwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa, upungufu wa wahudumnu wa afya pamoja na madaktari.
Serukamba alitolea mfano Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Dar es Salaam akisema kuna haja hatua za haraka kuchukuliwa ili kupunguza adha hiyo.
Aidha Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM), alishauri Serikali kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma za afya.
“Utaratibu wa ‘Public Private Partnership’ ni utaratibu muhimu sana, naomba uendelee, tunapoboresha hospitali za Serikali tusisahau umuhimu wa kuhakikisha kwamba zile ambazo tulikuwa nazo tunalinda uwezo wake kwa sababu tusije ikawa kama ule msemo wa wazungu unaosema ‘tusimwibie Paulo kumlipa Petro’.
“Hapa inatakiwa ‘balance’ na nitaomba sana waziri anapokuja kwenye majumuisho tusikie mkakati alionao kuhakikisha kwamba hizo hospitali tulizokuwa nazo zinaendelea kufaidika na hii ‘partnership’ iliyokuwepo, la sivyo tunaweza kujikuta kwamba hospitali hizo zinadidimia.
“Mheshimiwa Naibu Spika, sina budi kusema kwamba hospitali si majengo ila ni huduma, na katika hili, waziri pia aangalie hali halisi ya hospitali za ‘referral’ (rufaa), napongeza juhudi za Serikali ya awamu ya nne iliyokamilisha Hospitali ya Mloganzila, lakini hospitali hiyo ni hospitali majengo kwani hakuna ‘hospital town’ pale kwa ajili ya madaktari kukaa karibu na hospitali,” alisisitiza Profesa Tibaijuka.
Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema) alisema hospitalini karibu zote za rufaa hazina mashine za mionzi ya kutibu ugonjwa wa kansa jambo ambalo linachangia vifo vingi kwa Watanzania.
Alisema hakuna haja ya kupandisha hadhi hospitali bila kuwepo vifaa vya kutosha, huku akisema wakuu wa hospitali za rufaa nchini kilio chao kikuu ni kununua mashine za kutibu ugonjwa wa kansa bila kulazimika kwenda hospitali ya kansa ya Ocean Road ya Dar es Salaam.
Katika kuhitimisha hotuba yake, Waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu alisema anazichukua changamoto mbalimbali zilizoainishwa na wabunge na anaamini hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa bajeti ya 2018/2019 fedha za kutekeleza miradi kadhaa zitakuwa zimepatikana.
WIZARA YA UCHUKUZI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Serikali kutafuta fedha za kulipa wakandarasi wazawa ambazo hazikutolewa katika bajeti ya 2018/2019 iliyoidhishwa na Bunge.
Akisoma maoni ya kamati yake, Mwenyekiti Moshi Kakoso alisema kuna ongezeko la fedha za miradi ya maendeleo kwa wizara hiyo kutoka Sh trilioni 4.2 kwa mwaka 2018/2019 hadi Sh trilioni 4.8 kwa mwaka wa fedha ujao 2019/2020.
“Kwa upande wa fedha za miradi ya maendeleo kwa sekta ya mawasiliano, hakuna fedha yoyote iliyotengwa. Hata hivyo kamati ilielezwa kuwa fedha hizo zitatolewa kutoka katika fedha za mkongo wa taifa wa mawasiliano.
“Kamati inasisitiza kuwa ni muhimu fedha hizo zitolewe ili kuendeleza miradi muhimu iliyokuwa inaendelea, kama vile mradi wa anuani za makazi na misimbo ya posta, mkongo wa taifa wa mawasiliano na ujenzi wa kituo cha kutengeneza vifaa vya Tehama,” alisema Kakoso.
Kuhusu bandari, kamati hiyo ilishauri Serikali kubakisha angalau asilimia 40 ya makusanyo ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili ziweze kuendeleza baadhi ya miradi katika bandari zake.
Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Lindi, Riziki Lulida (CUF) alisema kuna ubaguzi mkubwa unaofanywa na mawaziri katika ugawaji wa miradi ya maendeleo.
Bila kuwataja mawaziri hao, alisema: “Barabara ya Liwale tangu enzi za Tanganyika haijawahi kutengewa fedha, na mnajua Waziri Mkuu wa zamani, Rashid Kawawa alikuwa anatokea huko. Kwanini mnashindwa hata kumuenzi mzee wetu huyu, Liwale imegeuka Guantanamo kwanini?
“Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Bunge lako tukufu tutengue kanuni ya kuapa kwa kushika Biblia na Quran kwa sababu vitabu hivi havitaki kusema uongo, tuanze kutumia Katiba,” alisema.
Aidha Lulida alikwenda mbali zaidi kwa kusema watu wa Lindi wanakuwa na maumbo mafupi kutokana na kubeba mizigo ya matenga na kutembea umbali mrefu kwa sababu ya kukosa barabara.
“Mheshimiwa Naibu Spika, hii mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ni ya uchumi mkubwa wa korosho, lakini haipewi barabara, leo mnasema watu wasiuze korosho zao kwa kangomba. Je, wafanyeje wakati hao wanunuzi binafsi ndio wanajitoa muhanga kupeleka magari yao huko kwenda kununua korosho?” alihoji mbunge huyo.
Mwisho
Majaliwa kupokea watalii 343 kutoka China leo
Na ELIYA MBONEA
-ARUSHA
KUNDI la watalii 343 kutoka China linatarajiwa kuwasili nchini leo kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii kwa siku tano.
Watalii hao wanajumuisha watu maarufu, wawekezaji kutoka kampuni 27, waandishi wa habari 40, maofisa wa Serikali ya China na mawakala wa kampuni tatu kubwa za utalii.
Akizungumzia ujio wa watalii hao jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devotha Mdachi alisema kundi hilo litawasili Jumapili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
“Watalii hawa watapokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala, Katibu Mkuu wa Wizara, Professa Adolf Mkenda,” alisema Mdachi na kuongeza:
“Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya TTB, Jaji mstaafu Thomas Mihayo na viongozi wengine wa idara na taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii na wananchi,” alisema.
Aliyataja maeneo ya vivutio watakayotembelea ni Hifadhi ya Taifa ya Manyara, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Olduvai Gorge, maboma ya Wamaasai, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vivutio vya utalii vya Zanzibar ikiwamo Stone Town.
“Ujio huu umetokana na makubaliano ambayo TTB iliingia na Kampuni ya Touch road International Holdings Groups ya China Novemba mwaka jana wakati wa ziara ya kutangaza utalii katika miji ya Beijing, Shanghai, Chengdu, Guangzhou na Hong Kong,” alisema Mdachi.
Alisema mbali ya watalii hao kutembelea vivutio, pia watapata fursa ya kushiriki kongamano la uwekezaji litakalofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Mei 13.
Alisema ni dhamira ya TTB kutangaza utalii katika soko la China kwa kutumia mbinu mbalimbali na kwamba Juni wanatarajia kufanya ziara ya kutangaza utalii katika miji ya Nanjing, Hanzhou na Changsha.
“Tunaishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua kwa lengo la kukuza sekta ya utalii. Kwa jitihada hizi na za wadau wengine wa utalii, tutafikia lengo la watalii milioni mbili ifikapo mwaka 2020,” alisema Mdachi.
Ujio wa watalii hao kutoka China umechukua siku chache baada ya kundi jingine la watalii 1,000 kutoka nchini Israel kutembelea vivutio vilivyopo nchini kwa wiki moja.
Katika hatua nyingine, Mdachi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mtanzania Elizabeth Mwakajila aliyeshinda na kukabidhiwa tuzo ya kimataifa ya utalii nchini Switzerland hivi karibuni.
“Ushindi wa Elizabeth umeiletea nchi yetu heshima kubwa na hususani katika sekta ya utalii,” alisema Mdachi ambaye pia ni mwanachama wa Chama cha Wanawake katika Utalii nchini (AWOTTA).
Kwa upande wake, Elizabeth akielezea ziara yake nchini Switzerland, alisema ushiriki wake katika Jukwaa la Kidunia la Utalii umekuwa wa mafanikio makubwa kwani amechangia kutangaza na kuvisemea vivutio vilivyopo nchini.
“Nimefurahia kurudi na tuzo, niwaombe Watanzania kila walipo wahakikishe wanatangaza vivutio vya utalii kwani itasaidia wageni kuvifahamu na hatimaye kuja,” alisema Elizabeth.