25.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Uganda yamjia juu Rais Trump

KAMPALA, UGANDA

MSEMAJI wa Serikali ya Uganda, Ofwono Opondo  amesema kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump anapaswa kutatua matatizo ya taifa lake badala ya kuingilia masuala ya hapa.

Opondo alikuwa akijibu ujumbe wa Rais Trump katika mtandao wa Twitter, ambao ulisema watu hawatatamani kwenda Uganda hadi pale watekaji nyara wa raia wa Marekani, Kim Sue Endicott pamoja na mwongozaji wake, Jean-Paul Mirenge raia wa Congo watakapokamatwa.

Watekaji waliowakamata wawili hao kwa mtutu wa bunduki walikuwa wakidai kulipwa dola za Marekani 500,000 sawa na zaidi Sh bilioni moja.

Opondo alijibu kupitia mtandao wa Twitter akisema kuwa kuna vifo vingi vinavyotokana na matumizi ya bunduki nchini Marekani kulinganisha na tukio la nadra la utekaji nyara Uganda.

Aliongezea kuwa Uganda itaendelea kuimarisha hali yake ya usalama.

Awali kufuatia utekaji nyara wa wawili hao, Rais Trump alisema kitendo hicho huenda kikaathiri utalii nchini Uganda, akiongezea kuwa watekaji hao ni sharti wakamatwe kabla ya Wamarekani kuzuru taifa hilo.

Awali Rais Yoweri Museveni alikuwa ametuma ujumbe wa Twitter akisema kuwa taifa lake liko salama kwa raia wa Uganda na watalii huku akiwalaumu wahalifu wachache kwa visa kama hivyo.

Wawili hao walitekwa wakati walipokua wakitembea katika mbuga ya Malkia Elizabeth jioni ya Aprili 2.

Operesheni ya pamoja ya utafutaji iliyofanywa na wanajeshi, mamlaka ya wanyampori Uganda na kitengo cha polisi wa utalii ilianzishwa ili kumuokoa Endicott na Mirenge.

Vyombo vya habari vya nje vilisema kuwa wawili hao waliachiwa Jumapili baada ya fedha za kuwakomboa kulipwa kwa watekaji.

Lakini msemaji wa serikali alituma ujumbe wa Twitter kuwa waliokolewa na vikosi vya Serikali ya Uganda nchini Jamhuri ya Kidemokerasia ya Kongo (DRC) na kwamba walikuwa salama salimini mpakani mwa DRC na Uganda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,784FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles