Ugonjwa wa moyo waongezeka asilimia tatu nchini

0
644

AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema matatizo ya ugonjwa wa moyo yameongezeka na kufikia asilimia tatu.

Kutokana na hali hiyo, ameipongeza Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuendelea kuboresha                                                huduma za upasuaji wa moyo nchini.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam, wakati akizindua kambi ya upasuaji wa moyo kwa watoto 10, iliyoanza Septemba 13 hadi 20, mwaka huu.

Kambi hiyo ni mpango wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwapatia matibabu ya moyo watoto 60 wanaotoka katika kaya masikini katika kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka huu. 

“Kambi hii ninayoizindua leo (jana) inaitwa Small Heart Mission, inadhaminiwa na wenzetu kutoka Falme za Kiarabu chini ya uratibu wa Islamic Foundation, JKCI ni moja ya taasisi ambayo iko chini yangu, inafanya vizuri.

“Mwaka 2015 walikuwa wanafanya upasuaji kwa wagonjwa 624 na mwaka 2018 wagonjwa walikuwa 2,056. Tukiangalia  idadi ya wagonjwa, kuna ongezeko la watu asilimia 3.                                                                                                                                        “Chini ya uongozi wa Profesa Janabi, mwaka 2015 na leo (jana) 2019, tulikotoka yapo mafanikio makubwa.

“Mwaka 2015 upasuaji ulikuwa unafanywa na wataalamu wa ndani kwa asilimia 35, kwahiyo labda kwa wagonjwa 100 ni wagonjwa 35 tu wanafanyiwa upasuaji tofauti na leo kati ya wagonjwa 100 wagonjwa 90 wanaweza kufanyiwa upasuaji,” alisema.

Ummy alisema hali hiyo imefanya idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa nje kupungua, huku asilimia 95 wakitibiwa ndani ya nchi.

“Zamani wagonjwa wengi walikuwa wanapelekwa nje ya nchi. Ukimpeleka mgonjwa mmoja unatumia gharama ya Sh milioni 100, nikawaambia lazima tujenge uwezo wa ndani, sasa tumepunguza rufaa za nje kwa asilimia kubwa.

“Tunapata wagonjwa kutoka nchi za jirani kama Rwanda, Malawi, DRC na tunaamini tutaendelea kupata wagonjwa kutoka nchi nyingine,” alisema Ummy.

Kutokana na mpango huo, alimpongeza Mkuu wa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda kwa jitihada zake binafsi za kuhakikisha watoto kutoka kaya masikini kupata matibabu ya moyo.

Hata hivyo, alisema kuwa kati ya vifo 100 vinavyotokea hospitalini, 34 vinasababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, huku ugonjwa wa moyo ukishika nafasi ya pili.

“Ugonjwa wa rubella unasababisha watoto kuzaliwa wakiwa na matatizo ya moyo endapo mama mjamzito ataathirika na ugonjwa huo.

“Hivyo nawashauri wazazi au walezi kuwapeleka watoto kupata chanjo ya surua rubella kwani hali hii itasaidia kuepusha matatizo ya magonjwa ya moyo kwa watoto,” alisema

Pia Ummy aliwasisitiza wananchi kukata bima ya afya kwani itawasaidia katika kupata matibabu bila kuhofia gharama.

“Narudia kusema matibabu ni gharama, milioni tano ni gharama ya chini, hivyo mzazi mkatie bima mtoto ni Sh 50,400 tu.

“Nashangaa baadhi ya watu wanavyosema ni masikini wakati hela za ‘Kitchen Party’ wanazo, wana hela za kukodisha matarumbeta, hivyo watu wabadilike, wapeleke hela hizo kukata bima,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda, alisema kuwa kati ya Novemba na Desemba  mwaka huu atafanya kampeni za kuchangisha Sh bilioni moja ili kuwezesha matibabu ya moyo kwa watoto walioko JKCI.

“Nitapita kwa wadau mbalimbali wakiwamo mabenki, wale wenye malori na marafiki zangu wengine ili kuhakikisha tunapata kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya watoto.

“Mimi na balozi wa Falme za Kiarabu pia tuna mpago wa kuwawezesha watoto wadogo 500 waliofanyiwa upasuaji hapa kupata bima za afya, wakiwamo hawa watoto 60 kwani wanatakiwa waendelee na kliniki,” alisema.

Balozi wa Falme za Kiarabu hapa nchini, Abdulrahman Marzooqi,  alisema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kuboresha huduma za afya, hasa katika Taasisi ya JKCI.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here