JOSEPH HIZA Na MASHIRIKA,
ASILIMIA 80 ya Wakenya milioni 46.5 kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia 2015 inatokana na watu wenye umri wa miaka 35 kushuka chini.
Kwa mujibu wa demographia ya Kenya, taifa hilo linaongoza kwa wingi wa wapiga kura vijana katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Zaidi ya nusu ya wapiga kura milioni 19 waliojisajiri nchini Kenya ni vijana na hivyo ushiriki wao katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8 utakuwa muhimu mno.
Ni kwa sababu pamoja na mambo mengine unaweza kuamua nani atakayeshinda kiti cha urais baina ya farasi wawili Rais Uhuru Kenyatta wa Chama cha Jubilee na Raila Odinga wa muungano wa National Super Alliance (NASA).
Kwa miaka mingi, baadhi ya wanasiasa vigogo wa Kenya wamekuwa wakiwatumia vijana vibaya ili kutimiza matakwa yao ya kisiasa kisha kuwatupa.
Baadhi hununua kura kutoka kwa vijana hao wenye njaa ya ajira na fedha huku wakiahidiwa ahadi kem kem, yote hayo yakilenga kuongeza wigo wa kura wa aina hii ya wanasiasa muflisi.
Pale wanasiasa wanaposhindwa katika uchaguzi, makucha yao mabaya huonekana dhahiri, wakiwatumia kuchochea vurugu na machafuko kupinga matokeo ya uchaguzi baada ya kuwaaminisha kupitia ushawishi wa maneno laghai, fedha au viroba kuwa wameibiwa kura.
Baada ya chaguzi, vijana daima hujikuta katika hali ya sononi, kukata tamaa kwani wanakuja kushtukia kuwa ahadi zile walizopewa zilikuwa hewa!.
Si ahadi za ajira, udhamini wa masomo wala nini vile, zinazotekelezwa wakati huo huo gharama za maisha zikizidi kuuma.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, vijana wengi wa Kenya hasa wale wasiondekeza chembe za ukabila wanaonekana kuzungumza kwa lugha moja, wakisema ‘sasa basi imetosha!.’
Vijana hawa wanataka si tu kushiriki moja kwa moja katika shughuli za maendeleo ya taifa lao bali pia katika uongozi wa nchi yao.
Kwa msingi huo, wachambuzi wa mambo wanaamini safari hii, chaguzi za mwaka huu zitakuwa tofauti linapokuja suala la maamuzi ya vijana katika kura.
Kwa mujibu ya wachambuzi kadhaa wa kisiasa nchini humo, viongozi wa miaka nenda rudi kisiasa, ambao kwa miaka yote hiyo wamekuwa wakiwatumia vijana kutimiza matakwa yao kisiasa, wamekuwa wakiwateleleza vijana mara baada ya utimilizo wa ajenda zao hizo.
Kwa sababu hiyo, vijana wanaamini wakati umefika kwao kushiriki chaguzi kwa kupigiwa kura badala ya kupiga tu na kuwaajiri wanasiasa hao wakongwe.
Vijana wamepanga kuwapigia kura zaidi vijana wenzao wanaowania nyadhifa za kisiasa kwa sababu wanaamini watawapigania vyema wakiamini ndio wanaoyafahamu fika matatizo yao kulinganisha na wanasiasa wakongwe.
Katika kijiwe kimoja cha mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi, wanaonekana vijana wakiwa wamekusanyika kutazama mechi ya mtaani ya mpira wa miguu.
Licha ya kwamba lengo la uwepo wao ni kutazama mechi hiyo, hilo haliwazuii kila wapatapo nafasi ikiwamo wakati wa mapumziko wa mechi hiyo kuzungumzia uchaguzi mkuu wa Agosti 8.
Mpiga kura mmoja kijana anasimulia namna alivyochoka kutumiwa na wanasiasa wakongwe, ambao alidai wamewahi mtumia hata kumwaga damu ili tu kutimiza ajenda zao za kisiasa.
“Vijana tunapaswa kuchagua viongozi stahili tukiweka maslahi ya taifa mbele, kuhoji ilani zao za uchaguzi na kuzisoma na kupigia kura viongozi wanaofaa si wale waendekezao porojo tamu za kilaghai au wenye siasa nyepesi,”anasema.
Ripoti ya karibuni ya Benki ya Dunia ilionesha kuwa mmoja kati ya kila vijana watano wenye umri wa miaka 15 na 29 nchini Kenya hawana ajira.
Vijana wa Kenya wamepanga kutumia idadi yao kubwa kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini humo.
Mchambuzi wa siasa nchini humo, Naftali Mwaura anasema hakuwahi kushuhudia ari kubwa miongoni mwa vijana katika chaguzi kama ilivyo sasa.
“Aina hii ya demographia itakuwa na jukumu muhimu la kuamua mshindi, huenda wanashikilia matokeo ya uchaguzi huu,” Mwaura alisema.
Kwa mujibu wa Mwaura, kwa sababu hiyo, vijana watakuwa kundi lenye nguvu lisilopaswa kupuuzwa wakati wa uchaguzi wa mwaka huu kwa vile uwezekano mkubwa watakuwa waamuzi wa nani wa kuingia madarakani.
Mwaura alisema kizazi kikongwe cha wanasiasa chenye nguvu ya fedha na siasa, kinapaswa kutambua uwapo wa vijana hawa wanaoweza kuwaumbua hasa iwapo wanapambana na wagombea vijana.
Ni kwa vile vijana wanaamini taifa hili chini ya viongozi waliopo madarakani, siasa za nchi hii haziendi katika mwelekeo sahihi.
Hata hivyo, mandhari ya sasa kisiasa nchini Kenya si rafiki kwa vijana kwa vile imejaa misingi ya ukabila na migawanyiko, ambayo mara nyingi huwakimbiza vijana kutoka katika siasa au kujiweka pembeni kupiga kura.
Wakiwa wamekulia au kuzaliwa katika miji na vitongoji vyenye idadi kubwa ya mseto wa watu, wengi wa vijana hawa hawana uhusiano mkubwa na historia za kule wanakotoka baba au mababu zao, mwanya, ambao wanasiasa wa toka nitoke daima wamekuwa wakiutumia kujinufaisha.
Vijana hawa pia ni vigumu kwenda maeneo wanakotoka kunakoendekezwa ukabila wakagombea na kushinda!
Lakini pia wakati tukiona mandhari ya kisiasa si rafiki kwao, udhaifu wao huo ndio unaoweza geuka dhahabu, ni nguvu kubwa kisiasa wakiitumia vyema.
Ni kwa sababu, kutokuwa na chembe ya ukabila vijana hawa hawatapiga kura kwa misingi hiyo bali kwa mgombea wanayeamini anaweza kutatua matatizo yao.
Wakati ikiwa hivyo kwa wapiga kura vijana, pia kuna mfano wa wanasiasa vijana wasio na chembe za ukabila mmoja wao akiwa Seneta wa Nairobi, ambao sasa anawania ugavana wa kaunti hiyo, Mike Sonko.
Sonko aliyezaliwa Mombasa, asili yake ni kabila la Kamba, ana wafuasi wengi Nairobi, ambako kuna mseto wa makabila, ijapokuwa hilo halimhakikishii ushindi kwa vile ana mpinzani mwenye sifa kama zake jijini humo.
Kwa mujibu wa Kenya Shirika la taifa la Takwimu ‘(NBS), makabila makubwa ni Kikuyu (watu milioni 6.6, Luhya (milioni 5.3), Kalenjin (milioni 5), Luo (milioni 4) na Kamba (milioni 3.9).
Rais Kenyatta, chama chake cha Jubilee kinaungwa mkono na makabila ya Kikuyu analotokea na Kalenjin analotokea naibu wake William Ruto.
Hasimu wake Odinga, muungano wake wa NASA unaungwa mkono na kabila la Luo analotoka, Luhya analotoka kinara mwenzake Musalia Mudavadi na Kamba analotoka kinara mwingine Kalonzo.
Sasa ndani na nje ya makabila hayo, kundi la vijana lililojiandikisha kupiga kura, ambalo ukabila hauko ndani ya damu.
Ni kundi, ambalo halipaswi kupuuzwa na linatarajia kuamua mshindi baina ya vyama hivyo vikuu. Wacha tuone.!