Na VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM
UCHANGIAJI wa damu katika benki ya taifa ya mpango wa damu salama ni muhimu kunusuru maisha ya Watanzania kutoka maeneo mbalimbali nchini, imeelezwa.
Hivyo Watanzania wameaswa kuendelea kujitolea katika utoaji na uchangiaji wa damu kwa kuwa mahitaji ya damu bado ni makubwa.
“Jukumu la kuchangia damu limapaswa kuwa na kila mtanzania, kila kampuni, kila taasisi, kila sekta na kila mmoja wetu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Mrisho Yassin,
Alikuwa akiongoza wafanyakazi wa Kampuni ya Swisspor walipokuwa wakichangia damu kwa waratibu wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama jana.
Alisema huu ni mwaka wa pili mfululizo kwa kampuni yao kuchangia damu katika kuokoa maisha ya Watanzania.
“Tumejitahidi kuhamasisha wafanyakazi wetu ofisini kuendelea kujitolea damu kama sehemu ya kurudisha fadhila kwa wananchi tunaowatumikia kwa uaminifu mkubwa.
“Mahitaji ya damu nchini bado ni changamoto kubwa, tunapaswa kuweka nguvu kuwaelimisha wananchi kuendelea kuchangia damu kunusuru majeruhi wa ajali na wagonjwa mbalimbali wenye uhitaji kwa kuboresha benki ya damu ya taifa.”alisema Yassin.
Mmoja wa wafanyakazi wa Swissport, Gilead Marisa alisema yeye ana tabia ya kutoa damu kusaidia wanawake wanaokwenda kujifungua na majeruhi wa ajali na watu mbalimbali wenye shida ya damu salama.
Aliitaka jamii kujenga mazoea ya kuchangia damu kuokoa maisha ya watu wengi.
Ofisa Uhamasishaji wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Fatuma Mjungu alisema kwa mwaka, mahitaji ya damu nchini ni chupa 300,000.
Alisema kila mkoa umejiwekea lengo la kuchangia chupa 100 za damu salama ambako kwa mikoa yote 25 ya Tanzania bara zitapatikana chupa 2,500.