31 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI MKUU MAREKANI 2016

Hillary Clinton speaks in Washington
Hillary Clinton

 

* Kura za mchujo somo tosha kwa Trump, Clinton

LABDA tu kitokee kitu kisichotarajiwa, wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa Marekani hapo Novemba mwaka huu ni Hillary Clinton na Donald Trump.

Ni uchaguzi wa kipekee kwa vile unahusisha wagombea, ambao hawaungwi mkono vya kutosha na vyama vyao na Wamarekani kwa ujumla ijapokuwa Clinton anaongoza kura za maoni hadi sasa.

Kwanini? Kwa kuanzia Clinton, kashfa haziishi kumwandama huku mpinzani wake- Trump akilaumiwa kwa kauli tata zikiwamo za chuki dhidi ya makundi fulani ya jamii.

Lakini halitarajii kuwazuia kupitishwa rasmi na vyama vyao vya Democratic na Republican wakati wa mikutano mikuu itakayofanyika baadaye mwezi huu.

Ni kwa sababu wote walipata kura za kutosha za wajumbe majimboni na hivyo ‘mhuri’ tu vinginevyo wangejikuta wakisubiri uamuzi wa wajumbe wakuu (superdelegates) kuamua wakati wa mikutano hiyo.

Kiuhalisia, ijapokuwa Clinton ana kundi kubwa la wajumbe wakuu, hakuna hata mmoja ambaye atafikiria kumtosa kwa ajili ya aliyekuwa mpinzani wake pekee Bernie Sanders.

Lakini wagombea hawa wamefikaje hapo? Clinton asingefika hapo bila kushinda katika majimbo makubwa, akisomba kura kwa wingi kusini mwa nchi na kuungwa mkono na wenye umri mkubwa na wapiga kura wasio weupe.

Kwa Trump, kampeni dhidi yake ndani ya chama chake cha Republican ilimnufaisha pande zote za nchi, muhimu zaidi ikiwa katika majimbo kama Florida na New York na miongoni mwa wapiga kura weupe au wanaume.

Somo lilitokana na kura hizo za mchujo linabakia kuwa na umuhimu bado kwa wawili hao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Novemba 2016.

Miongoni mwa mambo ya kuzingatiwa kutokana na somo lililotokea wakati wa mchakato wa kura za mchujo ni pamoja na masuala ya demografia, mwitikio wa wapiga kura na jiografia.

Donald Trump
Donald Trump

Demografia

Ushindi wa Clinton na Trump katika kinyang’anyiro cha mchujo katika vyama vyao umetokana na sababu ya kila mmoja kuwa na kundi la kijamii linalomuunga mkono vya kutosha.

Hata hivyo, kuyafahamu makundi ya Wamarekani yaliyoshiriki wakati wa mchujo ni kazi ngumu sana kwa sababu hutegemea matokeo ya kura za awali zijulikanazo kama exit polls.

Kura hizo ni utaratibu wa kuwauliza wapiga kura mgombea waliyemchagua wakati wanapoondoka katika vituo vya kupiga kura, mchakato ambao ni gharama mno kufuatilia.

Kura hizo za awali daima zinapaswa kuchukuliwa kwa uangalifu mkubwa; mara nyingi huleta matokeo tofauti, kwa sababu ni vigumu kupata sampuli wakilishi za wapiga kura wakati wa siku ya uchaguzi. Lakini bado zinaweza kutoa mwelekeo namna na aina ya demografia  zilizowapendelea Trump na Clinton.

Kwa kuchukulia mfano huu, sehemu kubwa ya majimbo 27, ambayo kura za awali za Republican zilizoendeshwa na Shirika la Habari la Marekani (CNN), wapiga kura weupe, wanaume, wenye umri mkubwa, wasio na shahada ya chuo na wale wenye kipato cha chini walimpigia kura Trump.

Katika majimbo hayo, ambako pia CNN waliendesha kura za awali kwa wapiga kura wa Democratic, waliohojiwa, ambao hawakuwa weupe, walio wasomi wa chuo na matajiri walimpigia kura zaidi Clinton.

Kwa sababu hiyo Demografia ina mchango mkubwa katika uchaguzi wa Novemba.  Angalia hili pia, ushindi wa Obama mwaka 2008 ulitokana na sababu hii; kutokana na kuungwa mkono na wapiga kura vijana.

Hali kadhalika ushindi wa George W Bush mwaka 2004 ulitokana na kuungwa mkono zaidi na wanaume na wapiga kura weupe.

Lakini kwa kuangalia namna demografia ilivyowatazama Trump na Clinton, wawili hao wanakubalika na Wamarekani wa makundi tofauti.

Kwa sababu hiyo, Clinton hatarajii kutumia nguvu nyingi kuwashawishi wanachama wa Republican weupe na wanaume kumpigia kura katika uchaguzi huo.

Wagombea wote wawili wanafahamu fika kujaribu kupanua wigo wa makundi ya kuwaunga mkono huzidi kuwa ngumu kwa kadiri uchaguzi unavyokaribia.

Badala yake wawili hao wanatarajia kujikita zaidi katika kupanua uungwaji mkono katika eneo wanalokubalika zaidi kwa kuhakikisha watu wengi kutoka makundi hayo ya demografia wanaenda kupiga kura siku ya uchaguzi.

Kuhamasisha makundi yao kujitokeza kwa wingi, kunamaanisha kwamba mwitikio wa wapiga kura ni muhimu pia kuleta ushindi kwao.

Mwitikio wa wapiga kura

Kufikia Machi mwaka huu, mwitikio wa wapiga kura katika kura za mchujo ulionekana kuwa asimilia 29 kwa mujibu wa Kituo cha Utafiti cha Pew – ikiwa pungufu tu ya asilimia moja ya ilivyokuwa mwaka 2008, wakati mwitikio ulipokuwa juu katika historia ya siasa za taifa hilo ukichagizwa na kampeni za Rais Obama na Clinton.

Lakini pia mwitikio wa sasa kukaribia ule wa 2008 umechagizwa kwa kiasi kikubwa na wana-Republican, ambao kwa kipindi cha miaka 26 iliyopita walikuwa nadra kuzifikia tarakimu mbili, lakini safari hii waliweza kusimama kwa karibu asilimia 17.

Je, hilo linamaanisha kuwa mwitikio wa Republican pia utakuwa juu katika historia ya uchaguzi mkuu? Si lazima iwe hivyo. Kujaribu kuilinganisha mwitikio wa kura za mchujo na chaguzi kuu unatakiwa kutohusisha chaguzi kama wa 2012, ambao mbio za mchujo zilihusisha uteuzi wa chama kimoja tu.

Kwa kuziangalia chaguzi sita kati ya 11 zilizopita ambazo kura za mchujo zilihusisha vyama vyote viwili, kunaonekana uwiano mdogo baina ya mwitikio wa kura za mchujo na ule wa uchaguzi mkuu.

Iwapo mpambano utaonekana wa ushindani wa karibu, Trump na Clinton watalazimika kuwasihi wapiga kura ambao hawajaamua nani wa kumpigia kura.

Kisha watahamia kwa wapiga kura huru, ambao hawajitambulishi kuwa wa chama chochote na ambao idadi yao imekuwa ikikua kipindi cha miongo mitatu iliyopita.

Mwaka 2015, asilimia 42 ya Wamarekani walijitambulisha kama huru, kwa mujibu wa Gallup, wakati asilimia 29 tu ikijitambulisha kuwa  wapiga kura wa Democratic na asilimia 26 wa Republican.

Jiografia

Sanders alishinda michuano zaidi ya 20 ya kura za mchujo. Lakini tatizo lake ni kwamba hakushinda vya kutosha kwa idadi kubwa lakini pia alishinda mahala pasipo sahihi.

Ijapokuwa ushindi wake wa kishindo huko Vermont ulikuwa mafanikio makubwa, lakini jimbo hilo likiwa na wajumbe 16 tu, hakukuleta maana kubwa.

Kwa kulinganisha, mafanikio ya Clinton katika majimbo ya kusini kama vile Texas (ambalo lina wajumbe 251), Florida (246) na Georgia (117) kulikuwa muhimu kwa mafanikio yake.

Kwamba Clinton alipata ushindi katika majimbo makubwa, Sanders alishinda kwa kishindo katika yale madogo yenye wajumbe wachache.

Kwa sababu kila jimbo lina idadi tofauti ya wajumbe, na hivyo haijalishi kwamba umeshinda, bali wapi umeshinda. Hilo pia ni katika ngazi ya kitaifa hapo Novemba, kwa vile kura pia hazigawanyi sawa. Kwa mfano Texas ina kura 38, wakati South Dakota ina kura tatu tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles