Na FARAJA MASINDE,
UNAPOTAJA kampuni kubwa duniani zilizopiga hatua kwenye eneo la teknolojia, huwezi kuiacha Kampuni ya Microsoft ambayo ni maarufu zaidi dunaini.
Microsoft inayomilikiwa na bilionea Bill Gates, imekuwa na mikakati mbalimbali katika kujiimarisha zaidi pamoja na kukuza zaidi teknolojia. Sababu hizo ndizo zimefanya kampuni hiyo kuanzisha mpango wa maendeleo wenye kuchochea matumizi ya teknolojia Afrika (Microsoft 4Africa Initiative).
Licha ya kwamba umekuwapo kwa siku nyingi, lakini wengi wamekuwa hawaujui malengo yake kwa Afrika. Kwanza kabisa mpango huu wa Microsoft 4Afrika Initiative ulianzishwa Februali 2013 ukiwa na lengo la kusaidia ukuaji uchumi wa Bara la Afrika kupitia uwezo wa kiushindani wa teknolojia huku ukizingatia gharama nafuu pamoja na ubunifu wa kiwango cha kimataifa ambapo hayo yamekuwa ni miongoni mwa mambo muhimu.
Eneo la teknolojia
Kampuni ya Microsoft inasaidia jitihada za uwepo wa teknolojia kwa gharama nafuu, ambapo hapa inajumuisha vifaa na teknolojia mbalimbali ikiwamo ile ya cloud.
Microsoft inaamini kuwa na teknolojia imara na ya kisasa ni jambo bora zaidi linaloweza kuchochea ukuaji wa haraka wa maendeleo barani Afrika.
Hii inamaana kwamba iwapo teknolojia itaimarika, basi huduma za kijamii, biashara, usafiri na sehemu za uzalishaji kama viwandani kutakuwa na uboreshaji mkubwa katika utayarishaji na kutoa huduma.
Hivyo, kupitia mkakati huu Microsoft wamekuwa na mpango kabambe wa kusambaza vifaa muhimu vya kiteknolojia zikiwamo kompyuta za Window, programu za kisasa zaidi, simu, Laptop pamoja na vifaa vingine kwa vijana wa Afrika, lengo likiwa ni moja tu – kuhakikisha wanatumia teknolojia ipasavyo ili waweze kukuza uchumi wao na Afrika kwa ujumla.
Microsoft wanaamini kuwa Afrika inawatu wengi ambao wanamawazo mapana na ndoto kubwa za kiuchumi ikiwamo wale wenye kutengeneza program (Apps) zenye kutatua changamoto mbalimbali lakini wamekuwa wakishindwa kuzitekeleza kutokana ufinyu wa vifaa vya teknolojia.
Katika kuhakikisha kuwa vijana wa Afrika wanakuza ujuzi wao kwenye masuala mbalimbali ikiwamo teknolojia, tayari Microsoft wameanzisha kituo cha mafunzo cha Afrika Academy, mkakati ambao unaelezwa kuwa utawapa manufaa wasomi mbalimbali wakiwamo pia viongozi wa serikali Afrika.
Ni wazi kuwa Afrika imesalia kuwa nyuma kwenye eneo zima la maendeleo ya teknolojia kutokana na kukabiliwa na changamoto ya ujuzi, hivyo ni kweli kuwa kupitia mipango kama hii ya Microsoft inaweza kuwa njia bora kwa Afrika kupiga hatua kwenye eneo hili la teknolojia na uchumi kwa ujumla.
0653045474