26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Uchunguzi mlipuko wa kemikali ulioua 100 Beirut waanza

BEIRUT, LEBANON

Rais wa Lebanon, Michel Aoun, amesema uchunguzi ulioanzishwa kuhusu mlipuko mkubwa ulioutikisa mji mkuu wa nchi hiyo Beirut utatoa majibu ya haraka iwezekanavyo juu ya jinsi mkasa huo ulivyotokea.

Akizungumza mapema katika hotuba iliyorushwa na televisheni wakati wa kuanza kikao cha Baraza la Mawaziri, Rais Aoun alisema wamedhamiria kuchunguza na kufichua kile kilichotokea na kisha kuwaadhibu wale walihusika.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa uzembe wa miaka mingi wa kuhifadhi kemikali hatari katika ghala moja karibu na bandari mjini Beirut ndiyo chanzo cha mlipuko wa juzi uliowauwa watu 100 na kujeruhi maelfu wengine.

Rais Aoun ameitumia hotuba yake kuendelea kutoa rai kwa mataifa mengine duniani kuisadia Lebanon katika juhudi zinazoendelea za kutafuta wahanga pamoja pia na kuzishukuru nchi ambazo tayari zimeahidi kutuma msaada.

“Ninawashukuru maofisa wote wa nchi jirani na rafiki waliowasiliana nasi kuonesha mshikamano na nia yao ya kutusaidia, ninawarai kuongeza kasi ya kuzisaidia hospitali zetu, familia zilizoathirika na kutusaidia kurekebisha uharibifu ulioyakumba majengo na bandari ya Beirut.” amesema Auon.

Siku nzima ya jana vikosi vya uokozi vimeendelea na juhudi za kuwatafuta watu waliokwama kutoka vifusi vya majengo yaliyoporomoka pamoja na kuanza matengenezo baada ya mlipuko wa jana kuharibu kwa sehe.

UOKOAJI

Katika hatua nyingine vikosi vya uokozi vimeendelea na juhudi za kuwatafuta wahanga kutoka vifusi vya majengo yaliyoporomoka kutokana na mlipuko huo.

Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Lebanon, George Ketteneh, ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, kuwa idadi ya vifo kutokana na mkasa huo inaweza kuongezeka katika wakati ambapo watu 4,000 wamejeruhiwa kwa kiwango tofauti.

Ofisa mmoja wa vikosi vya usalama alisema bado wanaendelea kutafuta watu waliokwama chini ya mabaki na vifusi vya majengo hususani katika eneo la kuzunguka bandari ya Beirut ambako mlipuko ulitokea.

Mapema jana vikosi vya uokozi vilikuwa vikiondowa mabaki ya vitu ili kufungua barabara na kuanza matengenezo baada ya mlipuko wa juzi kuharibu kwa sehemu kubwa majengo, magari na kuzua taharuki kwa wakaazi wa mji wa Beirut.

Hadi sasa ripoti zinasema chanzo cha mlipuko huo ni moto uliozuka katika ghala moja iliyohifadhi shehena ya fashifashi na kemikali hatari ya Amonium Nitrate ambayo ilikamatwa miaka sita iliyopita.

Waziri Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab, ametoa wito kwa

mataifa yote na marafiki wa nchi yake kutoa msaada kwa taifa hilo dogo akisema linashuhudia janga kubwa kutokana na maafa ya mkasa wa mjini Beirut.

Diab pia ameahidi kuchukua hatua kwa wote waliohusika na kutokea kwa janga hilo.

“Kilichotokea hakitopita bila uwajibikaji, wale wanaohusika watalipa kutokana na janga hili. Hii ni ahadi kwa waliopoteza maisha na waliojeruhiwa. Hii ni azma ya taifa, kutakuwa na ukweli uliotangazwa kuhusu ghala hatari ambalo limekuwepo tangu 2014, kwa miaka sitra” alisema Diab.

Mataifa mbalimbali duniani yameendelea kutuma salamu za pole na rambarambi kwa Lebanon huku mengi yakiahidi kutuma msaada wa uokozi na fedha kuisadia nchi hiyo kupambana na maafa yaliyotokea.

Iran, Ufaransa, Ubelgiji, Jamhuri ya Czech, Uturuki, Uholanzi na Uingereza ni miongoni mwa mataifa yaliyosema yanatuma waokoaji na shehena za vifaa na vyakula kwenda mjini Beirut kuongeza juhudi za utafutaji wahanga na kuwasaidia waliojeruhiwa.

Israel pia ambaye imekuwa kwenye mvutano na Lebanon imesema iko tayari kuwatibu majeruhi wa mlipuko wa mjini Beirut.

Mlipuko huo ambao ni mbaya kabisa katika historia ya taifa hilo la Mashariki ya Kati umetokea wakati Lebanon inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi kuwahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa

vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1975-1990.

Raisi wan chi hiyo, Michel Aoun alisema kwamba tani 2,750 za ammonium nitrate zilikuwa zimewekwa vibaya katika ghala moja kwa miaka sita.

Aliitisha kikao cha dharura jana na kutangaza hali ya dharura ya wiki mbili .

Alitangaza kuwa serikali itatoa dola milioni 66 kusaidia kupunguza athari za tukio hilo kwa taifa hilo ambalo mbali ya mzozo wa uchumi linazongwa pia na kadhia ya janga la virusi vya corona.

Kemikali ya Ammonium Nitrate inayodaiwa kusababisha mlipoko huo, ilikuwa imeshushwa kutoka kwenye meli iliokamatwa katika bandari hiyo 2013 na kuwekwa katika ghala.

Mlipuko huo unajiri wakati mgumu kwa upande wa taifa hilo huku likikabiliwa na mgogoro wa kiuchumi unaosababishwa na mgawanyiko wa jadi pamoja na mgogoro mwingine wa virusi vya corona.

Hali ya wasiwasi pia ilikuwa juu kabla ya uamuzi wa siku ya Ijumaa kuhusu kesi ya mauaji ya aliyekuwa waziri mkuu Rafik Hariri 2005.

Je ni nini kilichotokea?

Mlipuko huo ulitokea muda mfupi baada ya mwendo wa saa kumi na mbili siku ya Jumanne.

Mwandishi wa BBC aliyekuwa katika eneo hilo aliripoti miili ya watu waliokuwa wameuawa na uharibifu mkubwa unaoweza kuifunga bandari

hiyo ya Beirut kwa muda.
Vyombo vya habari

viliwaonyesha watu wakiwa wamenasa chini ya vifusi.

Shahidi mmoja alielezea mlipuko huo kuwa mkubwa hali inayoweza kusababisha watu kuwa viziwi, huku kanda ya video ikionesha magari yalioathirika pakubwa mbali na majumba yalioharibika.

‘’Majumba yote yaliokuwa karibu na mlipuko huu yameanguka. Ninatembea juu ya vigae na vifusi wakati wa usiku’’, shahidi mmoja karibu na bandari hiyo aliambia AFP.

Hospitali zilidaiwa kushindwa kuhimili idadi ya watu na majumba mengi yaliharibiwa.

Mlipuko huo ulisikika umbali wa kilomita 240 katika kisiwa cha Cyprus mashariki mwa bahari ya mediterenean, huku watu katika eneo hilo wakisema walidhania lilikuwa tetemeko la ardhi.

Evelyn Wanjiru ni raia wa Kenya anayeishi na kufanya kazi mjini Beirut umbali wa dakika 10 kwa gari kutoka eneo kulipotokea mlipuko.

Wanjiru anasema alikuwa anatarajia kuhudhuria mkutano na alipofika nyumbani kutoka kazini akaanza kujitayarisha lakini ghafla akasikia nyumba inatetemeka na vitu vikaanza kudondoka.

‘’Nilipoanza kusikia mtetemeko nikatoka bafuni mbio na kwenda kuangalia rafiki zangu ninaokaa nao karibu. Lakini nusu ya safari nilisikia kitu kinanivuta kwa nyuma, nikagongwa mgongoni na kuanguka’’, Wanjiru amesema.

Wanjiru anasema rafiki yake

mmoja alimuona akiwa ameanguka akamsaidia kusimama na kukimbilia usalama wao.

Wasijue kwamba kule walikokuwa wanakimbilia ndiko kunakotoka mvutano na shinikizo la juu na wakati huohuo nyumba yao bado inaendelea kutetemeka kweli.

Wakajiona wamekutana wanne kila mmoja anakimbia na hajui anakoelekea.

‘’Tulikumbatiana na kupeana moyo tukaelekea upande wa pili kwenye kona fulani na tukasimama.’’ Wanjiru ameelezea.

Kwasababu hawakuwa wanajua nini kinachoendelea, baada ya dakika mbili hivi nyumba ikaacha kutetemeka, wakakimbilia kwenye ushoroba wa juu na hapo ndipo walipoona moshi mkubwa ajabu hewani unafuka uliokuwa wa rangi nyekundu.

‘’Tukaanza kusikia sauti za magari ya kubeba wagonjwa na hapo ndipo tulipoamua kufungua televisheni’’. Amesema Wanjiru.

Kwa mujibu wa Wanjiru, hospitali iliyokuwa karibu ilichukua watu mia tano ikasema haiwezi kuchukua idadi zaidi ya hiyo na waathirika wengine wakaanza kupelekwa katika hospitali zingine.

‘’Karibu na eneo la mlipuko kuna mahoteli na huku maisha ni saa 24 yaani maisha ya raha hivi’’ amesema Wanjiru.

Ingawa Serikali ilikuwa imesema kwamba chanzo cha mlipuko huo huenda ikawa ni fataki lakini kwa jinsi hali ilivyokuwa, vitu kuanguka vyenyewe na mitetemeko ya ajabu, wakaazi wamelitilia mashaka.

Tukio hilo bado limeendelea kuzua maswali na wasiwasi mkubwa kwa umma hasa kwa kushindwa kung’amua ni nini hasa kilichotokea.

Ammonium nitrate ni nini?

Amonium nitrate ina matumizi tofauti lakini matumizi yake mawili maarufu zaidi ni kilimo kama mbolea na kutengeneza vilipuzi.

Inalipuka kwa haraka inapokutana na moto na inapolipuka hutoa gesi yenye sumu ikiwemo ile ya nitrogen oxide na gesi ya ammonia.

Na kwasababu ni rahisi kulipuka kuna masharti makali kuhusu jinsi ambavyo inafaa kuhifadhiwa ili kusalia salama ikiwemo sharti kwamba eneo la kuihifadhi linafaa kuzuiwa kuvutia moto.

Hali ikoje nchini Lebanon?

Lebanon inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa huku kukiwa na maandamano dhidi ya Serikali kwa kushindwa kukabiliana na tatizo la kushuka kwa uchumi tangu mgogoro wa kiuchumi wa 1975-1990.

Wengi wanalaumu maofisa wakuu Serikalini ambao wanatawala siasa kwa miaka kadhaa na kujilimbikizia mali huku wakishindwa kufanya mabadiliko muhimu ya kutatua tatizo la taifa hilo.

Raia wanakabiliwa na tatizo la kukatwa kwa umeme kila siku, ukosefu wa maji safi ya kunywa na huduma ya afya .

Kumekuwa na hofu katika mpaka na Israel ambayo ilisema wiki iliopita kwamba ilizuia jaribio la Hezbollah kuingia katika himaya ya Israel.

Lakini afisa mmoja mkuu wa Israel ameambia BBC kwamba Israel haina uhusiano wowote na mlipuko wa Beirut.

Mlipuko huo ulitokea karibu na eneo ambalo mlipuko mkubwa wa gari ulimuua waziri huyo wa zamani Hariri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles