UDAHILI MPYA MAFUNZO YA UFUNDI NAFUU KWA WANAFUNZI

0
1114

Na Mwandishi Wetu


BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), ni chombo kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Sura ya 129 kwa lengo la kusimamia na kuratibu mafunzo yatolewayo na taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi nchini.

Ukisoma sheria hiyo unaona kwamba vifungu Na. 5.(1) vipengele vidogo vya (d),(f) na (p) vinaelekeza Baraza kusaidia taasisi za elimu kutoa elimu ya ufundi iliyo na ubora kwa kuzingatia vigezo vya ubora wa elimu ya ufundi.

Vigezo hivi ni vile vilivyoidhinishwa na Baraza pamoja na mengine ili kuhakikisha tuzo za elimu ya ufundi  zina ubora wakati wote wa utoaji mafunzo, pia zinakubalika kitaifa na kimataifa, pamoja na kuchukua hatua madhubuti kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza malengo ya uanzishwaji wa Baraza hilo.

Wakati mwaka wa masomo ukitarajiwa kuanza tena Septemba mwaka huu, kumekuwapo maswali mengi kwa wanafunzi kuhusu mfumo ambao utatumika, kufuatia agizo la Serikali kwamba wanafunzi wakafanyiwe udahili moja kwa moja kwenye vyuo wanavyopenda kusoma.

Ni kutokana na maswali hayo, Kaimu Katibu Mtendaji wa NACTE, Dk. Adolf Rutayuga amelazimika kutoa ufafanuzi wa namna ambavyo wanafunzi watadahiliwa na kisha kujiunga na vyuo.

Anasema kwa kuwa udahili wa wanafunzi una mchango mkubwa kwenye ubora wa elimu,  katika mwaka wa masomo 2006/2007 serikali ililiagiza Baraza kuhakikisha wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya Stashahada ya Juu au Shahada wanadahiliwa kwa uratibu wa Baraza kwa kushirikiana na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

“Uratibu huu ulilenga kuondoa changomoto za  udahili wa wanafunzi kwa ajili ya kozi husika, ikiwamo baadhi ya waombaji kuchaguliwa zaidi ya chuo kimoja au kozi moja kulikosababisha waombaji wengine wenye sifa kukosa nafasi,” anasema na kuongeza:

“Ikumbukwe kwamba kabla ya hapo, hakukuwa na njia ya kuondoa udanganyifu kwenye udahili kwa kuwa baadhi ya waombaji walitumia vyeti bandia, wengine walitwishwa mzigo mkubwa wa kutoa ada kwa kila kozi aliyoomba kwenye vyuo tofauti, lakini pia baadhi ya  waombaji  hawakuwa na uhakika juu ya hadhi ya usajili wa vyuo vilivyokuwa vinatangaza nafasi za masomo.”

Kwa kutambua changamoto hizo, anafafanua kwamba Baraza kwa kushirikiana na TCU pamoja na vyuo vya ufundi na vyuo vikuu kupitia vikao vya kupitisha majina ya wanafunzi waliochaguliwa na vyuo (Joint Admission Committee Meetings) liliazimia kutafuta njia mbadala ya kuondoa changomoto hizo.

“Katika mwaka wa masomo 2009/2010, NACTE ikishirikiana na TCU ilifanya upembuzi yakinifu juu ya uwezekano wa kuondoa changamoto za udahili.

Na katika mwaka wa masomo 2011/12, Serikali kupitia wizara yenye dhamana ya elimu ya juu ilitoa fedha kwa ajili ya kuajiri mtaalamu mwelekezi ili kuanzisha udahili wa pamoja kwa ajili ya waombaji wa Shahada wenye elimu ya kidato cha sita tu.

Wahitimu wenye diploma waliendelea kudahiliwa kupitia vyuoni. Wahitimu wenye elimu ya Diploma walianza kudahiliwa kupitia udahili wa pamoja kwa mwaka wa masomo wa 2012/13,” anafafanua.

Udahili wa pamoja kwa ngazi ya cheti na diploma umekuwa na manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kudhibiti udanganyifu katika udahili uliotokana na baadhi ya waombaji kutumia vyeti vya bandia.

Anasema udahili wa pamoja pia  umesaidia kuwapunguzia waombaji gharama za kuomba udahili katika vyuo mbalimbali, kuondoa uwezekano wa mwombaji udahili mmoja kudahiliwa zaidi ya mara moja na kuwanyima waombaji wengine nafasi.

Kama vile haitoshi, manufaa mengine ni pamoja na kuiwezesha serikali kuwa na takwimu sahihi za waombaji. Udahili kwa ajili ya kufanikisha mipango ya elimu nchini, lakini pia kuwawezesha waombaji kujiunga na mafunzo kwenye taasisi zinazotambuliwa na serikali.

Aidha, Dk. Rutayuga anasema kuanzia mwaka wa masomo 2017/18 serikali imeagiza udahili wa wanafunzi ufanyike vyuoni moja kwa moja.

Dk. Rutayuga anasema kufuatia maelekezo hayo ya serikali,   NACTE imelazimika kubadili mwelekeo na mfumo wa kudahili wanafunzi, kuanzia mwaka wa masomo 2017/18 nia ikiwa ni kuboresha upatikaji wa elimu ya ufundi hapa nchini.

Dk. Rutayuga anasema kuanzia sasa udahili na uchaguzi wa wanafunzi kwa ajili ya masomo ya Astashahada na Stashahada mbalimbali yanayotolewa na vyuo vyote hapa nchini, utafanyika moja kwa moja vyuoni, isipokuwa kozi za afya na ualimu zinazotolewa na vyuo vya serikali tu.

Anasema maombi yote ya nafasi za masomo lazima yatumwe kwenye chuo husika.

Hata hivyo, anasisitiza udahili wa kozi za afya na ualimu katika vyuo vya serikali utaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na NACTE.

Katika kuboresha elimu zaidi, anasema vyuo vyote vitalazimika kutangaza au kuwafahamisha moja kwa moja waombaji majina ya watakaochaguliwa kujiunga na kozi mbalimbali; lakini wale wa kozi za afya na ualimu watatangazwa na wizara husika na kupitia tovuti ya NACTE.

“Baraza linapenda pia kuwafahamisha kuwa vyuo vimeshaanza kupokea maombi ya udahili wa wanafunzi kuanzia Mei 15, 2017 utaratibu ambao utaendelea hadi Agosti 20 mwaka huu. Majina ya waliochaguliwa yatatangazwa Septemba 14 mwaka huu. Masomo kwa mwaka wa masomo 2017/2018 yanatarajiwa kuanza rasmi Septemba 25, mwaka huu,” anasema.

“Kuanzia Agosti 21 hadi 27 mwaka huu, vyuo vitafanya uchaguzi wa wanafunzi walio na vigezo vya kusoma kozi husika. Lakini pia vitatumia utaratibu husika (Machinery organs) kupitisha majina ya wanafunzi waliochaguliwa,” anasema na kuongeza:

“Baada ya hapo vyuo vitatuma majina ya wanafunzi waliochaguliwa NACTE kwa njia ya mtandao utaratibu ambao utaendeleo hadi Agosti 31 mwaka huu.”

Dk. Rutayuga anasema NACTE itapokea majina ya wanafunzi waliochaguliwa kutoka vyuoni kwa njia ya mtandao na uhakiki wa wanafunzi hao utaanza Septemba mosi hadi 13 mwaka huu.

Nia ya kuhakiki wanafunzi waliochaguliwa ni kuangalia kama wana vigezo vinavyotakiwa, lakini pia kubainisha wanafunzi waliochaguliwa katika vyuo tofauti (multiple selections).

Anasema baada ya zoezi hilo, NACTE itatuma taarifa ya uhakiki wa majina ya wanafunzi waliochaguliwa kwenye vyuo kwa njia ya mtandao.

Kaimu Katibu Mtendaji huyo wa NACTE anasema maelezo ya uhakiki wa wanafunzi waliochaguliwa na chuo utahusisha kuangalia mambo muhimu yakiwamo sifa za kila mwanafunzi alizonazo, kulinganisha matokeo yake ya mitihani ya kidato cha nne na wale waliomaliza kidato cha sita.

Anayataja mambo mengine kuwa ni kuangalia kama chuo alichoomba mwanafunzi kimesajiliwa na kutambuliwa na mamlaka husika, kuangalia kama programu ambayo mwanafunzi amechaguliwa inatambuliwa na NACTE au TCU, pia kuangalia kama chuo kimezingatia uwezo wake wa kupokea wanafunzi (enrolment capacity).

Katika utaratibu huo mpya, Dk. Rutayuga anasema baada ya mchakato wote huo, chuo kitalipia gharama za uhakiki wa kila mwanafunzi aliyechaguliwa kiasi cha Sh 20,000 kwenye mfumo wa udahili na uhakiki wa wanafunzi kupitia ‘Institutional Panel.’

Anasema kwakuwa utaratibu huu ni  mpya, sifa za kujiunga, kozi zilizosajiliwa, uwezo wa chuo kudahili wanafunzi, gharama za masomo na vyuo vyote vinavyotambuliwa na NACTE vimeorodheshwa kwenye kitabu cha mwongozo wa udahili.

Anasema baada ya kupokea majina yaliyohakikikiwa chuo kinatakiwa kuwaarifu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na chuo husika.

Anaongeza pia kutakuwa na utaratibu wa kuondoa wanafunzi waliochaguliwa katika vyuo tofauti, hii ni chini ya mfumo huu mpya.

Anasema kuanzia Septemba 25 hadi Oktoba 16 mwaka huu, vyuo vitaanza kupokea wanafunzi waliochaguliwa tayari kwa ajili ya masomo.

Kaimu Katibu Mtendaji huyo anasema vyuo vitaanza kuwasajili wanafunzi wote waliofika vyuo kupitia Institutional Panel, ambapo mfumo (system) utatoa namba ya usajili wa mwanafunzi husika.

“Mwanafunzi akisha sajiliwa kwenye chuo husika, hatasajiliwa tena kwenye chuo kingine. Akitaka kusajiliwa chuo kingine mfumo utaonesha kwamba tayari amesajiliwa katika chuo fulani,” anasema.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here