HOSPITALI ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, inakabiliwa na upungufu mkubwa wa damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu hospitalini hapo.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mganga Mkuu wa Hospital ya Mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti, alipokuwa akizungumza katika kikao cha Kamati ya Maafa ya Mkoa, ambapo alisema hospitali hiyo inahitaji uniti 1560 za damu salama, waka akiba ya damu salama iliyopo ni uniti 40 .
Kutokana na upungufu huo, Dk. Frida, aliwataka wananchi na wadau mbalimbali nchini kujitokeza ili waweze kujitolea damu ambayo itaokoa maisha ya wagonjwa.
Alisema upungufu mkubwa wa adamu unasababisha wagonjwa wanaosubiri matibabu yanayotegemea damu salama kuwa katika wakati mgumu ili kuokoa maisha yao.
“Akiba ya damu salama iliyopo ni kidogo sana kuokoa maisha ya wagonjwa ambao matibabu yao yanahitaji damu nyingi, hivyo naomba wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa.
“Mahitaji makubwa ya damu salama yanatokana na wingi wa wagonjwa wanaofika hospitali kwa ajili ya matibabu yao na imekuwa ndiyo tegemeo kwa wagonjwa wa mkoa wetu na mikoa jirani,” alisema.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha (RAS), Anza Ndosa, aliwataka wakurugenzi wa halmashauri za wilaya walifanyie kazi suala hilo kwa kuhakikisha wanahamasisha jamii kuhusu uchagiaji wa damu.