31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

UGAIDI, UTEKAJI NYARA TISHIO AFRIKA MASHARIKI

Na MARKUS MPANGALA,

USALAMA wa raia katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki ni jambo linalopaswa kutiliwa mkazo katika kipindi hiki na kijacho kutokana na matukio mbalimbali yanayoashiria kuziweka nchi hizo katika mtanziko. Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Sudan kusini, Rwanda na Burundi.

Takwimu za idadi ya watu na makazi kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonyesha nchi za Afrika Mashariki zina jumla ya watu milioni 144. Asilimia 62 ya wananchi wa eneo hili ni vijana wenye umri chini ya miaka 25.

Tunafahamu kuwa Somalia na Sudan Kusini zilikuwa nchi za mwisho kuomba uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Bahati iliangukia kwa Sudan kusini pekee ndiyo ilikidhi vigezo, huku Somalia ikiambiwa ihakikishe kwanza kigezo nambari moja cha ulinzi na usalama wa ndani kinatekelezwa.

Somalia ilinyimwa uanachama sababu ya ukosefu wa ulinzi na usalama. Pia iliambiwa inakabiliwa na imekuwa tishio ndani ya nchi kwa hiyo matatizo yake hayakutakiwa kuhamishiwa kwenye Jumuiya hiyo.

Aidha, tunafahamu kuwa Kamati ya Usalama wa nchi za Afrika (Committee of Intelligence and Security Services of Africa -CISSA) ilikutana kwenye mkutano wa masuala ya usalama huko Khartoum nchini Sudan hivi karibuni.

Nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa wanachama wa Umoja wa Afrika, hatua ambayo inamaanisha kuwapo kwa tishio la uhalifu, ugaidi na utekaji nyara.

Takwimu za Kamati ya CISSA inayoundwa na wanachama 51 wa Umoja wa Afrika, ambapo inawahudumia watu bilioni 1 wanakabiliwa na hatari  tano katika nchi zao ikiwemo tishio la ugaidi, utekaji nyara na kupotea kwa baadhi ya raia au watu maarufu.

Miongoni mwa matukio yanayodhihirisha sababu ya ukosefu wa usalama ndani ya Somalia, ni la hivi karibuni la kuuawa kwa kupigwa risasi Waziri wa Kazi na Marekebisho ya Umma, Abbas Abdullahi Sheikh Siraji, akiwa na umri wa miaka 32.

Sehemu kubwa ya maisha yake Waziri Abbas alikulia kwenye kambi za wakimbizi huko Dadaab nchini Kenya kutokana na hali ya kisiasa, ulinzi na usalama wa Somalia. Hata hivyo, tishio hilo limeibuka kwenye nchi nyingine ambazo ni wanachama wa EAC.  

RWANDA

Taifa hili liliwahi kukumbwa na machafuko ya kisiasa ambayo yalisababisha vita ya kikabila kati ya Wahutu na Watutsi mwaka 1994. Makabiliano baina ya makabila hayo yalichochea uhasama mkubwa kabla ya kumpa Rais Paul Kagame ambayo anaonekana kuidhibiti nchi hiyo kwa mkono wa chuma.

Mei 11, mwaka huu mwanachama wa Chama cha Upinzani cha  United Democratic Forces party (FDU) ambacho kimepigwa marufuku, Jean Damascene Habarugira, ameuawa ikiwa imebaki miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi la Polisi, Theos Badege, alisema mwili wa Jean Damascene Habarugira aliyetoweka kwa siku tatu kabla, ulipatikana Jumatatu wiki hii umbali wa kilomita 60 kutoka jijini Kigali.

Makamu wa Rais wa Chama cha FDU, Boniface Twagirimana, aliliambia gazeti la mtandaoni la News24 la nchi hiyo kuwa  Habarugira mwenye umri wa miaka 52 ameuawa kwa sababu za kisiasa hususani upinzani wake dhidi ya Serikali katika sera za kilimo huko Kijiji cha Ngoma, Mashariki ya Rwanda.

“Tunatangaza haya ni mauaji. Mwanachama wetu alitoweka kwa muda wa siku tatu mara baada ya kukutana na askari wa zamani anayehusika na kulinda katika kijiji chake,” alisema Badege.

Aidha, alibainisha kuwa mtuhumiwa wa tukio hilo ni Bizama Theophile ambapo uchunguzi unaendelea tangu Habarugira alipotoweka.

Chama cha FDU kinaongozwa na mwanasiasa Victoire Ingabire ambaye anatumikia kifungo cha miaka 15 jela kwa makosa ya uchochezi na kugawa watu kwa misingi ya ukabila.

Ingabire kutoka kabila la Wahutu alikamatwa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2010, ambapo alikuwa akiwania urais dhidi ya Paul Kagame.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Paul Kagame anagombea muhula wa tatu, kutokana na mabadiliko ya kikatiba yaliyofanyika mwaka jana.  

Matukio ya mauaji, kutoweka kwa watu na utekaji nyara yamekuwa tishio na kusababisha hofu miongoni mwa raia. Mnamo Julai 13, mwaka 2010, Makamu wa rais wa zamani wa Chama cha Democratic Green Party (DGP), Andre Kagwa Rwisereka ambaye ni mzaliwa Mji wa Butare nchini Rwanda alitekwa na baadaye mwili wake kukutwa umetenganishwa na kichwa.

Machi 26, mwaka jana, mwanaharakati Illuminee Iragena alitekwa nyara na watu wasiofahamika. Mwanamama huyo alitekwa nyara akiwa njiani kuelekea kazini. Hajulikani mahali alipo hadi leo, hali ambayo inazidi kutishia usalama wa Rwanda.

Aidha, mgombea huru wa urais nchini Rwanda, Diane Rwigara, amewahi kuguswa na suala la utekaji nyara baada ya rafiki yake wa karibu kutekwa miezi minne iliyopita mwaka huu na hajaonekana hadi leo.

TANZANIA

Inakaribia kutimiza nusu mwaka sasa tangu kupotea kwa Bernard Saanane au maarufu kama Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Maswali yanayoulizwa na Watanzania hadi leo hii; Kuna nini? Wanachukuliwa na nani na wako wapi? Kwanini wapoteaji ni wale wa kuwasema watu wa aina fulani tu? Yuko wapi Ben Saanane?

Mwingine aliyetekwa ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Ibrahim Mussa maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki kabla ya  siku nne baadaye kuonekana. Jeshi la Polisi liliutangazia umma kuwa hakujulikani alipo ingawaje simu zake zilikuwa hewani.

Kupatikana kwa miili ya watu kwenye mifuko ya Sandarusi huko wilayani Bagamoyo, kumezusha hofu miongoni mwa wananchi, huku wakijiuliza ni kitu gani kinachoendelea katika usalama wao.

Aidha, matukio ya mauaji huko mkoani Pwani katika maeneo ya Kitibi, Mkuranga na Ikwiriri yameacha doa kubwa na hofu miongoni mwa wananchi.

Katika kutafuta ufumbuzi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, akiwasilisha bajeti ya Wizara yake, amesema Jeshi la Polisi linatarajiwa kuanzisha Mkoa wa Kipolisi katika maeneo ya Kibiti, Mkuranga mkoani Pwani ili kudhibiti matukio yote  ya uhalifu dhidi ya wananchi.

Wataalamu wa masuala ya ulinzi na usalama wanataja kuwa aina ya mauaji yanayofanyika huko mkoani Pwani yanaashiria kutendwa na watu wenye uzoefu katika matukio hayo. Kwa hali hiyo hili ni tishio la dhahiri kwenye usalama wa nchi yetu.

KENYA

Hivi karibuni vyombo vya usalama vya Kenya vimetahadharishwa juu ya uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

Msemaji wa Jeshi la polisi nchini Kenya, George Kinoti, alisema tayari kumesambazwa taarifa kwamba magaidi tisa wanafanya kila linalowezekana kutekeleza mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

Magaidi wamekuwa wakifanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Serikali huko Kenya baada ya kupata pigo mbele ya wanajeshi. Kundi la kigaidi la Al Shabab lenye makao yake nchini Somalia limekuwa likifanya mashambulizi na hujuma mbalimbali katika ardhi ya Kenya; jambo linalowatia wasiwasi wananchi na viongozi wa Serikali.

Aidha, wiki iliyopita wanamgambo 15 wa kundi la kigaidi la Al Shabab waliuawa katika mapigano na wanajeshi wa Kenya katika eneo la Gedo kusini mwa Somalia. Eneo hilo ni la mpaka wa pamoja kati ya nchi za Somalia na Kenya. 

Kwa upande mwingine, mauaji kiholela kupitia kikosi maalumu cha Flying Sqaud, yamekuwa tishio kwa usalama wa wananchi katika ardhi ya Kenya. Kikosi hicho ambacho kiliundwa kukabiliana na uhalifu kimetajwa kuua watu wanaodaiwa kuwa majambazi na kutelekeza miili yao maeneo mbalimbali mitaani.

Wakati Kenya inaingia kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu, suala la usalama wa raia limekuwa mtambuka kwa kila rika. Ni suala ambalo limeongeza shinikizo na joto la uchaguzi mwaka huu kati ya wagombea 18 wa nafasi ya urais.

BURUNDI

Mauaji kiholela yametamalaki nchini Burundi. Nchi hii ilishuhudia wabunge wake wa Afrika amshariki (EALA) wakishindwa kusafiri nchini humo mapema Februari mwaka huu kutokana na hali mbaya ya usalama.

Aidha, Burundi ilishindwa kuchukua kijiti cha uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na hali mbaya ya usalama. Machafuko na jaribio la mapinduzi dhidi ya Serikali ya Burundi ni jambo linalotishia usalama wa raia na mali zake.

Mapema Januari mwaka huu, Jeshi la Polisi nchini Burundi lilimkamata mwanamke mmoja akimtuhumu kuhusika na mauaji ya Waziri wa Mazingira, Emmanuel Niyokuru. Polisi ilisema mwanamke aliyekamatwa alikuwa na waziri huyo kwenye gari wakati wa mauaji. Mauaji ya Kiyokuru ni mojawapo ya matukio yaliyokithiri nchini humo ambapo majenerali kadhaa waliuawa kutokana na ghasia za kisiasa zinazoendelea.

Takwimu zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2015, ambapo hadi sasa watu 500  wameuawa na wengine 300,000 wameyakimbia makazi yao tangu Rais Pierre Nkurunziza kutangaza, kuwania na kushinda muhula wa tatu, licha ya kuzuiwa na katiba ambayo inaweka ukomo wa vipindi viwili.

UGANDA

Mwanzoni mwa wiki hii, kiongozi wa kambi ya upinzani nchini Uganda, Dk. Kizza Besigye, alikamatwa na maofisa wa Jeshi la Polisi kwa madai ya kuvunja sheria za nchi hiyo.

Machi 17, mwaka huu Inspekta Jenerali Msaidizi wa Polisi, Andrew Felix Kaweesi, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mjini Kampala, Uganda katika tukio lililowashtua wengi na kumlazimu Rais Yoweri Museveni kuagiza kamera ziwekwe katika miji yote mikubwa nchini humo.

Kaweesi alikuwa mmoja wa maofisa wa juu kabisa wa polisi katika taifa hilo.

Watu wengine waliouawa kwa mtindo huo, Joan Kagezi, mwendesha mashtaka mwandamizi alipigwa risasi barabani na muuaji akatoroka pamoja na mshirika wake kwenye pikipiki.

Novemba mwaka jana, ofisa wa Jeshi la Uganda, Meja Muhammad Kiggundu, muasi wa zamani wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) alipigwa risasi na kuuawa akiwa katika gari lake na watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki mbili. Uhalifu wote huo bado haujapatiwa jawabu.

Matukio ya kuuawa kwa watu mbalimbali yamezua mtafaruku miongoni mwa wananchi na kuliona eneo la Afrika Mashariki kama lenye tishio kubwa kwa usalama wa raia na mali zao.

KIKOSI CHA EASF KUNUSURU?

Njia inayotakiwa kufanyiwa kazi kwa sasa ni kutafuta ufumbuzi wa matukio yote yenye kuleta tishio katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Nchi 10 za mashariki mwa Afrika zimeunda kikosi cha pamoja cha kijeshi kitakachofahamika kama East Africa Standby Force (EASF).

Hafla ya kuzindua rasmi kikosi hicho ilifanyika Nairobi nchini Kenya. Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Kenya (KDF), Samson Mwathethe, alisema kikosi hicho cha kieneo kinazijumuisha nchi za Kenya, Burundi, Visiwa vya Comoro, Djibouti, Ethiopia, Rwanda, Ushelisheli, Somalia, Sudan na Uganda.

Amesema nchi wanachama wa kikosi hicho cha kieneo (EASF) kadhalika zimezindua Mfuko wa Amani ambao una hazina ya takriban Dola milioni moja za Marekani zitakazotumika katika operesheni zake za kijeshi.

Kikosi hicho cha kikanda kimeanza kazi rasmi kujiunga na vikosi vingine vinne vya kieneo vilioundwa na jumuiya za kiuchumi za Ecowas, Eccas, Sadc na Sekritariati ya EASF iko katika mtaa wa Karen jijini Nairobi. Aidha, makao makuu ya kilojistiki ya kikosi hicho cha kieneo yakiwa katika Mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Kikosi hiki kwa sasa kina wanajeshi wake wanaofanya kazi chini ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Somalia (AMISOM) na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS).

Azma ya kuwa na kikosi kimoja cha kijeshi barani Afrika ilizaliwa mwaka 2002, katika mkutano wa Umoja wa Afrika, mjini Durban nchini Afrika Kusini, kwa shabaha ya kukomesha utegemezi wa vikosi kutoka nje ya bara hilo.

Na kwa kuwa eneo la Afrika Mashariki limekumbwa na hali ya sintofahamu kutokana na matukio ya utekaji nyara na ugaidi hivyo kuwa tishio, swali kubwa linaloulizwa hapa ni kwa namna gani kikosi hiki kitaweza kurejesha amani na mioyo ya wananchi? Ni kwa muda gani eneo hili litakuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles