25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

UHABA WA DAMU UNAWATESA WAGONJWA MUHIMBILI

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza na Fransisca Alphone aliyejitolea kuchangia damu.

 

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

JARIBU kutafakari, kwa mfano umelazwa wodini ukisubiri kufanyiwa upasuaji mkubwa kutibu tatizo linalokusumbua mwilini, lakini ghafla anakuja daktari wako na kukuomba radhi.

Anakueleza inabidi uendelee kusubiri wodini kwa siku kadhaa kwani wamelazimika kusogeza mbele tarehe yako ya kufanyiwa upasuaji kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.

Kwamba hospitali imepokea majeruhi wengi ambao wamepata ajali hivi punde na wanalazimika kuwahudumia haraka kuokoa maisha yao.

Anakueleza ingawa wanao uwezo wa kuwapa huduma majeruhi hao na wewe hata hivyo wanalazimika kuahirisha upasuaji wako kwa sababu hakuna damu ya kutosha.

Hapana shaka suala hilo litakusikitisha na kukukatisha tamaa, lakini utalazimika kukubaliana nalo huku ukizidi kumuomba Mwenyezi Mungu akusaidie uweze kufanyiwa upasuaji huo ili uwe na afya njema.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Plaxeda Ogweyo anasema kuna wakati hulazimika kusubirisha wagonjwa wodini kutokana na uhaba wa damu.

“Inajulikana wazi, Muhimbili ni hospitali kubwa nchini ambayo inapokea wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa yote, kuna wakati huwa tunalazimika kusubirisha wagonjwa wodini wale ambao hawahitaji kuongezewa damu ili tuhudumie wale wanaokuwa na uhitaji kwa wakati huo tuweze kuokoa maisha yao,” anasema.

Dk. Ogweyo anasema ili kutosheleza mahitaji ya hospitali hiyo kila siku wanahitaji kukusanya chupa za damu 100 hadi 120 hata hivyo huwa inakusanya chupa 60 hadi 70 pekee.

“Hii ni changamoto kwa kweli, tunao uwezo wa kuhudumia wagonjwa wote lakini inabidi tuanze na wale wanaokuwa wanahitaji huduma ya dharura kwa mfano majeruhi wa ajali ambao huhitaji kuongezewa damu,” anasema.

Dk. Ogwola anasema ili kukabiliana na hali hiyo, huwa wanafanya kampeni za ukusanyaji damu kwa kupita katika shule mbalimbali, vyuo, ofisi za umma na binafsi kuhamasisha wananchi wajitolee damu. 

Hali ilivyo JKCI

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dk. Peter Kisenge anasema uhitaji wa damu katika hospitali hiyo ni mkubwa.

Anasema mara nyingi kwa siku huwa wanafanya oparesheni mbili kubwa za moyo na ili kufanikisha upasuaji huo huhitaji kutumia kati ya chupa tatu hadi tano za damu kwa mgonjwa mmoja.

“Damu ni muhimu katika mwili wa binadamu, ili mtu aweze kuishi anahitaji damu, yenyewe huhitajika kupeleka oksijeni na virutubisho mwilini mwake,” anasema.

Daktari huyo anasema ingawa suala la upatikanaji damu kutosheleza mahitaji ni tatizo, lakini changamoto kubwa ambayo hukabiliana nayo ni upatikanaji wa damu ya watu waliopo kwenye kundi B- na B+.

“Kuna wakati tunapata wagonjwa waliopo katika kundi hili la damu ingawa huwa si wengi, mara nyingi ni kati ya wawili au watatu inapotokea tunakosa damu ya kuwaongezea huwa tunalazimika kuwapigia watu ambao tunawafahamu wapo kundi hilo tunawaomba waje kujitolea damu kusaidia wagonjwa hao, na kwa kuwa wapo tayari kujitolea huwa wanakuja,” anasema.

Anasema kuna kipindi uhitaji wa damu huwa mkubwa zaidi hasa zinapotokea ajali kwani majeruhi huhitaji kuongezewa damu kuokoa maisha yao.

“Siku hizi ajali za bodaboda zimekuwa nyingi mno hivyo, JKCI tunapata shida mno, unakuta tunalazimika kubadili ratiba ya upasuaji ikiwa tulipanga kuwafanyia wagonjwa watano kwa wiki inabidi tuwafanyie wagonjwa watatu tu,” anasema. 

Hali halisi

Ukweli ni kwamba hali ya upatikanaji wa damu nchini bado hairidhishi, kiasi kinachokusanywa kwa mwaka hakitoshelezi mahitaji halisi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza, kila nchi iwe na hifadhi ya damu kwa kiwango cha asilimia moja ya idadi ya watu wake ili kuweza kutosheleza mahitaji yake.

Kwa uwiano huo, Tanzania inapaswa kukusanya chupa za damu 500,000 kila mwaka, lakini Mpango wa Taifa wa Damu Salama nchini haijawahi kufikia kiwango hicho cha ukusanyaji wa damu nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema takwimu za ripoti ya mwaka 2016 zinaonesha kwa mwaka jana pekee jumla ya chupa za damu 196,735 zilikusanywa kwa kipindi cha Januari mpaka Desemba.

“Ingawa inaonesha kuongezeka kwa makusanyo ya damu zaidi ya mara tatu ikilinganishwa na chupa za damu 65,000 ambazo zilikusanywa mwaka 2015, hata hivyo bado ni changamoto,” anasema.

Anasema mahitaji ya damu ni makubwa nchini hasa kwa kundi la wanawake ambao wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa kuvuja damu nyingi hasa wakati wa kujifungua.

“Iwapo kungekuwa na akiba ya kutosha ya damu, wanawake wengi wasingepoteza maisha yao kwa kukosa damu, kufariki kwa kukosa damu ni kifo ambacho kinaweza kuzuilika.

“Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha, takribani wanawake 556 kati ya vizazi hai 100,000 hufa kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi nchini, inakadiriwa asilimia 40 ya vifo hivyo vingeweza kuepukika kama kungekuwa na akiba ya kutosha ya damu salama,” anasema.

Anasema Juni 14, kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Wachangiaji Damu Duniani kwa lengo la kuhamasisha jamii ijitolee damu kwa ajili ya kusaidia wengine.

“Siku ni ukumbusho wa siku ya kuzaliwa Karl Landsteiner, huyu ndiye aliyegundua mfumo wa makundi ya damu ambayo ni kundi A, B na O na alizawadiwa tuzo ya Nobel kutokana na ugunduzi huo,” anabainisha.

Waziri Ummy anasema maadhimisho ya mwaka huu yalipewa kauli mbiu isemayo, ‘Changia damu Changia sasa na Changia mara kwa mara.

“Kauli mbiu hiyo imelenga kuhamasisha uchangiaji damu ili kukabiliana na dharura inayoweza tokea ya uhitaji wa damu, kila mwananchi mwenye vigezo vya kuchangia damu anakumbushwa kujenga utamaduni wa kuchangia damu mara kwa mara ili Taifa liwe na akiba ya kutosha ya damu,” anasema.

Anasema Wizara kwa kutumia wataalamu wake itaendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari na kutoa rasilimali watu na fedha ili Mpango wa Taifa wa Damu Salama uweze kutimiza majukumu yake na hatimaye kupunguza vifo ambavyo vinaweza kusababishwa na ukosefu wa damu.

“Ndiyo maana serikali imeongeza kiwango cha fedha kwenye bajeti  ya mwaka 2017/18, kiasi cha Sh bilioni 5.5 zimetengwa kwa ajili ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama kutoka Sh 4.5 bilioni zilizotengwa mwaka 2016/17,” anafafanua.

Anaongeza: “Pamoja na hatua hizo, ni vema halmashauri zote nchini zitenge bajeti kwa ajili ya kununulia vifaa vya kukusanyia damu, kila mkoa na halmashauri inapaswa kuhakikisha hospitali zake zinakuwa na damu salama wakati wote.

“Viongozi wa mikoa na halmashauri waweke utaratibu wa  kukusanya damu kutoka kwa wachangia damu wa hiari na kuacha  tabia ya kutegemea kupata damu toka kwa wachangia damu wanandugu ( Family replacement donors).

“Wanandugu kuchangia damu uwe ni utaratibu wa dharura ambao wakati mwingine si salama kwani ndugu hulazimika kuchangia damu hata kama hawana vigezo vya kuchangia damu,” anasema.

Anaongeza: “Ili kuendelea kuwapo ubora wa damu inayokusanywa, sampuli zote zitumwe katika vituo vya kanda vya Mpango wa Taifa wa Damu Salama ili zipimwe katika ubora na viwango vinavyotakiwa  ( Quality assured manner). 

Umuhimu wa damu mwilini

Wanasayansi wanaeleza kwamba ili mnyama na binadamu waweze kuishi wanahitaji damu, damu ni tishu inayopatikana katika mwili wa binadamu na manyama ambayo huzunguka mwilini ndani ya mishipa ya damu ikisukumwa na moyo kwa lengo la kumuwezesha kuishi.

Wanataja kazi kuu ya damu kuwa ni kupeleka lishe na hewa ya oksijeni katika seli za mwili na kutoa hewa ya kaboni daioksaidi pamoja na taka zingine kutoka kwenye seli hizo.

Wanafafanua kwamba ndani ya damu kuna ute-gili (plasma) na seli za damu nyeupe na nyekundu. Kazi kuu ya seli nyekundu za damu ni kubeba hewa ya oksijeni.

Wanasema kazi ya ute-gili ni kubeba hewa ya kaboni dioksaidi. Wakati seli hai nyeupe za damu zenyewe hufanya kazi kama walinzi wa mwili wa kupambana na magonjwa na zipo pia chembe sahani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles