29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Ufaulu wapanda kidato cha nne

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MATOKEO ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 2018 yametangazwa  ambako watahiniwa 322,965 ( asilimia 78.38 ya waliofanya mtihani huo) wamefaulu, wasichana wakiwa ni 163,920  (asilimia 77.58) na wavulana ni 159,045 (asilimia 79.23).

Mwaka 2017, watahiniwa waliofaulu walikuwa 287,713 (asilimia 77.09).

Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Neta), Dk Charles Msonde, alisema, “ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 1.29 ikilinganishwa na mwaka 2017.”

Katika mtihani huo, watahiniwa 426,988 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wasichana wakiwa ni 219,171 (asilimia 51.33) na wavulana 207,817 (asilimia 48.67).

Kati ya watahiniwa hao, wa shule walikuwa 368,037  na wakujitengea wakiwa 58,951.

Watahiniwa wa shule

Kwa   watahiniwa wa shule  matokeo hayo yanaonyesha   idadi ya   waliofaulu imeongezeka kwa asilimia 1.29 kutoka asilimia 77.09 ya mwaka 2017 hadi asilimia 78.38 mwaka 2018.

 “Watahiniwa wa shule waliofaulu ni 284,126 (asilimia 79.27 ya waliofanya mtihani) ambako wasichana waliofaulu ni 142,888 (asilimia 78.51) na wavulana ni 141,238  (asilimia 80.05).

“Mwaka 2017 watahiniwa 245,274 sawa na asilimia 77.57 ya watahiniwa wa shule walifanya mtihani huo hivyo ufaulu watahiniwa umeongezeka kwa asilimia 1.70 ikilinganishwa na mwaka 2017.

Alisema watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani ni 38,839 (asilimia 72.44) huku mwaka 2017 watahiniwa wa kujitegemea 42,439 (asilimia 74.41 waliofanya mtihani huo),hivyo ufaulu umeshuka kwa asilimia 1.97 ikilinganishwa na mwaka 2017.

Kuhusiana na mtihani wa Maarifa (QT) waliofaulu ni 7 (asilimia 62.46),  ambako mwaka 2017 watahiniwa wa mtihani wa maarifa 8,280 (asilimia 60.11) walifaulu mtihani huo, hivyo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.35 ikilinganishwa na mwaka 2017.

UBORA WA UFAULU

Kuhusu ubora wa ufaulu, alisema watahiniwa waliofaulu kwa daraja I-III  ni 113,825 ( asilimia 31.76) wakiwamo wasichana 47,779 (asilimia 26.25) na wavulana 66,046.

Alisema idadi hiyo imeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita ambako mwaka 2016 ilikuwa ni asilimia 27.60 na mwaka 2017 ilikuwa 30.15.

Watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 13,524 (asilimia 3.77 ya watahiniwa wote), wavulana wakiwa wakiwa 7,922 (asilimia 4.49) na wasichana wakiwa ni 5,602 (asilimia 3.08).

Waliopata daraja la pili ni 39,665 (asilimia 11.07) wavulana wakiwa 24,267 (asilimia 13.75) na wasichana wakiwa ni 15,398 (asilimia 8.46).

Waliopata daraja la tatu ni 60,636 (asilimia 16.92) wavulana wakiwa ni 33,857  (asilimia 19.19) na wasichana wakiwa ni 26,778 (asilimia 14.71).

Watahiniwa waliopata daraja la nne ni 170,301 (asilimia 47.51) wavulana wakiwa ni 75,192  (asilimia 42.62) na wasichana wakiwa 95,109 (asilimia 52.26).

Kwa upande wa watahiniwa waliopata sifuri ni 74,301 (asilimia 20.73),  wavulana wakiwa ni 35,193 (asilimia 19.95) na wasichana wakiwa ni 39,108 (asilimia 21.49).

UFAULU WA MASOMO KWA WATAHINIWA

Dk.Msonde alisema ufaulu wa shule katika masomo ya Historia, Kiswahili, Fizikia, Kemia, Basic Mathematic na Book-Keeping umepanda kati ya asilimia 0.83 na 8.76 ikilinganishwa na mwaka 2017.

Alisema ufaulu wa juu   ni ule wa somo la Kiswahili ambako asilimia 89.32 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hilo wamefaulu.

Alisema ufaulu wa chini  ni ule wa somo la Basic Mathematics ambako asilimia 20.02 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hilo wamefaulu.

SHULE ZILIZOFANYA VIZURI

Dk.Msonde alizitaja shule 10 zilizofanya vizuri katika mtihani huo huku   shule ya St Francis Girls ya Mbeya ikiongoza katika matokeo hayo ikifuatiwa na Kemebos ya mkoani  Kagera.

Alizitaja shule nyingine kuwa ni Marian Boys ya mkoani Pwani, Ahmes ya mkoani Pwani, Canossa ya Dar es salaam, Maua Seminary ya Kilimanjaro, Precious Blood ya Arusha, Marian Girls ya Pwani, Bright Future Girls ya Dar es Salaam na Bethel Sabs Girls ya Iringa.

Shule 10 za mwisho

Vilevile alizitaja shule 10 za mwisho kuwa ni Pwani Mchangani (1) ya Kaskazini Unguja, Ukuta (2) ya Kusini Pemba, Kwediboma (3) ya Tanga, Rwemondo (4) ya Mkoani Kagera,Namatula (5) ya mkoani Lindi.

Nyingine  ni Kijini (6) ya Kaskazini Unguja, Komkalakala(7) ya mkoani Tanga,Kwizu (8) ya  Kilimanjaro, Seute (9) ya   Tanga na Masjid Qubah Muslim (10) ya   Dar es salaam.

Watahiniwa 10 bora

 Dk.Msonde aliwataja watahiniwa 10  waliofanya vizuri katika mtihani kuwa ni Hope Mwaibaje wa Shule ya Ilboru ya Mkoani Arusha ambaye ameongoza.

Wengine na nafasina  katika mabano   ni Avith Kibani (2) kutoka shule ya Marian Boys ya  Pwani,         Maria Manyama(3) wa shule ya St Francis Girls ya Mbeya, Atughulile Mlimba(4) St Francis Girls ya Mbeya.

Pia wamo Flavia Nkongoki (5) kutoka St Francis Girls ya Mbeya, Leticia Ulaya(6) kutoka St Francis Girls ya Mbeya, Gibson Katuma (7) Marian Boys ya Pwani, Bryson Jandwa (8)ya Pwani, Idegalda Kiluba (9) kutoka  St Francis ya  Mbeya na Isack Julius (10) kutoka shule ya Marian Boys ya  Pwani.

Wasichana 10 bora

Aliwataja wasichana 10 waliofanya vizuri katika matokeo hayo kuwa  ni kutoka shule ya St Francis Girls  ambayo imetoa wanafunzi tisa kati ya 10.

Dk.Msonde alisema  Maria Manyama, ameongoza katika matokeo hayo akifuatiwa na Atughulile Mlimba kutoka shule hiyo hiyo.

Aliwataja wengine kuwa ni Flavia Nkongoki (3),Letcia Ulaya (4),Idegalda Kiluba (5), Subilaga Mwaisela (6), Joyce Sapali (7), Ivony Anangisye (8), Saraha Kasala (9) St Francis Girls na Theresia Karugwa(10) kutoka Anwarite Girls ya Mkoani Kilimanjaro.

Wanaume 10 bora

Kwa   wanaume, Hope Mwaibinje wa shule ya Ilboru ameongoza akifuatiwa na Avith Kibani wa shule ya Marian Boys ya  Pwani.

Wengine ni Gibron Katuma(3) kutoka shule ya Marian Boys, Brison Jandwa (4) kutoka Marian Boys, Isack Julius (5) kutoka Marian Boys, Justine Byarasobile 6) kutoka Katoke Seminary ya   Kagera.

Aliwataja wengine kuwa  ni Emanuel Kandege (7) kutoka Uwata mkoani Mbeya, Saitoti Upendo (8) kutoka Ilboru ya Arusha, Peter Kiama kutoka Feza Boys ya  Dar es Salaam na David Sichone kutoka Pandahill ya  Mbeya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles