23.9 C
Dar es Salaam
Saturday, September 21, 2024

Contact us: [email protected]

UDOM wahamasisha matumizi teknolojia za kisasa kuongeza tija kwenye kilimo

Na Nora Damian, Mtanzania Digital Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewahamasisha wakulima kutumia mbinu na teknolojia mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi walizozibuni kwa lengo la kuongeza tija na kukuza sekta ya kilimo.

Akizungumza kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko UDOM, Rose Mdami, amesema wanataaluma wa chuo hicho kwa kushirikiana na wanafunzi wamekuwa wakifanya tafiti na kubuni teknolojia mbalimbali ambazo ndio njia pekee ya kuwainua wakulima.

Miongoni mwa teknolojia zinazooneshwa na chuo hicho katika maonesho hayo ni kifaaa cha kulishia samaki kinachotoa tarifa kwa mfugaji kuhusu muda na kiasi cha chakula.

Amesema wanahakikisha chuo kinakuwa na mchango katika kuhakikisha mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia yanayotokea duniani yanatumika kuendeleza na kukuza sekta ya kilimo.

“Lengo letu ni kuendelea kuboresha huduma zetu na kuwafikia wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na chuo chao kwa maendeleo makubwa ya taifa letu.

“Kwenye maonesho ya Nanenane chuo kimekuja na bidhaa zinazohusiana na kilimo na lengo letu ni kushiriki kwa kutumia wanataaluma wake kwenye suala zima la kuendeleza na kukuza kilimo, chuo kinafundisha sayansi na kinazalisha wanataaluma na wanasayansi na teknolojia zinazotumika katika uzalishaji mkubwa wa kilimo,” amesema Mdami.

Amesema bidhaa nyingi za kilimo wanazoonesha kwenye maonesho hayo zimetokana na tafiti ambazo chuo kinaendelea kufanya na kutolea mfano Mkoa wa Dodoma ambao hauna mvua nyingi kwa kubuni mazao ambayo yanastahimili ukame.

“Tunaamini tukiendelea kufanya hivyo tutazalisha wataalam ambao watakwenda kusaidia jamii ikajifunza kutoka chuo kikuu cha Dodoma tukaendelea kuongeza uzalishaji na wananchi kupenda na kujihusisha na kilimo,” amesema.

Amewasihi Watanzania wanaokwenda kwenye maonesho hayo kupita katika banda la Udom ili kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo.

Katika maonesho hayo chuo hicho pia kinafanya udahili kwa wahitimu wa kidato cha sita na wale waliomaliza diploma na kuwataka wanaotaka kujiunga kuanzia ngazi ya stashahada, shahada za awali na shashada ya uzamivu kutembelea katika banda la UDOM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles