Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM
UFANYWAJI wa Tafiti na majaribio ya dawa ni sehemu muhimu zaidi hasa katika maendeleo ya nchi za uchumi wa kati na chini kama Tanzania.
Hii huendana na ubora wa maabara ambazo zinatumika kufanya tafiti na vipimo ili kuleta manufaa kwa wananchi ambao mwisho wa siku ndio wanatumia matokeo hayo.
Hapa nchini Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA) ndio yenye jukumu la kuhakikisha uimara na ubora wa bidhaa hizo ambapo hayo yote hutoka katika upimaji unaofaa wa maabara.
Serikali inazingatia ukaguzi na uimarishaji wa maabara mbalimbali ili kuweza kukidhi vigezo vinavyotakiwa.
Katika kulibainisha hilo MTANZANIA Jumapili limezungumza na Mkurugenzi wa Pharm R&D Lab kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi shirikishi Muhimbili(MUHAS) Prof Eliangiringa Kaale ambaye anaeleza ni jinsi ambavyo wanafanikiwa katika kupima uwezo wa maabara zilizopo kanda ya Afika Mashariki na Nchi zingine za Afrika.
Prof Kaale anasema lengo la kuanzishwa kwa maabara hiyo ni kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wafanyakazi wa viwanda vya dawa na wanafunzi wanasoma famasia.
“Kimsingi kuna mambo mawili katika maabara kuna kufanya formulation na kufanya majaribio ya dawa,tumeanzisha huduma ya kutoa upimaji wa umahiri kwa wachunguzi wa sampuli.
“Tunafanya hivi kama maabara kwenye kiwanda kuna uzalishaji wa dawa na dawa hazijaachiliwa sokoni na zinapimwa ili kuhakikisha kama zinakidhi vigezo ambapo kuna maabara ambayo inafanya kazi hizo.
“Na pia maabara hizo ziko kwenye mamlaka ambazo zinadhibiti ubora kama TMDA, kwa hiyo sasa ili zile maabara zinazofanya uchunguzi matokeo yake yaaminike lazima zioneshe kwamba wana umahiri wa kuchunguza kwahiyo hiyo ‘program ya professional testing’ ni mpango mahususi onaopima ubora wa maabara katika kuchunguza sampuli,”anaeleza.
Anasema upimaji umahiri huongeza kuaminika kwa maabara katika viwango tofauti tofauti vya upimaji wa sampuli.
“Tunachokifanya tunatengeneza sampuli ambazo tunajua ina kiasi gani, mfano paracetamol kuna vitu tunaongeza ambazo wao hawavijui kwahiyo tunawasambazia na tunawaandikia na ‘protocol’ jinsi ya kupima ile sampuli.
“Halafu wakimaliza wanatutumia matokeo kuwa kuna kiasi gani kwa kila formular iliyopo kwahiyo tunapokea matokeo ya maabara zote ambazo zimeshiriki na kufanya upambanuzi.
“Na kuna jinsi ya kuwapima kigezo ikifika kati ya 0 na mbili tunasema maabara hiyo ina uwezo yaani matokeo yake yanakubalika kama ikifika kati ya mbili na tatu matokeo yake yana uwalakini yakiangukia tatu na kuendelea matokeo yake hayaaminiki tena,”anabainsha Prof Kaale.
Anaongeza;“Tunafanya kuwajaribu kwasababu tuna maabara kwaajili ya kutengeneza dawa na kwaajili ya kupima uwezo wa dawa mfano kama paracetamol utakuta kidonge kina mill 500 na kama ukitengeneza kidogo hicho maabara inaweza ikadanganya na wanaweza wasichunguze wakajaza tu matokeo kwasababu wameona hiyo mill 500.
Kwa mujibu wa Prof Kaale wanachokifanya kutengeneza vidonge vya dawa vinavyofanana katika umbo na zile ambazo zinatumika katika soko lakini wanapunguza au kuongezea vitu vilivyotumika katika kutengeneza dawa hiyo.
“Kwahiyo sasa wao wanatakiwa kupima na waripoti kilichopo kwasababu mara nyingi maabara zingine wanaweza wasipime wakaandika tu matokeo kwahiyo ndio lengo letu huwa tunawatega.
MAABARA ZINAZOFAULU ZAONGEZEKA
Kutokana na kufanya upimaji wa umahiri katika maabara Prof Kaale anasema hali hivyo imesababisha kuendelea kuongezeka kwa ubora wa maabara kila mwaka.
“Wakati tulivyokuwa tunaanza tuliliona hilo kwasababu walikuwa hawajui tumebadilisha kiwango lakini sasa wameendelea kuwa bora, mwaka 2013 ukiangalia mwenendo sasa tuko mzunguko wa tisa yaani maabara ambazo zinafaulu sasa zinaongezeka kila mwaka kila tukitoa mzunguko walioripoti walikuwa asilimia 57 sasa tuko kwenye asilimia 90.
“ Na kila tukifanya tukaona changamoto tunawapa mafunzo kwa kupitia matokeo pamoja na kusema changamoto zao tunazijadili jinsi ya kuzidhibiti kama njia ya kuimarisha ubora.
Anasema maabara wanazoangalia ni zile za kikanda za nchi za Afika Mashariki na nje ya Afrika Mashariki na mapungufu yote yaliyoripotiwa.
“ Lakini baada ya kuanzisha ukaguzi tangu 2013 hadi 2020 kumekuwa na mafanikio makubwa na tunategemea kuwa hili ni zoezi endelevu kwamaana kwamba ukishafikia kutoka matokeo hautapimwa tena.
“Mfano kama hizo maabara ambazo zinafanya uchunguzi kuna kiwango cha ISOL ambacho wanapimwa nacho ili uweze kutimiza masharti ya viwango lazima ushiriki katika upimaji wa umahiri ni kigezo kimoja wapo na sisi pia tunaendelea kufanyiwa ufuatiliaji.
Anasema licha ya kupima umahiri wa maabara mbalimbali lakini pia wao wanafanyiwa tahimini na shirika la kitaifa la Viwango .
“Na sisi kama watoa huduma tunatathiminiwa na bodi nyingine ili ioneshe kuwa na sisi huduma tunazotoa zinakidhi vigezo tuliomba tufanyiwe tathimini mara ya kwanza walikuja wakatufanyia pre assessment wakabaini mapungufu ya kawaida.
“Wakatueleza sehemu ambazo tunatakiwa kufanyia marekebisho tukazichukua na kuzifanyia kazi mwaka mmoja tukawatumia ripoti wakawatuma watu waje tena kwa ajili ya tahimini ya mwisho,”anaeleza Prof Kaale.
CHANGAMOTO
Anasema changamoto ni ushiriki mdogo wa maabara kutokana na kuwepo kwa maabara nyingi katika ukanda.
“Moja ni ushiriki lengo letu ni kuwa na washiriki wengi kwa mfano ukanda wetu kuna maabara nyingi zaidi ya 20 hadi 30 zinazoshiriki kwahiyo mwamko wa ushiriki bado mdogo hivyo ni vyema maabara kushirikia ili kuongeza viwago vya ubora.
UBORESHAJI UDHIBITI MAJARIBIO YA DAWA
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA)katika kuhakikisha kuwa wanaendelea kuboresha huduma imezindua mradi utakaowezesha udhibiti wa majaribio ya dawa, ufuatiliaji wa watu watakaopata madhara wakati wa majaribio ya dawa na mifumo ya utafiti.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mradi huo,Mganga Mkuu wa Serikali Prof Abel Makubi anasema mradi huo umehusisha taasisi saba za ndani na nje ya nchi na utaongeza kasi ya udhibiti.
“Tumekuja kuzindua mradi ambao una lenga kuboresha mifumo ya udhibiti ya majaribio ya dawa na tafiti mbalimbali tunazofanya Tanzania ,mradi huu unahusisha taasisi saba pamoja na TMDA tuna wenzetu wa NIMR,MUHAS,KCRI, ,mamalaka ya udhibiti wa dawa Zanzibar (ZAHRI) na taasisi ya utafiti Zanzibar(ZFDA)na taasisi ambazo ziko nje ya Tanzania universti ya st Andrews ya Scotlenda.
“Ujumuishaji wa taasisi wa nchi zilizoendelea na zile ambazo hazijaendelea ni utaratibu ambao upo chini ya mradi wa taasisi ya EDCTP unaotoa fedha kwenye taasisi ya nchi zinazoendelea na zilizopo Ulaya katika kuweka mifumo thabiti ya dawa na tafiti mbalimbali.
“Kikubwa ni kuweza kuimarisha mifumo ya udhibiti wa majaribio ya dawa ,mifumo ya utafiti ,namna ya kusoma na kupitisha maombi mbalimbali ya udhibiti wa majaribio ya dawa kabla ya kutumika nchini.
“Tunalenga pia Kuweka mifumo mizuri ya kufuatilia wale ambao watapata madhara wakati wanatumia dawa za majaribio huwa dawa za majaribio unakuwa hufahamu kama ni salama au sio salama hivyo unatakiwa kuweka mfumo ambao utahakikisha wale ambao wanapewa dawa hizo wanabaki kuwa salama bila kupata madhara yoyote kwa hivyo mradi huu utaboresha mfumo huo,”anasema Prof Makubi.
Anaeleza kuwa mradi huo utahusika katika kutoa mafunzo kwa wataalmu wa utafiti na walioko katika mamlaka ya udhibiti ili kuwajengea uelewa zaidi.
“Serikali na vyombo vyake tunawapongeza TMDA na kuwahimiza kuwa tafiti zote za ‘clinical trial’ zinaweza kudhibitiwa na kuwa na viwango vinavyotakiwa na mwisho wa siku ziweze kutoa majibu yanayotarajiwa kama ni dawa iweze kusaidia mwanadamu kama vipimo viweze kuonekana kugundua tunachokitarajia,”alisisitiza Prof Makubi.
ATAKA GHARAMA KUPUNGUA
Prof Makubi anatoa wito kwa TMDA kuangalia gharama za kujisajili ili uweze kupata majaribio hayo ya dawa na vipimo hasa kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
“Mliangalie hilo kuona jinsi gani mnaweza kutatua bila kubadilisha viwango vya tafiti suala hilo nalisisitiza tuwajengee uwezo watafiti wetu vijana kwasababu tunawategemea,”anasema Prof Makubi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo anasema tafiti zitakazofanywa na mradi huo zinalenga kugundua dawa au vipimo ambavyo vinaweza kutumika na mwanadamu.
“Ili utafiti ukamilike lazima kutumia hatua mbalimbali ili dawa kutumika au kutumia vipimo katika mfumo huo tunaanza na watu wachache ambao wanajitolea na baadae dawa ikionekana ina manufaa haina madhara ndio sasa inaingia hatua ya kuelekea mwishoni kwa kuanza kutumia
“Lengo letu ni kuhakikisha TMDA na vyombo vyake kupunguza kero moja wapo ya kero kuchelewa kupata uthibitisho ili mtu apewe kuwa kufanya majaribio ya dawa inachukua hadi miezi mitatu lakini kwa hii inajenga mifumo itakayoenda haraka,”anasema Fimbo.