24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI MKUU RWANDA 2017: MUHULA WA TATU WA URAIS WENYE KILIO CHA DEMOKRASIA

NA MARKUS MPANGALA,

AGOSTI 4, mwaka huu, wananchi wa Rwanda wataingia kwenye Uchaguzi Mkuu wa urais, wabunge na wawakilishi na viongozi mbalimbali.

Kwa kuwa Rwanda ni mwanachama wa Afrika Mashariki, MTANZANIA Jumapili tutakuletea uchambuzi wa kina kuhusu mwenendo wa uchaguzi na mambo mbalimbali kuhusu siasa za nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Katiba ya Rwanda, Uchaguzi Mkuu hufanyika kila baada ya miaka 7, lakini kuanzia mwaka 2024 kutakuwa na mabadiliko ya miaka ya kukaa madarakani kutoka miaka 7 hadi 5.

Mabadiliko hayo yametokana na marekebisho ya Katiba ya Rwanda, yaliyompa nafasi Kagame kuongeza muhula wa tatu na kupunguza muda wa kukaa madarakani.

Aidha, mabadiliko hayo pia yanamwezesha Paul Kagame kugombea muhula wa nne wa urais iwapo ataamua kufanya hivyo. Hii ina maana kama ataamua kugombea mwaka 2024, atadumu madarakani hadi mwaka 2029. Endapo mwaka 2029 akigombea tena atadumu hadi mwaka 2034.

Wiki hii chama cha RPF kimempitisha Paul Kagame kuwa mgombea wake wa urais mwaka huu. Taarifa zinasema Kagame anagombea kwa mara ya mwisho, kwani amepanga kustaafu siasa na uongozi ifikapo mwaka 2024. Uamuzi wa kustaafu ameutoa mwenyewe.

Akizungumza wakati wa kumpitisha, Kagame amesema imefika mahali sasa Rwanda ijiandae kuongozwa na mtu mwingine na kwamba anakitumia kipindi hicho cha mwisho kuweka maandalizi hayo.

Kagame amebainisha kuwa, Rwanda inaweza kuishi bila yeye na sasa ni wakati wa kumkaribisha kiongozi mpya atakapomaliza uongozi wake mwaka 2024.

Vilevile kuna vyama viwili vya upinzani nchini humo vimetangaza kumuunga mkono Rais Kagame kwenye Uchaguzi Mkuu wa urais. Hata hivyo, kuna swali moja wachambuzi wanajiuliza, itawezekana vipi Rwanda kuishi bila Kagame au itakuwa na taswira gani? Hilo tusubiri kuliona.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, kampeni zinatarajiwa kuanza mwezi ujao. Aidha, tume ya uchaguzi inatarajiwa kuthibitisha majina ya wagombea waliofuzu vigezo vya nafasi ya urais ifikapo Juni 27, mwaka huu, ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kampeni.

Kilio cha demokrasia

Mmoja wa wagombea urais wa Rwanda ni Diane Rwigara. Wakati akitoa tangazo la kugombea urais kama mgombea binafsi, alisema amesukumwa na uhaba wa demokrasia na umasikini uliotamalaki.

Baadhi ya wananchi na wanasiasa wanaona uamuzi wa Kagame kugombea muhula wa tatu ni uharibifu wa demokrasia, licha ya kufanyika mabadiliko ya Katiba.

Ikumbukwe kulikuwa na vuguvugu la kumtaka Kagame aruhusiwe kugombea urais na kwamba Katiba ifanyiwe marekebisho. Ndivyo ilivyokuwa, kwani Bunge la Rwanda liliazimia kwa kauli moja kubadilisha Katiba ili kuondoa ukomo wa urais.

Kwa upande wake, Paul Kagame amekuwa akijitetea kila anapopata fursa kwamba uamuzi wa kugombea muhula wa tatu umetokana na kura za maoni na mawazo ya Wanyarwanda.

“Sikuomba hili lifanywe, nenda kawaulize Wanyarwanda mbona wakajiingiza katika hili (kubadilisha Katiba), labda unaweza kupata wazo na kujua ni yapi yanatarajiwa. Wanyarwanda wana mustakabali gani? Si mimi ningedhibiti mustakabali wao. Wanashikilia hatima yao mikononi,” alisema Kagame, alipozungumza na vyombo vya habari mwaka jana, mara baada ya kupiga kura ya kubadilisha Katiba katika kituo cha Rugunga, mjini Kigali.

Wapiga kura walipigia kura marekebisho ya Katiba ya 2015, na miongoni mwa mambo mengine ni kupunguza muda wa rais kuongoza nchi hiyo na kuwa mihula miwili ya miaka mitano badala ya saba.

Jumuiya ya kimataifa, ikiongozwa na Marekani, ilipinga uamuzi uliofanywa na Rwanda wa kumuongezea muda wa kubaki madarakani Rais Kagame. Pamoja na kupinga huko, bado juhudi hizo hazikufua dafu.

Serikali ya mseto

Utawala wa Rais Kagame umekuwa ukilaumiwa kwa kuendesha nchi hiyo kwa mkono wa chuma, vikiwamo vitisho, utesaji na ukamatwaji wa wapinzani wa serikali popote walipo.

Aidha, kumekuwa na tuhuma kuwa Serikali ya Kagame inawafunga jela wanasiasa wote wanaojitokeza kumpinga kiongozi huyo.

Februari 26, mwaka huu, baadhi ya wanasiasa wa Kinyarwanda wa upande wa upinzani  wapatao 30 pamoja na wawakilishi wa mashirika mbalimbali,  kama vile vyama vya kiraia, wanaharakati wa haki za binadamu, walikusanyika katika mkutano mjini Paris, nchini Ufaransa, kwa madhumuni ya kukuza ujio wa serikali ya kidemokrasia na shauku ya kulinda maslahi ya wananchi wa Rwanda.

Mkutano huo ulijaa shutuma nyingi dhidi ya Kagame, kwamba anazuia kabisa nafasi ya kisiasa kwa vyama vya upinzani na kuweka vikwazo vyenye kukinufaisha chama chake, Rwanda Patriotic Front.

Pamoja na azimio hilo, bado wanasiasa hao hawakuwa na mwangwi unaoweza kumtisha Paul Kagame. Vilevile wanaweza kutumia uchaguzi huu kama njia ya kuhakikisha kuwa wanatimiza malengo yao, yakiwamo ya kuunda serikali ya mseto inayowashirikisha makundi mengi ya kijamii.

Kubana matumizi

Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Rwanda (NEC) imesema uchaguzi wa mwaka huu utatumia fedha kidogo kuliko chaguzi nyingine zilizopita.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Tume hiyo, Charles Munyaneza, dola milioni 6.9 za Marekani zimetengwa kwa ajili ya uchaguzi huo, ikiwa ni punguzo la asilimia 36 kulingana na uchaguzi wa rais wa mwaka 2010.

Tume hiyo imesema zaidi ya asilimia 95 ya bajeti ya uchaguzi huo itagharamiwa na serikali na zinazobaki zitachangiwa na wadau wa maendeleo.

Itaendelea Jumapili ijayo…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles