23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

UCHUNGU WA PROFESA MUHONGO UKO WAPI?

profesa-sospeter-muhongoMWITIKIO wa viongozi wa juu serikalini, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Rais Dk. John Magufuli, umekifanya kitendo cha hivi karibuni cha Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) cha kuidhinisha ongezeko la bei za umeme kionekane kama cha kukurupuka.

Lakini ukweli ni kuwa katika kupitisha ongezeko hilo la bei kutokana na maombi ya Tanesco, hakikuwa kitendo cha kukurupuka. Ewura ilifuata taratibu zote kama zinavyoainishwa katika sheria na pia katika Kanuni za Kupanga Bei za Umeme za mwaka 2013 (Electricity (Tariff Setting) Rules, 2013).

Baada ya Ewura kutimiza wajibu wake kisheria na kikanuni ndipo viongozi hawa wakaibuka; wakasema waliyoyasema na wakachukua hatua walizochukua.

Binafsi sikuafiki wazo la kupandishwa kwa bei ya umeme kwani hatua hiyo itawaumiza wananchi wa kawaida na uchumi wa nchi, lakini pia sikubaliani na utaratibu ambao viongozi wa juu wameuchukua baada ya Ewura kuafiki ongezeko la bei ya umeme.

Siafiki kwa sababu Ewura ilifuata sheria, kanuni na taratibu zote katika kulishughulikia suala hilo wakati viongozi wetu hawa hawajatueleza wanatumia sehemu gani ya sheria kupinga kazi iliyofanywa na Ewura.

Katika kauli zake, kati ya mambo mengi, Waziri Muhongo ametaka kuwaaaminisha Watanzania kuwa Ewura haikufuata taratibu katika kuidhinisha maombi ya Tanesco ya kuongeza bei ya umeme.

Lakini ni utaratibu huohuo ambao Ewura ilikuwa imeutumia iliposhughulikia maombi ya Tanesco kuongeza bei za umeme katika miaka ya nyuma na wala hatukusikia kuwa ilikuwa imekiuka sheria na kanuni.

Nadhani Profesa Muhongo anawajibika kutoa ufafanuzi wa vipengele mahususi vya sheria na kanuni ambavyo Ewura ilivikiuka wakati inashughulikia ombi la Tanesco.

Katika jambo jingine, Profesa Muhongo ameonyeshwa kusikitishwa sana na kitendo cha watumishi wa Tanesco kujilipa bonasi ya mamilioni ya shilingi kila mwisho wa mwaka. Anasema alikataa kupitisha bonasi hiyo mwaka juzi na ni dhahiri kuwa hata mwaka jana alikataa kuidhinisha pia.

Waziri Muhongo anasema pia kuwa wakati wa mchakato wa Ewura kutafuta maoni ya wadau, watu wengi walionekana kupinga ongezeko la bei lililoombwa na Tanesco.

Lakini kwa miaka mingi sasa Watanzania hao hao waliopinga ongezeko la bei za umeme wamekuwa wakiitaka wizara kusitisha mara moja malipo ya ‘capacity charges’ kwa kampuni ya Pan African Power (iliyonunua Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited – IPTL).

Lakini Profesa Muhongo, ambaye aliona malipo la bonasi ya Sh milioni 60 kwa mwaka ni makubwa bado haoni malipo ya takribani dola za Kimarekani milioni nne kila mwezi (zaidi ya Sh bilioni nane kwa thamani ya dola ya sasa) kuwa ni mzigo kwa Watanzania!

Hapa mtu unaweza kujiuliza hivi uchungu wa Waziri Muhongo upo wapi hasa?

Kwa wenye kumbukumbu wanafahamu kuwa ongezeko hili la majuzi la bei ya umeme si jambo lililoibuliwa mwaka jana. Jambo hili limo kwenye mpango wa muda wa kati wa Tanesco ambao uliainishwa tangu mwaka 2014. Mipango hiyo ambayo iliridhiwa na Wizara, inalenga kuifanya Tanesco iweze kuondokana na madeni na kuanza kujitegemea.

Na ni vema tukafahamu pia kuwa kiwango cha bei ya bidhaa yoyote ukiwamo umeme pamoja na kuangalia uwezo wa watumiaji, lakini kwa kiasi kikubwa huzingatia gharama za uzalishaji wa bidhaa husika.

Kama gharama za uzalishaji zinalitaka Tanesco kuongeza bei ya umeme kwa kiwango ambacho Ewura iliidhinisha baada ya kufanya hesabu za kitaalamu, ni vema Waziri Muhongo akatueleza jinsi ambavyo Tanesco wanaweza kuzalisha umeme na kuuza kwa bei ya kuwajali wananchi bila ya kupata hasara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles