23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Uenyekiti wa JPM ulivyomulika ulinzi, utengamano wa kiuchumi SADC

 NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

NAWASHUKURU waheshimiwa wakuu wa nchi kwa kuniamini na kunikabidhi jukumu la kuwa mwenyekiti wenu. Nimelipokea jukumu hilo kwa uenyenyekevu mkubwa, naahidi kuendeleza mambo yote mazuri kuhakikisha amani, utulivu na usalama unatawala kwenye jumuiya yetu. 

“Nawaomba waheshimiwa viongozi tushirikiane ili kuleta maendeleo kwenye nchi zetu na jumuiya yetu kwa ujumla. Umoja wetu ndiyo nguvu yetu. Na katika hilo, nawaahidi kuwa Tanzania ikiwa mwenyekiti wa jumuiya itashirikiana na nchi zote wanachama ili kufanikisha utekelezaji wa malengo na kuiletea maendeleo jumuiya yetu,” hii ni kauli ya Rais Dk. John Magufuli, wakati akifunga mkutano wa 39 wa SADC Agosti 18, 2019. 

Rais Dk. Magufuli alikabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja akipokea kijiti kutoka kwa Rais wa Namibia, Dk. Hage Geingob. 

Uenyekiti wa Tanzania katika jumuiya hiyo ulifikia ukomo wiki iliyopita ambapo Rais Dk. Magufuli alikabidhi kijiti kwa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Filipe Nyusi.

Mwaka mmoja wa uenyekiti huo, Tanzania inajivunia mafanikio kwa kutoa mchango ambao umesaidia kuisogeza mbele jumuiya hiyo.

Akizungumza wakati wa mkutano wa 40 wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao akiwa Ikulu ya Chamwino Dodoma, Rais Dk. Magufuli anasema uongozi wake umekuwa na mafanikio makubwa. 

“Unapopewa jukumu la kuongoza taasisi unapokamilisha uwe umetoa mchango utakaosaidia kusogeza mbele kuliko ulivyoikuta. Tumeweza kutoa mchango ambao umesaidia kuisogeza mbele jumuiya yetu,” anasema Rais Dk. Magufuli.

Wakati Tanzania ikikabidhiwa uenyekiti huo, wakuu wa nchi walipitisha maazimio kadhaa sambamba na kusaini itifaki mbalimbali zilizotekelezwa chini ya uenyekiti wa Tanzania.

Rais Dk. Magufuli anasema kumekuwapo mafanikio katika masuala mbalimbali kama vile siasa, ulinzi na usalama, utawala bora na demokrasia, utengamano wa kiuchumi, masuala ya kijamii na mengine.

ULINZI NA USALAMA

Rais Dk. Magufuli anasema moja ya maeneo muhimu na ya kipaumbele katika jumuiya hiyo ni ulinzi na usalama na kwamba wamejitahidi kusimamia jukumu hilo kikamilifu kwa kuhakikisha amani na usalama unaendela kutawala.

Anasema wameshughulikia baadhi ya migogoro iliyopo ikiwemo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Lesotho.

“Namshukuru Rais Emmerson Mnangagwa (wa Zimbabwe) kwa jitihada za kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro nchini DRC, naipongeza Lesotho kwa kufikia makubaliano ya amani chini ya msuluhishi Rais wa Afrika Kusini.

“Hatua hii itaimarisha amani na utulivu Lesotho na kuwawezesha raia wa nchi hiyo kujikita katika shughuli za maendeleo,” anasema.

UTENGAMANO WA KIUCHUMI

Wakati wa mkutano wa 39 nchi wanachama zilikubaliana kuutumia vizuri mwaka huo ili kuhakikisha mkakati wa viwanda wa Sadc unatekelezwa kwa vitendo. 

Rais Dk. Magufuli anasema kumekuwa na urahisi wa kufanya biashara mipakani hasa kwa wafanyabiashara wadogo baada ya kuzinduliwa kwa mfumo wa utoaji vyeti vya utambuzi kwa njia ya mtandao.

“Wakati wa mkutano wa 39 tulizindua Baraza la Biashara la SADC ambalo litachochea shughuli za uzalishaji na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi ambazo ni muhimu katika ujenzi wa uchumi,” anasema.

MAENDELEO YA VIWANDA

Mkutano wa 39 ulifanyika chini ya kaulimbiu isemayo ‘Mazingira Wezeshi ya Biashara kwa ajili ya Kuwezesha Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda, Kukuza Biashara na Kuongeza Fursa za Ajira’ ambayo imeweka msisitizo katika kuboresha mazingira ya biashara, ikiwemo kuondoa vikwazo vya mipakani, ukiritimba kwenye maamuzi, rushwa, ili kukuza sekta ya viwanda na kustawisha biashara kwenye ukanda huo.

Rais Dk. Magufuli anasema chini ya uenyekiti wake upatikanaji wa umeme wa uhakika umeongezeka kwa megawati 3,595 na kwamba baadhi ya nchi zimesaini makubaliano ya kusafirisha umeme kwa pamoja zikiwamo Tanzania na Zambia, Malawi na Msumbiji.

Anasema pia wameandaa ajenda za maendelo ya SADC baada ya 2020 kwani tangu mwaka 2000 zimekuwa zikisimamiwa na mpango mkakati elekezi wa maendeleo ya kikanda wa 2015 na mpango mkakati wa asasi ya siasa, ulinzi na usalama awamu ya pili.

Kwa mujibu wa Rais Dk. Magufuli, mikakati yote hiyo inafikia ukomo mwishoni mwa mwaka huu hivyo wameweza kuandaa Dira ya Maendeleo ya SADC ya 2050 na Mpango Elekezi wa Maendelo ya Kikanda wa 2020 hadi 2030.

Anasema ana imani mikakati hiyo itatoa mwelekeo mpya wa kufikia malengo ya SADC wanayoitaka.

“Tulijitahidi kuzihimiza nchi zote wanachama kuweka kipaumbele kutengeneza mazingira mazuri ya kustawisha ukuaji wa sekta ya viwanda katika nchi zetu,” anasema Rais Dk. Magufuli.

KISWAHILI

Mojawapo ya ajenda zilizowasilishwa na Tanzania kwenye mkutano huo ni suala la lugha ya Kiswahili ili itambuliwe rasmi katika jumuiya hiyo ambayo awali ilikuwa na lugha tatu tu; Kingereza, Kifaransa na Kireno.

Tanzania iliwasilisha ajenda hiyo ikizingatiwa kuwa lugha ni chombo muhimu katika kuimarisha uhusiano baina ya watu, kukuza na kuimarisha ushirikiano na utengamano kati na baina ya mataifa.

Awali Rais Dk. Magufuli alianza kampeni ya kukipigania Kiswahili kuwa lugha rasmi kwa kukizungumza katika mikutano mbalimbali ya kimataifa na hata alipotembelea baadhi ya nchi wanachama kama vile Namibia aligawa vitabu vya Kiswahili.

Rais Dk. Magufuli anasema wakati wa harakati za ukombozi, Mwalimu Nyerere alijitoa yeye na nchi yake na alikuwa tayari watu wake wapate shida ili nchi nyingine zikombolewe na katika shughuli zote hizo walikuwa wanatumia Kiswahili.

“Baada ya kusoma sehemu ya hotuba yangu ya ukaribisho kwa Lugha ya Kiswahili, Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC walifurahi na kuvutiwa. Tulipokutana kwenye mkutano wetu wa ndani wote kwa pamoja na kwa kauli moja walifanya uamuzi wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ya SADC.

“Haya yote ni kutokana na uongozi bora na kujitoa kwa baba mmoja aliyependa majirani zake, Julius Kambarage Nyerere.

“Suala la kutoa huwa ni gumu, wapo wanaojitolea figo kusaidia wagonjwa na wapo wanaosaidia kuokoa wengine, na baba wa Taifa aliamua kutoa upendo wake kusaidia wengine. Tunafurahi tumefuta machozi 

 ya Mwalimu Nyerere,” anasema Rais Dk. Magufuli.

Mwaka mmoja baada ya lugha hiyo kuridhiwa Rais Dk. Magufuli anasema kumekuwa na mafanikio kutokana na kuendelea kuenea kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo. 

“Kiswahili kitachochea ushirikiano na utengamano ndani ya jumuiya ndiyo sababu hata leo (siku aliyokabidhi uenyekiti kwa Msumbiji) nimeona nitoe hotuba yangu kwa Kiswahili,” anasema Rais Dk. Magufuli.

Kiswahili ni lugha ya 10 duniani ya 13 Afrika na ya sita katika nchi za SADC kuzungumzwa na watu wengi.

MGOGORO WA ZIMBABWE

Nchi wanachama zilikubaliana kuendelea kujadiliana na kufanya mawasiliano na jumuiya ya kimataifa ili kuwezesha kuondolewa kwa vikwazo Zimbabwe.

Rais Dk. Magufuli anasema wameendelea kufanya mawasiliano na jumuiya za kimataifa kuwezesha Zimbabwe kuondolewa vikwazo sambamba na kutekeleza azimio la Oktoba 25 kila mwaka kama siku maalumu ya kupinga vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo.

“Tuliendelea kuandaa makongamano, midahalo ya kutoa matamko yenye kupinga vikwazo vya Zimbabwe, Oktoba 25, 2019 tulitekeleza azimio hili, pia tulijumuisha suala hilo kwenye hotuba zetu na majukwaa mbalimbali ya kimataifa na baadhi ya mafanikio yameanza kupatikana.

“Umoja wa Ulaya umeanza kuona umuhimu wa kutatua migogoro kwa kutoa misaada ya kibinadamu,” anasema Rais Dk. Magufuli.

Anasema vikwazo vimekuwa na athari kubwa kwa wananchi wa Zimbabwe hususan wanawake, wazee na watoto na kwamba vikiondolewa nchi hiyo itatoa mchango mkubwa si tu kwenye jumuiya hiyo bali duniani kwa ujumla.

“Nazishukuru nchi zote wanachama kwa ushirikiano mkubwa iliotupatia, kufikia malengo endelevu katika ukanda huu, nina uhakika sasa tunaanza kuona maendeleo kwa kasi zaidi. Tunaahidi kumpa mwenyekiti mpya ushirikiano wa kutosha,” anasema Rais Magufuli.

CHANGAMOTO

Licha ya mafanikio yaliyopatikana Rais Magufuli anasema kipindi cha uongozi wake kulikuwa na changamoto mbalimbali kama za migogoro, ugaidi, corona na nyingine.

“Changamoto zinatukumbusha umuhimu wa kuendelea kushirikiana, nina matumanini chini ya uongozi wake (Rais Nyusi) atatoa mchango mkubwa wa kuzishughulikia baadhi ya changamoto nilizozitaja,” anasema Rais Magufuli.

Aidha anaziomba nchi zinazoendelea kuendelea kutoa misamaha ya kodi kuziwezesha nchi maskini kukabiliana na janga la corona.

“Nchi zinazoendelea ziangalie uwezekano wa kusamehe madeni au kutoka mikopo na misaada isiyo ya riba ili ziweze kukabilaina na athari za kiafya na kiuchumi za ugonjwa wa corona.

“Tuendelee kushirikiana na kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kukabiliana na ugonjwa huu, nchi wanachama tushirikiane kuharakisha uanzishwaji wa mfuko wa maafa,” anasema.

Anasema pia walitoa miongozo ya kufanya biashara kwenye maeneo ya mipakani ambayo imewezesha wananchi kuendelea kufanya biashara licha ya kuwepo kwa corona na kupunguza athari za kiuchumi kwa wananchi na nchi kwa ujumla.

RAIS NYUSI

Kwa upande wake Rais Nyusi anampongeza Rais Magufuli kwa kuongoza vema jumuiya hiyo na kuahidi kushirikiana na nchi wanachama kuhakikisha malengo ya jumuiya hiyo yanafikiwa.

“Kwa unyenyekevu mkubwa watu wa Msumbiji tutahakikisha tunaendana na malengo ya umoja huu, tunaamini mafanikio tutakayoyapata yatatokana na ushirikiano wa nchi wanachama.

“Tunashukuru kwa waanzilishi wa jumuiya hii na michango yao waliyotoa katika ukombozi wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. Tuna uhakika kwamba tutaongoza jumuiya katika muktadha na mafanikio ya pamoja ambayo siku zote tumekuwa tukiyatazamia,” anasema Rais Nyusi.

Ni wazi kuwa uenyekiti wa Tanzania umekuwa mwanzo mpya wa mafanikio na utatuzi wa changamoto zinazoikabili Sadc ambayo imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanafikiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles