24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ufugaji nyuki kisasa una faida zaidi,hutunza mazingira

Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero, Oscar Kunambi (aliyechuchumaa kushoto) akisaidiana na mwanakikundi cha Dakawa Green Voices, Neema Obeid, kuweka vizuri mzinga.
Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero, Oscar Kunambi (aliyechuchumaa kushoto) akisaidiana na mwanakikundi cha Dakawa Green Voices, Neema Obeid, kuweka vizuri mzinga.

Na Sidi Mgumia, Mvomero

Mariam Bigambo ni miongoni mwa akinamama 15 waliopatiwa mafunzo nchini Hispania mwanzoni mwa mwaka huu na wanatekeleza kwa vitendo mradi wa Green Voices, ambao umelenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mradi huo unafadhiliwa na Taasisi ya Wanawake wa Afrika lenye makao yake Makuu jijini Madrid nchini Hipsnia, na lengo lake kuu ni kufanikisha nufaiko kubwa kwa wanawake wengi wa Mvomero, Morogoro.

Taasisi hiyo inayoshughulika na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Women for Africa Foundation inaongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega Sanz.

Kwa kupitia akina mama zaidi ya 20 wa kikundi cha akina mama kinachoitwa Dakawa Green Voices Women Group wameamua kuingia kwenye ujasiriamali wa ufugaji wa nyuki kwa malengo makubwa mawili ambayo ni kupata fedha kutokana na mazao ya nyuki pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Mariam ambaye ndiye kiongozi wa kikundi hicho, anasema kwa muda mrefu sasa misitu imekuwa ikiteketea kwa shughuli za kukata mbao na kuchoma mkaa pia kilimo, na mbaya zaidi wakata miti hao huwa hawapandi mingine kwa ajili ya kuifanya iwe endelevu.

Kikundi hicho kinafanyia shughuli zake katika eneo ambalo lina umbali wa kilometa 10 kutoka Kijiji cha Dakawa ambako kuna kitongoji cha Magogo kilichoko msituni mahali ambapo akina mama hao wametundika mizinga yao.

Anasema lakini kwa kuanzisha ufugaji wa kisasa wa nyuki, hawako tayari kuona watu wakikata miti hovyo kwani wanaihitaji sana na haswa kwa umuhimu wa ufugaji wa nyuki.

Ufugaji wa nyuki wa kisasa ni ule unoazingatia matumizi ya vifaa bora ambao huzalisha asali bora lakini pia mafunzo ambayo yanamsaidia mfugaji kujua nyuki wanaofaa kufungwa kwa ajili ya asali kwani wapo ambao ni maadui na hawafai kufugwa kwani hata asali hawatoi.

Mariam anaongeza kuwa kuna aina mbili ya ufugaji ambao ni ule wa mizinga ya asili kwa kutumia magome na magogo ambao kwa sasa haushauriwi sana. Pia kuna ufugaji wa mizinga ya kisasa ambao wao wanautumia na muda si mrefu watajenga mabanda kwa ufugaji wa kisasa zaidi.

Mama Bigambo anasema kwamba, ufugaji huo unahitaji kutunza mazingira ili kuwawezesha nyuki kupata chakula chao hasa nekta na maji, hivyo ni vizuri kuhakikisha mazingira yanakuwa salama.

“Kupitia chama chetu hapa Mvomero, kitasaidiana na Serikali katika kutatua Changamoto zinazowakabili wafugaji Nyuki na wadau wengine wa sekta ya nyuki nchini,” anasema Mariam

Pia anasisitiza kuwa ukuaji wa Sekta ya Nyuki utategemeana na juhudi binafsi za wafugaji nyuki, wadau wa sekta ya ufugaji nyuki kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania pamoja na taasisi nyingine nchini zinazojihusisha na suala la ufugaji nyuki.

“Ili uweze kufanya vizuri katika shughuli hizi ni vyema kuwe na mafunzo ufugaji nyuki kwa wadau, vitendea kazi na soko la uhakika bila kusahau kufuga nyuki ili kutunza misitu na mazingira kwa kizazi cha sasa na baadae,” alisema Mariam

Mariam anasema utunzaji wa mazingira na haswa miti yenye misitu ni vyema ukiangaliwa kwa umakini kwani kutunza mazingira hata hao wanaokata mkaa na wanaotafuta mashamba watajuta baadaye kwa kuwa miti itakwisha na kubaki na jangwa ambao halitatoa mazao tena.

Akizungumzia umuhimu na faida za nyuki, Mariam anasema kuwa licha ya kusaidia kutunza mazingira, lakini nyuki ni muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai vyote, kwani ndio wanaofanya uchavushaji wa mimea.

Anazitaja faida za ufugaji nyuki kuwa ni kupatikana kwa asali na nta, mazao ambayo yana faida kubwa hata katika soko la kimataifa. Lakini pia dawa ya kifua, kutibu vidonda vya kuungua na moto, aliyevunjika mguu kuunga mfupa, utunzaji wa vyakula mfano uokaji wa mikate pia viwanda kutengenezea peremende.

Kwa upande mwingine mama huyu anawapongeza wanawake wa Green Voices, Mvomero kwa juhudi zao katika uzalishaji huu kwani kwa muda mrefu sasa ufugaji nyuki umekuwa ukifanywa na wanaume lakini sasa hata wanawake wanazifanya tena kwa ustadi mkubwa.

Kwasasa wana heka nne na matarajio yao ni kuwa na mizinga 4000,na kwakupitia ufugaji wa kisasa kwahiyo ni matarajio yao kuvuna kwa wingi asali hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Wilaya ya Mvomero, George Mkindo, amewapongeza akinamama hao kwa jitihada zao na akasema halmashauri yake itawaunga mkono kwa kila hali.

“Najua wana eneo dogo na nimewashauri watafute eneo lingine kubwa. Ili kuwasaidia tutaongea na vijiji ili kutenga mashamba kwa ajili ya ufugaji wa nyuki kwa sababu inatupunguzia hata sisi kazi kubwa ya kupambana na waharibifu wa mazingira, kwa kuwa wananchi wenyewe watakuwa walinzi,” anasema.

Amewasihi wanawake hao kutokukata tamaa japo kuna changamoto ya mtaji ambapo ni gharama kufanikisha lengo la mizinga 4000.

“Mjitahidi, msikate tamaa kwani gharama za ufugaji nyuki hua kubwa mwanzoni mwa ufugaji wa nyuki ambapo kikubwa ni kupata mizinga ambayo mmoja una gharimu shilingi 70,000 pia kupata eneo zuri kwa ajili ya shughuli hizo lenye maji karibu pia maua,” anasema Mkindo

“Yakiwa mavuno mazuri kwa mzinga mmoja unaweza kupata lita 10 hadi 15. Na kama yote imejaa wakivuna mara moja wanapata wastani wa lita 300 na lita moja ni shilingi 13,000. Kwa hiyo ni kipato kizuri,” anasema Mkurugenzi Mkindo

Anaendelea kusema kuwa kwa ufugaji huo, wakina mama hawa watasaidia kutunza mazingira kwani wakiwa na mashamba yanayozalisha mana yake hakutakatwa miti na kutakuwa na miti mingi ya aina mbalimbali ambayo itasaidia kutunza mazingira pia kupambana na kukabili hewa ya ukaa.

Akiongelea urahisi ya ufugaji wa nyuki, Mariam anasema nyuki hawahitaji matunzo sana kama ilivyo kwa mifugo mingine bali ni kutundukia mizinga mahali rasmi na baada ya hapo unaacha waendelee wenyewe na utakachokifanya wewe ni kwenda kuangalia maendeleo tu.

“Tumelenga kufanya ufugaji wa kisasa ambao ni wakutumia mabanda maalumu ili kuhakikisha kuwa nyuki wetu wanapata mahitaji muhimu katika eneo husika ikiwemo maji kwa wingi,” alisema Mariam

4.Baadhi ya mizinga ya akinamama wa Dakawa Green Voices ikionekana kuning’inia kwenye miti. Mizinga hii tayari ina nyuki.
4. Baadhi ya mizinga ya akinamama wa Dakawa Green Voices ikionekana kuning’inia kwenye miti. Mizinga hii tayari ina nyuki.

Akizungumzia umuhimu wa maswala haya Kwa upande mwingine, Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Oscar Kunambi, anasema kwamba kuanzishwa kwa mradi wa akinamama hao kutachochea jamii kuingia kwenye ufugaji wa nyuki wilayani humo badala ya kutegemea kilimo na mifugo pekee.

Anasema kwamba, soko la asali ni kubwa nchini Tanzania, ambapo tayari kuna kiwanda kikubwa wilayani Kibaha kinachohitaji malighafi lakini asali inayozalishwa haitoshelezi mahitaji.

Aidha, anasema kwamba, wilaya hiyo ina maeneo mengi yenye misitu ambayo ikitumiwa kwa ufugaji wa nyuki inaweza kuleta faida kubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

“Unapofuga nyuki, mbali ya kupata faida kutokana na mazao yake, lakini unasaidia kuyalinda maeneo hayo kwa sababu hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kwenda kukata miti sehemu ambayo kuna nyuki, kwanza usalama wake utakuwa mdogo,” anasema.

Kwa upande wake Katibu wa kikundi hicho, Amina Buteta, ana matumaini makubwa kwenye mradi huo na anasema kwamba unaweza kuwakomboa wanawake wa Dakawa na vijiji vya jirani kwa kujipatia kipato kikubwa.

“Tunakuja huku shamba kila baada ya wiki, wakati mwingine tunakuja kwa zamu kuangalia maendeleo, hivyo hatubanwi na ufugaji wa nyuki na tunaendelea na shughuli zetu nyingine,” anasema.

Amina anasema kwamba, wameanza na mizinga 30, lakini malengo yao ni kuwa na mizinga 4,000, lakini changamoto wanayokabiliana nayo ni mtaji wa kununulia mizinga hiyo pia kununua Mavazi maalumu kwa ajili kujizuia kung’atwa na nyuki(beekeeping gears) ambayo pia yanagharimu pesa nyingi kuyapata.

Anasema, kukosekana kwa mvua katika misimu tarajiwa kama ilivyokuwa zamani pamoja na mafuriko makubwa yanayosababisha maafa ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni vyema wananchi wakaangalia miradi mingine endelevu yenye kipato lakini inayoweza kutunza mazingira.

Kwa ujumla, wananchi wanapaswa kuitunza vizuri misitu ili kuweza kuendelea kupata mvua kwa wingi na kuondokana na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyopo kwa sasa.

Kwani kwa mujibu wa sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa (UNCCD), 2014, zaidi ya watu bilioni 1 ulimwenguni  leo hii hawana maji na mahitaji yataongezeka kwa asilimia 30 ifikapo 2030.

Sekretarieti hiyo inasisitiza kuwa ifikapo 2025 hadi watu bilioni 2.4 ulimwenguni wana uwezekano wa kuishi katika maeneo yenye vipindi vya ukame na ukosefu wa maji ambao utawasababishia watu zaidi ya milioni 700 kuhama makazi yao ifikapo 2030.

Inaongeza kuwa wengi bado wana ukosefu wa maji safi ya kunywa na kwa ujumla wanawake kutoka bara la Africa wanatumia zaidi ya saa bilioni 4 kwa mwaka wakichota maji.

Hivyo kwa hili juhudi za makusudo lazima zichukuliwe ili kuakikisha maji yanapatikana kwa wingi kwani maji ni uhai wa binadamu pia wanyama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles