PARIS, UFARANSA
TIMU ya taifa ya wanawake ya Brazil, imeyaaga mashindano ya Kombe la Dunia nchini Ufaransa baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo.
Brazil walitajwa kuwa miongoni mwa timu ngumu msimu huu na walipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri, lakini Ufaransa wameweza kutumia vizuri ardhi ya nyumbani na kufanikiwa kuwafungashia virago wababe hao.
Hadi dakika 90 zinamalizika, timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, lakini Ufaransa walifanikiwa kupata bao la kusonga mbele katika dakika 30 za nyongeza likiwekwa wavuni na Amandine Henry.
Hata hivyo Ufaransa walikuwa wa kwanza kupata bao, lakini bao hilo lilikataliwa na mfumo wa VAR, hivyo walipambana tena na kufanikiwa kupata bao la kuongoza katika dakika ya 52, likiwekwa wavuni na Valerie Gauvin kabla ya bao la pili kufungwa na Thaisa kumalizia bao la ushindi katika dakika ya 106.
“Hii ni ndoto yetu kufanya vizuri kwenye michuano hii mikubwa duniani ambayo inapigwa kwenye viwanja vyetu vya nyumbani, haikuwa kazi rahisi kufika hapa, lakini kutokana na maandalizi pamoja na umoja wetu umetufanya tuwe hapa.
“Tunaamini bado tuna nafasi ya kuendelea kufanya vizuri kwa ajili ya kuliwakilisha taifa kama ilivyokuwa kwa timu ya wanaume mwaka jana nchini Urusi, hivyo tutahakikisha tunapambana hadi hatua ya mwisho,” alisema Valerie.
Ufaransa wanaonekana kuwa bora katika soka la kimataifa, mwaka jana timu ya soka ya wanaume ilifanya makubwa nchini Urusi na kufanikiwa kuwa mabingwa wa dunia, hivyo wanaamini timu ya wanawake inaweza kufanya hivyo na kuandika historia mpya.
Kutokana na matokeo hayo ya juzi, timu hiyo sasa inatarajia kukutana na timu ya taifa ya Marakani au Hispania katika hatua hiyo ya robo fainaili.