28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

UDOM kuongeza nguvu katika tafiti zinazotatua changamoto kwenye jamii

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimesema kimejielekeza kufanya tafiti zinazotoa majibu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kuhakikisha kunakuwa na ustawi kwa Watanzania.

Akizungumza Julai 3,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wineaster Anderson, amesema tafiti hizo zinafanywa na wanafunzi pamoja na wanataaluma.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wineaster Anderson (katikati), akiangalia bidhaa zinazoonyeshwa katika banda la chuo hicho kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Dar es Salaam.

“Mwaka huu tumekuja na bidhaa mpya kuwaonesha Watanzania kwa sababu mwaka jana tulikuwa na bidhaa tofauti, nyingine tumeziongeza mwaka huu kuanzia aina za mashine ambazo zinasaidia katika sekta ya samaki. Lakini wanafunzi wetu wameingia katika uwanja wa kutengeneza ‘rockets’ na kwenye maeneo ya vyakula ili kutibu maradhi mbalimbali kwa kutumia lishe asili.

“Udom inajipambanua kwa kuangalia matatizo ya jamii ya Watanzania na kutumia akili za wanafunzi na wafanyakazi wake kuangalia namna ya kuzitatua hasa katika eneo la afya, teknolojia na ukija Sabasaba utaziona,” amesema Profesa Wineaster.

Amesema bidhaa hizo ambazo zimetengenezwa na wanafunzi mbalimbali wa chuo hicho zinatokana na tafiti walizofanya pamoja na wanataaluma na kusisitiza ndizo zinazowezesha kuwepo kwa teknolojia mpya.

“Bila tafiti huwezi kuja na tekolojia mpya, huwezi kuja na ubunifu wowote kwahiyo tumejipambanua katika eneo hilo, licha ya kuwepo kwa changamoto ya rasilimali fedha kweye tafiti lakini tunaendelea kujitahidi katika eneo hilo…kikubwa tafiti zetu zimejikita katika jamii ya Watanzania na kutatua matatizo yaliyoko katika jamii yetu Tanzania,” amesema.

Profesa Wineaster amesema hivi sasa wanajielekeza kutoa mafunzo ya amali ambayo mwanafunzi yeyote katika chuo hicho anafunzwa kwa vitendo na darasani ili akimaliza masomo akatengeneze ajira badala ya kutafuta ajira.

Aidha amesema wanatarajia kufungua kampasi mpya mkoani Njombe itakayoanza kutoa mafunzo Septemba 2026 ambayo itajikita katika sekta zilizoko mkoani humo kama misitu, madini, uvuvi na nyingine.

Kwa mujibu wa Profesa Wineaster, ujenzi wa kampasi hiyo utatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na kwamba hivi sasa wako katika hatua za manunuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles