Na Mwandishi Wetu
Wakati shughuli mbalimbali zikiendelea katika eneo la hifadhi ya ngorongoro wananchi wameendelea kuitikia wito wa kuhama kwa hiyari huku zikishuhudiwa jumla ya kaya 79 zenye watu 367 na mifugo 995, kutoka hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera Handeni na maeneo mengine waliyochagua wenyewe.
Kuhama kwa wakazi hao ni matokeo ya uelimishwaji wa wananchi kuhusu shughuli za kimaisha zinazopelekea kuharibu mazingira halisia sambamba na uhatarishaji wa maisha ya wanadamu kwa kuingiliana kiukaribu na wanyamapori wakali katika eneo hilo la hifadhi ya ngorongoro.
Akiwaaga wananchi hao Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii (anayesimamia maliasili) CP Benedict Wakulyamba mapema tarehe 22 Agosti 2024 amesema kuwa kuondoka kwa kundi hilo leo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kulinusuru eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambapo wananchi wameendelea kuelimishwa na kuhama kwa hiari kwa ajili ya kuboresha maisha yao na kunufaika na fursa za kiuchumi zilizoko nje ya hifadhi.
Ametoa tahadhari kuwa wapo baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakihamia Msomera kinyemela bila kufuata utaratibu uliowekwa na kuleta changamoto kwa ndugu zao wanaowakuta huko na kuwasihi kuwa kufuata utaratibu na miongozo iliyowekwa ili wawe wakazi halali wa maeneo wanayopenda kuhamia.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kuhamisha wananchi wa Ngorongoro kwa hiari, Afisa Uhifadhi mkuu na Meneja mradi wa kuhamisha wananchi kwa hiari PCO Flora Assey amebainisha kuwa tangu zoezi hilo lilipoanza mwezi Juni, 2022 hadi kufikia mwezi Agosti, 2024 takriban kaya 1,598 zenye watu 9,618 na mifugo 39,779 imeshahama ndani ya hifadhi kwenda Kijiji cha Msomera na maeneo mengine.
Akiongea kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Kamishna msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Mhandisi Daniel Chegere ameeleza kuwa NCAA inaendelea na zoezi la kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhama kwa hiari katika eneo la hifadhi na kwenda maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa kujengewa miundombinu ya kisasa yenye huduma zote muhimu za kijamii ambazo ni salama zaidi tofauti na ilivyo ndani ya ya hifadhi.
Mhandisi Chegere ameongeza kuwa hali ya usalama katika hifadhi hiyo inaendelea vizuri, ambapo ulinzi umeimarishwa na wageni mbalimbali wanaotembelea hifadhi hiyo wanaendelea na shughuli za utalii bila changamoto.