29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAKAVU WA MAJENGO WAMTESA MKEMIA MKUU

   Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa                          Samwel Manyele

Na AZIZA MASOUD -DAR ES SALAAM

OFISI ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imeiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutenga bajeti kukarabati mitambo na majengo yake ambayo yamechakaa.

Akizungumza katika ghafla ya kutoa zawadi kwa walimu wanne na wanafunzi 18 waliohitimu na kufanyaa vizuri katika masomo ya Kemia na Biolojia kwenye mitihani ya taifa kidato cha nne 2015 na sita 2016, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, alisema moja ya changamoto inayoikabili ofisi hiyo ni uchakavu wa majengo ambayo yamejengwa tangu kipindi cha ukoloni.

“Majengo yaliyopo mengi ni yale yaliyorithiwa kutoka ukoloni wa Kijerumani, zipo jitihada zinazoendelea za kurekebisha majengo haya, lakini kutokana na ufinyu wa bajeti zinafanyika kwa kasi ndogo,” alisema Profesa Manyele.

Alisema wakala pia ina changamoto ya ukosefu wa vifaa na mitambo ya kisasa na upungufu wa rasilimali watu unaotokana na ufinyu wa bajeti.

Aliongeza kuwa ufinyu wa bajeti unatokana na wakala kutopata ruzuku kutoka serikalini na kulazimika kutumia mapato yake ya ndani kutekeleza vipaumbele vinavyotolewa na wizara.

Akizungumzia lengo la kutoa zawadi hizo, alisema ni kuleta hamasa kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi nchini waweze kufikia malengo waliyojiwekea.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Bakari, alisema mkakati wa wizara wa kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM) hauna budi kwenda sambamba na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa katika vyuo vya afya na ustawi wa jamii.

“Wizara inaendelea na juhudi za kuhamasisha vijana wetu kupenda masomo ya sayansi na hatimaye waweze kuongeza idadi ya wanaodahiliwa katika michepuo ya masomo ya sayansi,” alisema Dk. Bakari.

Wanafunzi wa kidato cha nne waliopata zawadi ni Marynas Duduye na Julieth Zannie kutoka Sekondari ya St. Francis, David Joseph kutoka Ilboru na Asha Mlanzi wa Jangwani.

Wanafunzi wa kidato cha sita waliofanya vizuri katika masomo hayo ni Sheikhas Rashid  wa shule ya Feza Wasichana, Prisca Kyando kutoka Kilakala na Gastory Munishi wa Mzumbe.

Mbali na wanafunzi, walimu waliokabidhiwa zawadi ni Vaileth Kalangali na Frank Mella wa Ilboru, Habil Selemani wa Feza Wavulana na Joram Yohana wa Uwata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles