28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Udom wanadi shahada ya sanaa na ubunifu Sabasaba

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimewahamasisha vijana kusoma fani ya sanaa na ubunifu ambayo inafundishwa katika ngazi ya shahada chuoni hapo.

Chuo hicho kinatumia Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) kunadi shughuli inazozifanya, masomo yanayofundishwa na kuonyesha kazi mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi hasa katika Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari.

Mkuu wa Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk. Deograsia Ndunguru, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Dar es Salaam.

Akizungumza Julai 7,2024 katika banda la chuo hicho lililopo katika maonesho hayo Mkuu wa Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari, Dk. Deograsia Ndunguru, amesema wanafunzi wanafundishwa mbinu mbalimbali za uchoraji na ufanyaji sanaa.

“Tumekuja na picha walizobuni wanafunzi na mapambo ambayo ni bunifu za wanafunzi, tunawafundisha uchanganyaji wa rangi, matumizi ya rangi zenyewe, kutumia fursa zinazowazunguka ili kujipatia kipato. Mfano kuna chupa za vinywaji mbalimbali ambazo tukishakunywa tunatupa, hizo takataka ni fursa kwa wanafunzi wetu, wanaokota na kutengeneza bidhaa mpya inayoweza kuwapatia kipato,” amesema Dk. Ndunguru.

Picha ya Rais Samia Suluhu Hassan inayomwelezea akiwa katika majukumu matatu ya kitaifa ambayo imechorwa na mwanafunzi wa fani ya Sanaa na Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Ametoa mfano wa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, Enock Tarimo, aliyechora picha ya Rais Samia Suluhu Hassan inayomwelezea akiwa katika majukumu matatu ya kitaifa ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa watembeleaji wa maonesho hayo.

“Picha inamzunguzia Dk. Samia Suluhu Hassan katika majukumu yake makuu matatu ya kitaifa; jukumu la kwanza la kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaiona picha ambayo ina ushungi mwekundu na vazi jeusi, analo jukumu la pili ambalo ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi tunamuona katika vazi la chama, ana ushungi mweusi na vazi la kijani. Jukumu la tatu tunamuona Dk. Samia Suluhu Hassan Amiri Jeshi Mkuu yuko katika vazi la kijeshi.

“Watu wengi walikuwa hawajui kama ngazi ya chuo kikuu mwanafunzi anaweza kujifunza kuchora, tunawatengeneza wanafunzi wakimaliza masomo waweze kujiajiri. Ajira zipo lakini hazitoshi, wanaomaliza ni wengi na si wote wanaweza kuajiriwa na serikali kwahiyo tunamuandaa mwanafunzi anapotoka anakuwa tayari ana kitu cha kufanya,” amesema.

Mmoja wa wahitimu katika fani hiyo, Sultan Samwel, amesema kumekuwa na dhana potofu na hata baadhi ya wazazi kudhani kwamba sanaa ni uhuni hali inayosababisha kuwapo kwa mwamko mdogo.

“Baada ya kumaliza kidato cha sita nilishinikizwa kusoma sheria lakini kwa kuwa nilikuwa napenda fani hii nilichagua vyuo viwili na vyote nilipata lakini niliamua kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Dodoma, nimehitimu mwaka jana (2023) na sasa najiendeleza na ujuzi nilioupata. Nina kampuni ambayo niliianzisha nikiwa chuoni, nimeshaisajili na ninaiendeleza…nafurahi sana kuwa zao la Chuo Kikuu cha Dodoma,” amesema Samwel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles