26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ufugaji ng’ombe chanzo muhimu cha nishati

Na Mwandishi Wetu

SEKTA ya mifugo ni miongoni mwa sekta chache ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa na hata mtu mmoja mmoja. Hadi kufikia mwaka jana, sekta ya mifugo imekua kwa asilimia tano na kuchangia asilimia 7.4 ya pato la taifa.

Kwa kutambua mchango wa sekta hiyo, wizara iliamua kuwekeza katika mashamba ya mifugo ili kuyapa uwezo wa kuzalisha mifugo bora itakayosaidia kukuza kipato cha taifa na wananchi wake.

Moja ya shamba ambalo Serikali imewekeza, ni shamba la mifugo la Sao Hill mkoani Iringa, Wilaya ya Mufindi, Kata ya Ikongosi, Kijiji cha Itulavanu.

Historia Shamba la Sao Hill

Akitoa historia ya shamba hilo, Kaimu Meneja, Mtama Galusi, anasema lilianzishwa mwaka 1967, baada ya serikali kulitaifisha kutoka kwa wakulima wa Kizungu.

Meneja huyo aliendelea kusema kuwa mwaka 1968 shamba hilo lilianza kufanya kazi rasmi na kutumika kama shamba la kuzalisha mitamba bora ‘breeding unit’ na kuwauzia wafugaji wadogo wadogo wa nyanda za juu kusini.

Galusi anasema shamba la Sao Hill, limekuwa na uzalishaji mzuri kwa sababu linafaidika na hali ya hewa nzuri ya baridi  inayowafanya mifugo kustawi vyema na kutoa uzalishaji mzuri tofauti na mashamba mengine ambayo yapo katika ukanda wa joto.

Anasema shamba hilo pia linafaidika na maji ya Mto Ruaha ambao unatiririsha maji kwenye bwawa la Mtera hivyo, mifugo hiyo inapata maji ya kutosha tofauti na mashamba mengine.

Mafanikio 

Akizungumzia mafanikio ya shamba hilo ambalo lina ng’ombe takriban 1,600   anasema shamba hilo limefanikiwa kuzalisha mitamba mingi na kuisambaza kwa kuwauzia wafugaji wadogo wadogo kwa bei nafuu mikoa ya Iringa na Mbeya na wilaya zake, huku akisema katika Wilaya ya Rungwe na Halmashauri ya Wilaya ya Mji wa Busokelo mkoani Mbeya kuna ng’ombe wengi wa maziwa ambao zao lake ni shamba la Sao Hill.

Anasema wilaya hizo zilifaidika na utaratibu waliouanzisha wa Kopa ng’ombe Lipa ng’ombe utaratibu ambao uliwanufaisha wananchi wengi.

Anasema shamba hilo limezalisha malisho, ikiwa ni pamoja na mbegu za malisho na kuwauzia wafugaji wadogo wadogo wa mikoa ya Iringa na Mbeya kwa bei nafuu.

Alisema shamba linauza ng’ombe wake kwa bei nafuu kwa mfano bei ya mtamba wenye mimba bei yake ni Sh 1,600,000 tofauti na mashamba ya watu binafsi yaliyopo katika Wilaya ya Mufindi ambayo bei yake inafika hadi Sh 3,000,000 hadi 4,500,000. 

Anaipongeza Serikali kwa kuwajali na kuwapa wafugaji Mitamba bora kwa bei ambayo kila mtu anaweza kununua.

Galusi anasema katika kila mafanikio hapakosi changamoto, anaanisha changamoto kadhaa ambazo zinakabili shamba hilo, ikiwamo uchache wa vitendea kazi hususan usafiri wa kutembelea maeneo ambayo ina mifugo, alisema  kuna baadhi ya maeneo ambayo yapo umbali wa kilomita sio chini ya 10  hivyo, bila usafiri inakuwa shida kufika eneo husika.

Anasema  changamoto nyingine ni kuwa eneo hilo lina mvua nyingi zinazosababisha kupungua kwa madini joto ambayo ni muhimu kwa mifugo jambo ambalo linawalazimu kununua madini hayo kwa bei kubwa.

Matarajio 

Anasemawanatarajia hadi kufikia Juni, mwaka huu, wawe wamesambaza mitamba aina ya Borani kati ya 120 hadi 130 kwa sababu uhitaji wa ng’ombe hao bado ni mkubwa.

Anasema mitamba dume aina ya Borani, inasaidia kuboresha kosaafu za ng’ombe wa asili kwa wafugaji wadogo wadogo.

Wito 

Anawashauri wadau wa mifugo kuzalisha kwa tija ili wawe na maziwa na nyama za kutosha hatimaye kujenga uwezo wa kusambaza kwenye viwanda vinavyochakata mazao ya mifugo.

Pia, aliwashauri wafugaji kutumia mashamba ya serikali kupata madume bora ili waboreshe kosaafu za mifugo yao pia kuyatumia kama mashamba darasa ya kujifunzia.

Anawashauri wadau wa mifugo kutumia njia ya uhimilishaji kwani inasaidia kuboresha kosaafu za ng’ombe ambao wanakuwa haraka tofauti na ukuaji wa ng’ombe wa asili. 

Ofisa Mifugo ambaye pia ni mratibu wa sekta ya ng’ombe wa maziwa, Robert Semaganga, anaishukuru serikali kwa kuanzisha na kuwekeza katika shamba la Sao Hill kwani limekuwa msaada mkubwa kwa wafugaji, huku akitolea mfano shamba la Justine Bimbiga ambaye ana ng’ombe 54 ambao wengi ni zao la shamba hilo na kusema kuwa wanatumia shamba la mfugaji huyo kuonesha matokeo ya shamba la Sao Hill  na pia wana vyuo hujifunzia hapo kwa vitendo.

Jobisho Mkonyi, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa wilayani Mufindi, anasema uwapo wa shamba hilo, kumewasaidia kupata mitamba kwa bei nafuu ambapo mtamba aliyekuwa anauzwa Sh 1,600,000, uongozi wa shamba uliwapunguzia Sh 200,000 na Sh 400,000 walipunguziwa kama ofa kwa wafugaji.

Anasema uwapo wa shamba hilo unawafanya wapate huduma za wataalamu wa mifugo kirahisi kutoka shambani hapo.

Anaiomba Serikali kuendelea kuwasaidia ili waendelee kupata ng’ombe walio bora zaidi wanaotoa maziwa mengi. 

Ushauri wa Serikali 

Mkurugenzi wa Idara ya Malisho, Dk. Asimwe Rwiguza, anasema wafugaji wengi bado wanategemea malisho ya asili ambayo kimsingi hayatoshelezi na hayana viini lishe vya kutosha hivyo kuwahimiza wafugaji kuandaa mashamba ya malisho na kutumia mbegu bora zinazopatikana kwenye mashamba ya serikali ili kuboresha lishe za mifugo yao. 

Anasema wizara kupitia Idara ya Malisho na Uendelezaji wa Rasilimali za Mifugo, imeendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu uzalishaji na utunzaji wa malisho.

Faida ya ziada 

Ufugaji wa ng’ombe unaweza kuwa na faida zaidi kama wafugaji wataendelea kupewa elimu ya kutosha kutambua faida nyingine zaidi ya nyama, maziwa na ngozi.

Faida ya ziada anayoweza kuipata mfugaji kutoka kwa ng’ombe aliyefugwa vizuri ni upatikanaji wa nishati ya gesi ambayo kitaalamu inaitwa ‘Biogas’, nishati hii ya gesi inaweza kupatikana kutokana na kinyesi cha ng’ombe ambacho wengi wanakiita samadi.

Wafugaji wakielimishwa na kuhamasishwa vizuri kutumia njia hii mbadala ya matumizi ya nishati ya gesi inayotokana na samadi na faida zake huenda itasaidia  kupunguza matumizi ya kuni ambayo kwa muda mrefu sasa serikali imekuwa ikiyapiga vita kwani yanatajwa kuwa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira na uoto wa asili nchini.

Katikati ya Aprili, mwaka huu, maofisa habari wa wizara walifanya ziara katika Shamba la Mifugo la Sao Hill ambapo pamoja na mambo mengine, walifanya  mahojiano maalumu na Michael Mhosole, mfugaji na mkulima wa kijiji cha Igowole, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ambaye anafanya ufugaji wa ng’ombe wa kisasa kutoka katika shamba la Sao Hill.

Kwenye mahojiano hayo  Mhosole anasema pamoja na faida ya maziwa anayoipata kutokana na ufugaji wa ng’ombe hao pia anapata nishati ya gesi ambayo anaitumia kwa matumizi ya nyumbani kwake.

Anasema anapata nishati hiyo ya gesi baada ya kujenga mtambo unaotumika kuchakata samadi ya ng’ombe na kuibadilisha kuwa nishati ya gesi tayari kwa matumizi ya kupikia.

Anasema nishati ya gesi inayotokana na ng’ombe ikitumika vizuri inasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

 Serikali na wataalamu wakiwajengea wananchi uwezo na  elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya nishati ya gesi inayotokana na samadi  itakuwa ni chanzo kizuri cha ajira kwa vijana.

Anaongeza kuwa baada ya samadi hiyo kutumika kama chanzo cha nishati hutolewa na kupelekwa shambani na kwenda kutumika tena kama mbolea ya kukuzia mazao.

Kwa msingi huo, Mhosole   aliwahamasisha  wafugaji wenzake waone umuhimu wa kutumia nishati hiyo ili wapunguze gharama za matumizi na kutumia kwa usahihi mazao yanayotokana na mifugo ya ng’ombe.

Anatoa wito kwa wafugaji wenzake na kuwataka wajitahidi kutunza mifugo yao vizuri kwa kuwapatia huduma zinazohitajika ikiwemo kuandaa mashamba ya malisho yatakayowasaidia kuwa na chakula cha kutosha katika kipindi cha kiangazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles