26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

UCHUNGUZI MALI ZA CHAMA:VIGOGO CCM MATUMBO JOTO

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


RIPOTI ya kuchunguza mali za Chama Cha Mapinduzi (CCM), imebaini upotevu mkubwa wa mali uliosababishwa na mikataba mibaya, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeleshaji wa miradi.

Kutokana na hilo, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli, ameagiza ripoti hiyo kupelekwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ndani ya mwezi huu ili wajadili na viongozi kutoa maelekezo.

Desemba mwaka jana, Rais Magufuli aliunda tume yenye wajumbe tisa kufuatilia mali za chama hicho tawala.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Dk. Bashiru Kakurwa, alieleza upotevu huo wa mali za CCM mbele ya Rais Magufuli wakati akimkabidhi ripoti hiyo, katika Ofisi ndogo ya CCM Lumumba, Dar es Salaam jana.

“Tume imebaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibaya, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama,” alisema mwenyekiti huyo.

Pamoja na mambo mengine, Dk. Kakurwa alisema kamati hiyo imefanya kazi kwa miezi mitano ambapo imekusanya taarifa, imehakiki na kuchambua taarifa na nyaraka zenye maelezo kuhusu idadi.

“Pia imehakiki aina na hali ya mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na chama, imeangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wa mali na kukusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya mikakati na ushauri wa kusimamia mali za chama.

“Uhakiki umefanyika kwa kutembelea maeneo yenye mali za chama, kuwahoji watu mbalimbali wakiwemo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa, upitiaji wa nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo,” alisema.

Aidha, alisema uhakiki huo umefanyika katika mali za chama zilizo chini ya Baraza Kuu, jumuiya za chama na kampuni za chama.

Kwa upande wake, Rais Magufuli aliipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya, huku akisema ripoti hiyo itawasilishwa katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kufanyiwa uamuzi.

“Nilipokuwa nateua tume hii, nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki sasa ni kuifanyia kazi,” alisema Rais Magufuli.

Aliwaagiza wajumbe wa sekretarieti kuanza kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na kwamba masuala mengine yataamuliwa na vikao vikuu vya chama.

Alisema CCM imeamua kuchukua hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa dhamira yake ya kupiga vita rushwa na ufisadi, huku akisema na tume ya Dk. Kakurwa imefanya kazi nzuri.

“Huwezi ukaanza kupiga vita rushwa na ufisadi ndani ya Serikali wakati chama kina rushwa na ufisadi, chama nacho tunataka tukisafishe, mambo ya rushwa na ufisadi yaishe ili Tanzania iende vizuri.

“Ndiyo maana tumeunda Tume ya Dk. Bashiru Ally, imefanya kazi nzuri sana na ripoti hii tutaipeleka Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ndani ya mwezi huu ili tuijadili na viongozi watoe maelekezo,” alisema Rais Magufuli.

Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, aliipongeza tume hiyo huku akisema imefanya kazi kubwa na kudhihirisha kuwa baadhi ya watu walioonekana kukisaidia chama, hawakuwa wanakisaidia bali kujinufaisha.

Desemba 20, mwaka huu, Rais Magufuli, aliunda tume ya kuchunguza mali za CCM iliyoongozwa na Dk. Kakurwa, huku wajumbe wake wakiwa ni Walter Msigwa, Albert Msando, Galala Wabanhu, Albert Chalamila, William Sarakikya, Komanya Kitwara, Dk. Fenela Mkangara na Mariam Mungula.

Kamati hiyo iliyopewa hadidu rejea, ilitakiwa kufanya kazi ya uchunguzi wa mali za CCM na kampuni zake ikiwemo kupitia mikataba mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles