UCHU, GHILBA, BAHATI YATAWALA ‘BETTING’

0
759

 

Na Joseph Lino


NI kawaida kwa siku hizi mchana au usiku vijana hukusanyika sehemu za starehe, ikiwamo baa au klabu na katika vituo vya michezo ya kubashiri matokeo, hasa mchezo wa soka nchini au mashindano ya nje. Pool table nyingi sasa zimegeuka na kuwa vijiwe vya betting rasmi au sio rasmi, mradi watu wanatengeneza pesa. Kando yake huwa uvutaji wa shisha. Starehe tupu!

Kila siku na hasa mwishoni mwa juma vijana huhangaika kununua tiketi kwa ajili ya kubashiri, ikiwa njia moja ya kujipatia pesa kiurahisi bila kutumia nguvu zaidi. Mambo haya yanafanyika wazi na hadharani, huku kuna sheria inayozuia kiserikali na wakati mwingine kidini inazuiliwa.

Kwa wengi tunaona kitu cha kawaida, lakini kimaadili ni mmomonyoko wa hali ya juu na hivyo juhudi stahiki zifanywe kuzuia janga hili, kwani likizoeleka lina nafasi ya kuharibu  jamii yetu kwa kuchukia kazi na kuendeleza starehe zinazoambatana na utumiaji madawa ya kulevya, shisha  na  biashara ya  umalaya, kwani  vyote huenda pamoja.

Kuibuka kwa biashara ya kamari au ‘betting’ kama inavyojulikana ili ikubalike na jamii ni mwendelezo wa mmomonyoko wa maadili.

Biashara hii inaendelea kwa kasi na kufadhiliwa na mitandao ya nchini na nje ya nchi ambayo inaendelea kukua kwa kasi na kuleta hisia tofauti kutokana vijana wengi wanaojihusisha huwa hawana kazi maalumu zaidi ya kuwaza pesa zitakazopatikana kupitia kubashiri matokeo ya michezo, hususan mechi za mpira za klabu maarufu.

Tunavyojua Watanzania hupenda michezo, hasa mpira wa miguu ambapo makundi ya watu hukusanyika na marafiki katika maeneo ya kuonyesha mpira wa miguu, lakini kuna kitu kinachoendelea ndani ya mioyo yao ambacho huwezi kutambua kiurahisi zaidi ya kuwaza kushinda pesa.

Michezo ambayo ni burudani kwa wengi sasa imegeuka kuwa biashara na mtaji wa  kuzalisha pesa au kupoteza kwa kuwa bingwa wa kujua wachezaji husika na hivyo kuwa na uwezo na uthubutu wa ubashiri wa ushindi; ndio pesa ilipo hapa, kwani wachezaji wanapocheza mpira watazamaji wanacheza kamari ya kubashiri matokeo na kiuchumi inawalipa wanaobashiri.

Idadi kubwa ya vijana nchini kati ya miaka 18 hadi 40 sasa wamekuwa walevi wa michezo hiyo, ambayo ni haramu na kinyume cha sheria wanajihusisha na michezo ya betting ambapo wanatumia pesa nyingi na hivyo kuongeza kiwango cha uhalifu mitaani, kwani fedha mpya lazima ipatikane kuendesha mchezo, kwani kamari ikishamiri akili hupotea na mtu huingia katika matatizo makubwa ya madeni, kwani baadhi ya wachezaji hufanya hivyo kwa minajili ya kufanya wizi kwa wenzi wao.

Kwa sasa hakuna takwimu sahihi zinazoonyesha watu wangapi wanajihusisha na masuala ya kamari ya ‘betting’, hasa katika michezo wa soka kila mara.

Ripoti ya Gambling Outlook 2014 iliyotolewa na kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa mahesabu PricewaterhouseCoopers, ilibainisha Kenya, Nigeria na Afrika Kusini michezo ya betting inakadiriwa kuwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 37 ifikapo mwaka 2018. Tanzania wakati huo ilikuwa bado kuingia kwenye zahama hii, lakini sasa biashara hiyo imekolea na kuanzisha hata taasisi kubwa kama SportPesa bet,  inayodhamini mchezo wa mpira kimataifa.

 

Michezo ya kubashiri nchini ni biashara inayokua kwa kasi katika soko lake duniani kote kinyume cha sheria.

Kampuni za betting kutoka Marekani na Ulaya wanapanua biashara katika bara la Afrika kutokana na fursa nyingi za biashara michezo ya betting na serikali kufumbia macho madhila ya mchezo huo kwa jamii husika.

 

Walengwa ni vijana

Vijana ni nguvu kazi ya taifa lolote lile, kwa hiyo chochote kinachotoa kundi hilo kwenye uzalishaji mali ni kibaya kama kitaendelea muda mrefu bila kuwekewa vikwazo.

Nchini Tanzania, vijana wengi wanaopendelea kucheza michezo ya kubashiri wanasema kwamba biashara hii inatoa fursa za ajira isiyo rasmi kwa vijana na kutoa pesa za haraka kama kipato  au mtaji bila kujali  athari zake kwa watu wa kawaida. Athari mbaya zaonekana kuwa nyingi kuliko faida.

Wengine huenda mbali zaidi kwa kudai pia huzalisha mapato kwa serikali na kuchangia ukuaji wa uchumi. Ukweli wake haujathibitishwa au kukataliwa na takwimu, lakini kwa wale wanaosimamia sheria wanadai kuwa mchezo huo hutumika kusafishia fedha haramu kuwa halali na majangili ya kimataifa kwa kuanzisha ‘kampuni dodoki’ za kufyonzea kipato.

Gazeti la Mtanzania tunaangalia kiundani kiini cha biashara ya kubashiri nchini.  Ni ukweli uliyowazi kwamba biashara hii inaendelea kupanuka nchini kote kwa haraka mno kupitia kampuni kubwa za kubashiri duniani na hivyo kuleta dhana potofu kuwa biashara ni halali kwa sababu inafanywa na wakubwa na wenye nacho, kwani ukubwa ni dawa yaani ‘might is always right’. Kwani kuna tofauti gani na karata tatu?

Pia tunaangalia namna biashara ya kubashiri inavyotengeneza pesa, na vitu kadha vya kuzingatia na weledi unaotumika.

Kamari ni moto nyikani?  

Kwa uchunguzi wa juu juu na kwa mtindo wa utafiti uliofanywa na Mtanzania jijini Dar es Salaam na kwingineko kuhusiana na biashara hii, sababu kubwa inayochangia kushamiri kwa biashara ni idadi kubwa ya watu na hasa vijana nchini ambao hawana kazi ya ajira rasmi.

Ukosefu wa ajira rasmi unafanya idadi kubwa ya vijana wengi wao kugeukia kwenye michezo ya kubahatisha, ‘betting’, ambapo wanadai kuwa biashara hiyo inatoa fursa ya kuzalisha kipato na tumaini potofu la kufanikiwa kimaisha nchini. Wengine wameuza vitu vya thamani vya wazazi, wapenzi na wenzi ili kuweza kushiriki mchezo huo wenye mvuto mkubwa kwa vijana wakiwa na matumaini ya ‘kutoboa kwenye maisha.’ Ndoto hizo mara nyingi huishia gizani. Ni wachache tu hufanikiwa, kwani masharti ya ushindi ni magumu sana.

Katika michezo ya betting vijana hutumia kuanzia Sh 500 ambapo si kiasi kikubwa na hata ukikosa na hivyo hufanya wengi kushiriki kwa hasara. Mtu akibahatika hushinda mamilioni ya pesa taslimu na wengi kukosa.

Kutokana na hili, sio kitu cha kushangaza michezo ya betting hugeuka kuwa tabia sugu kwa mamilioni ya vijana ambao kila siku wanashinda katika maduka ya kubashiri wakijaribu bahati zao.

Tabia sugu ya betting husababisha vijana wengi kuingia katika madeni, ulevi na uhuni wa mwenendo na tabia. Kwani hufanyika kwenye sehemu za starehe, saa mbaya za usiku wa manane  kwenye michanganyiko ya jinsia.

Sababu nyingine ambayo imefanya soko la biashara hii kwenda kwa kasi ni kutokana Watanzania wengi hupenda michezo wa mpira wa miguu, kuna mashabiki wengi wa soka nchini, hasa vijana  wanaofuatilia  ligi za Ulaya, ikiwamo Uingereza, Hispania, Italia, Ujerumani  na Ufaransa.

Watanzania hubashiri matokeo ya mechi katika magoli ya kufunga au wachezaji wakaofunga  na hata pointi.

 

Aidha, masharti nafuu ya udhibiti na uthabiti wa michezo ya betting imeweza kufanya ongezeko la biashara hii nchini, ambapo cha kushangaza kampuni zote zinatoka nje na kuonekana kupata faida kubwa sana.

Hata hivyo, makampuni hayo yanaonekana hufanya vizuri katika nchi za Afrika ambako sheria zake bado hazijawa ngumu na maofisa wa serikali kutofuatilia kwa karibu masharti ya mchezo ambapo hakuna mamlaka imara na wafuatiliaji wa haki za wachezaji ambapo kuna madai ya kudhulumiwa zawadi zao za ushindi kwa njia moja au nyingine na waendeshaji wakorofi wasio waaminifu.

Kuna mchezaji mmoja kule Singida inasemekana alishinda Sh milioni 50, lakini waendeshaji mchezo walitaka kumdhulumu hadi Gaming Board walipoingilia kati ndipo akalipwa fedha yake. Si mchezo!

 

Pia ongezeko la matumizi ya intaneti katika simu za mikononi kumechangia kiasi kikubwa nchini na bara la Afrika kwa ujumla.

Baadhi ya makampuni yanashirikiana na watoa huduma za simu za mikononi katika biashara hii ambapo wateja hubashiri kupitia simu zao.

 

Biashara ya betting nchini

Biashara ya betting nchini inachangia kiasi cha Sh bilioni 1.6 kwa mwezi, na kampuni za michezo ya kubashiri ni 13, ambapo kuna vituo 231 nchini kote.

Kwa upande wa Dar es Salaam kuna vituo vya kubashiri 173.

Baadhi ya kampuni za kimataifa zinashiriki na hivyo kuongeza ushindani  nchini na kumekuwa na ongezeko kubwa la ushiriki na imani ya kufanikiwa sana, hasa baada ujio wa SportPesa kutoka nchini Kenya, ambayo imekuja kwa kishindo, huku ikidhamini timu za Simba na Yanga, ambao ni nyota katika fani ya mpira wa miguu.

Kampuni hiyo ina wateja zaidi ya milioni moja na hukusanya mapato zaidi ya dola za Marekani milioni 40 kwa mwaka.

Namna ya kuzalisha pesa

 

Kimsingi biashara ya michezo ya kubashiri hutegemea bahati ya mtu, lakini siku hizi kumezuka kundi la watu wanaojiita ‘wataalamu wa kubashiri’ au mafundi ambao misingi yao ni watu kubashiri na hutegemea hisia, umaarufu, mantiki na utafiti wa takwimu na kanza data; lakini bahati tu ndiyo inayotawala. Wengine hutumia waganga wa kienyeji na ramli kuongeza uwezo wao wa ‘kutoboa bahati’.

Mwisho wa yote ni kuwa kila mwisho wa mchezo kuna washindi na walioshindwa. Ukweli wa mambo wa biashara hii ni hkuwa kutegemea pesa za walioshindwa na kuwalipa washindi. Mara nyingi kimahesabu washindi ni wachache kuliko walioshindwa na hivyo kufanya ongezeko la thamani ya mchezo husika na kujenga msingi wa maendeleo yake.

 

Kampuni za betting hutumia mbinu rahisi ambazo huchukua pesa za walioshindwa na kufanya uwiano makini kwa malipo ya washindi.

Hata hivyo, tukiangalia uhalisia wenyewe ni kwamba, kampuni hizi huzalisha mapato mengi bado na hivyo kuna mambo ya kuangalia kwa upande wa mapato ya serikali na watu wa kawaida kama wanatendewa haki, hasa wale ambao si washindi na wamekuwa wamepoteza pesa zao.

Hii si biashara ndogo, kwani kwa takwimu za mwaka 2015/16, serikali ilizalisha Sh bilioni 21.9, sawa na dola milioni 9.79, ikilinganishwa na mapato yaliyotokona na biashara ya kamari ya Sh bilioni 21.2, sawa dola milioni 9.48.

 

Mchango wa sekta ya michezo ya kubahatisha kwenye uchumi unachangia asilimia 1.5 ya pato la taifa.

 

Katika bunge la bajeti la mwaka huu, serikali ilisema kuwa, inaweza kupata fedha nyingi kutokana na michezo ya kubahatisha, hivyo kuanzia Julai 1, 2017 mapato yote yatakayotokana na michezo ya kubahatisha yatakusanywa na TRA.

Mapato hayo yatawasilishwa mfuko mkuu wa serikali, serikali itaweka utaratibu wa kurejesha fedha hizo kwenye bodi ya michezo ya kubahatisha baada ya kuhakiki mahitaji na matumizi ya bodi, kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Ni kweli kwenye fedha msimamo huwa hautabiriki, ila huwa funika kombe mwanaharamu apite na hivyo haramu huwa halali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here