24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ugonjwa wa kisukari waongoza kupoteza viungo

GLORY LYAMUYA (DSJ) Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

UGONJWA wa kisukari unaelezwa kuwa unaongoza kutesa mamia ya Watanzania huku wengi wao wakijikuta wakipoteza viungo na kuhitaji vifaa tiba saidizi.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Vifaa Tiba Saidizi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dk. Leah Mamseri,  alisema idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika katika kitengo hicho kwa sasa kuhitaji viungo bandia ni wagonjwa wa kisukari.

Alisema ugonjwa huo unaongoza baada ya kudhibitiwa kwa ajali za barabarani ambazo awali ndizo zilikuwa zikiongoza.

“Idadi kubwa ya wagonjwa wenye kuhitaji vifaa saidizi vikiwamo viungo bandia ni wale wenye kisukari baada ya kudhibitiwa ajali za barabarani,” alisema Dk. Leah.

Alisema sababu nyingine inayosababisha watu kuhitaji vifaa saidizi ni kupooza kutokana na baadhi ya mishipa ya fahamu kupoteza uwezo wake wa kufanya kazi.

“Kuna watoto wanaozaliwa wakiwa na upungufu wa viungo, ajali za moto na za viwandani, kuumwa na nyoka, nazo huchangia kuhitaji vifaa tiba,” alisema Dk. Leah.

Aliwashauri waliopoteza viungo vyao kutokata tamaa ya maisha bali wafike hospitalini kupatiwa viungo saidizi  waendelee na maisha yao kama ilivyokuwa awali.

“Niwashauri Watanzania kubadili mfumo wa maisha yao kwa kula vyakula vya asili na kufanya mazoezi   kuepuka wagonjwa ya kisukari na kupooza,” alisema.

Wakati huohuo, Dk. Leah  amewataka watu wenye mahitaji ya viungo saidizi   kujiorodhesha hospitalini hapo  waweze kupatiwa viungo hivyo bure na Taasisi ya BMVSS kutoka India.

Alisema taasisi hiyo itaweka kambi nchini na kuwapatia viungo na vifaa saidizi watu 600.

“Niwaombe wenye mahitaji wajitokeze kujiorodhesha wapatiwe huduma hii bure kwa sababu  bima hazina mafao yanayoweza kulipia viungo hivi,” alisema Dk. Leah.

DALILI ZA KISUKARI

Watu wenye kisukari wapo katika hatari zaidi ya kupatwa na magonjwa ya moyo, kiharusi, matatizo na kuharibika   kibofu cha mkojo, shinikizo la juu la damu, upofu, kufa neva za fahamu, uharibifu katika fizi na ugonjwa wa fangasi.

Mtu anapokuwa na kisukari, mzunguko wa damu miguuni hupungua na ndiyo sababu kubwa ya kufa neva za fahamu na hivyo mtu kukosa hisia katika eneo hilo la mwili.

Matokeo ya hali hiyo ya kutohisi punde mtu anapodhurika na kusababisha kidonda ambacho mara nyingi mhusika anakuwa hafahamu hadi anapofahamishwa na mtu wa karibu au atakapokagua miguu yake.

Hii ni moja ya sababu kubwa ya watu kushauriwa kukagua miguu yao kila siku kabla ya kulala kuona kama kuna mchubuko wa aina yoyote au ukucha unaoweza kuchimba ngozi.

Kutokuzingatia masharti ya kujikagua huweza kusababisha kidonda kukua, kutotibika na hatimaye mgonjwa kuishia kupoteza kidole, unyayo au hata mguu.

JINSI YA KUZUIA

Vile vile, kutokuzingatia masharti ya kujua kiwango cha sukari mwilini huweza kusababisha mtu akapoteza fahamu kutokana na mwili kuzidiwa sukari asidi (diabetic ketoacidosis), na hii huweza kusababisha kifo.

Mgonjwa anaweza kuzuia madhara yatokanayo na kisukari kwa kuzingatia maelekezo, masharti na ushauri wa wahudumu wa afya, hasa kuhusu chakula na mazoezi na maelekezo ya matumizi  sahihi ya dawa au insulin.

Mgonjwa hatakiwi kuvuta sigara, awe anapima kiwango chake cha shinikizo la damu mara kwa mara na kuhakikisha kiwango chake cha lehemu kipo katika uwiano unaotakiwa.

Takwimu zinaonyesha   uzingatiaji wa hayo yaliyotajwa umesaidia watu wengi kupunguza madhara ya kisukari kwa asilimia 75.

Lishe mahsusi kwa mtu mwenye kisukari ni mlo wenye kiwango kidogo  cha mafuta, kiwango kidogo cha chumvi na kiwango kidogo cha sukari.

Mlo uwe na mchanganyiko wa nyuzinyuzi kama vile dona (unga wa mahindi yasiyokobolewa), nafaka, tambi, ndizi za kupika, mtama, uwele.

Vile vile matunda machachu na mboga za majani zinazolimwa na zile za porini zinazoliwa kama mchunga, tembele, majani ya maboga, majani ya kunde na mbilimbi.

Ni vema kujitahidi kula kiasi kidogo cha chakula walau mara tano kwa siku kuliko mlo mkubwa mara mbili au tatu kwa siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles