25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI MKUU KUAJIRI MAELFU YA WAFANYAKAZI

NAIROBI, KENYA

MAANDALIZI ya Uchaguzi Mkuu nchini Kenya yamepamba moto huku Tume ya Uchaguzi isiyo na Mipaka, IEBC ikitarajiwa kuajiri wafanyakazi wa muda mfupi takribani 360,000 kwa ajili ya kukamilisha zoezi la uchaguzi nchini humo utakaofanyika Agosti 8, mwaka huu.

Mengi yamejiri kufikia uamuzi wa Mahakama ya Rufaa nchini Kenya kupinga na kubatilisha uamuzi wa mahakama kuu kuzuia na kufuta zabuni ya uchapishaji wa karatasi za kupigia kura za urais kutokana na kesi iliyowasilishwa na muungano wa vyama vya upinzani, NASA katika mahakama hiyo kupinga uchapishwaji wa karatasi hizo.

Tume imesema uchaguzi utafanyika kwa siku 18 wakati Rais Uhuru Kenyatta anasisitiza kuwa uchaguzi lazima uendelee kama sheria inavyotaka. Upande wa upinzani ulitaka uchaguzi huo uahirishwe iwapo vifaa vya kuwezesha kupigia kura ya haki haviridhishi.

Zaidi ya kesi 10 zilifunguliwa na wapinzani na asasi za kiraia dhidi ya Tume ya Uchaguzi IEBC nchini humo.

Kati ya wafanyakazi wa muda mfupi  wanaoajiriwa ni maofisa wa polisi 180,000 wa kutoa ulinzi kwenye vituo zaidi ya 40,883 vya polisi, vituo 290 vya kuhesabu katika majimbo mbalimbali na vituo 47 vya kuhesabu kura za kila jimbo pamoja na kituo cha taifa cha uhesabuji wa kura cha Boma kilichopo jijini Nairobi.

Msemaji wa IEBC, Andrew Limo, jana alisema kwamba ingawa tume hiyo ina magari lakini itaongeza magari mengine 25,000 ili kusaidia zoezi la ugawaji wa vifaa vya kupigia kura.

“Kila kituo kati ya vituo 40,883 vya kupigia kura vina magari, makarani 6, wasimamizi na manaibu wake, maofisa usalama wawili pamoja na wataalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano.”

Makarani wa vituo vya kupigia kura, maofisa uongozi na wasaidizi wake watapewa mafunzo maalumu na wakufunzi wa jimbo kwa ajili ya mchakato mzima wa uchaguzi huo.

Tume inatarajia kuwaajiri viongozi 91,032 na manaibu wake, makarani wa uchaguzi 262,665 pamoja na wataalamu wa teknolojia 580 wakiwa wawili kwa kila jimbo kati ya majimbo yote 290 na waelimishaji 2,900, ambapo kila kituo watawekwa wawili katika kata 1,450.

Wasimamizi hao wa uchaguzi na wasaidizi wao watafanya kazi kwa mkataba wa siku 13 kwa malipo ya shilingi 2,000 na 1,800 kwa mtiririko huo.

Aidha, makarani wa vituo hivyo wataajiriwa kwa kazi ya siku 9 na kulipwa shilingi 1,000 kwa siku.

Pia eneo jingine ambalo litazalisha ajira katika uchaguzi huo ni maofisa wa usafirishaji wa vifaa vya uchaguzi 377, mmoja kwa kila jimbo kati ya majimbo yote 290 na tarafa 47 ambao ajira yao itakuwa ya siku 30 na kulipwa shilingi 1,500 kwa siku.

“Pia tutaajiri si chini ya magari 25,000”, aliongeza.

Kwa mujibu wa IEBC idadi ya maofisa wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu imeongezeka mara mbili zaidi ya idadi ile iliyotumika kwenye uchaguzi wa mwaka 2013.

Kulingana na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Joseph Borret, maofisa wa usalama na ulinzi watakaotumika kwenye uchaguzi huo watapatiwa mafunzo maalumu ya kipolisi ambao kazi yao itakuwa ni kutekeleza sheria kabla na wakati wa uchaguzi.

“Hatutaki siasa, hatutapendelea na wala kutumia sheria vibaya. Haturuhusu upuuzi wowote kwa yeyote bila kujali itikadi za vyama vya saisa,” alisema Boinet.

Julai 18, IFBC walipokea mizigo ya karatasi za kupiga kura kwa majimbo 41 ya uchaguzi katika nafasi ya ugavana kupitia Mkurugenzi Mtendaji wa IEBC, Ezra Chiloba, ambaye alibainisha kuwa tume hiyo inatarajiwa kupokea karatasi nyingine awamu ya pili tofauti kila baada ya siku mbili.

“Tumepokea vifaa hivi na tutavipeleka kwenye ghala letu chini ya ulinzi mkali,” alisema akiwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Majaji watano wa Mahakama ya Rufaa, Erastus Githinji, Rose Nambuye, Alunashir Visran, Jamila Mohammed na Otieno Odek, wamepitisha amri ya kuendelea na utekelezaji wa zabuni ya uchapishaji na usambazaji wa karatasi hizo kwa Kampuni ya Al-Ghurair ya Dubai.

“Hatutakuwa na karatasi za urais kama hatutaanza kuzichapa kama ilivyotarajiwa. Haiwezekani kwa IEBC kuanzisha zabuni nyingine mpya kwani itatuchukua karibu siku 52 kukamilisha mchakato mzima,” alisema mshauri wa mwandamizi mbele ya mahakama, Paul Muite.

Karatasi za urais zilipangwa zichapwe kwa mara ya kwanza Julai 18, 2017 na kwa awamu yake ya pili ni Agosti 2, 2017.

Wakati zoezi hilo lilipositishwa na Majaji watatu wa Mahakama Kuu, sababu kubwa ilikuwa kutoshirikishwa kwa wananchi katika utoaji wa zabuni hiyo, liliirudisha nyuma tume ya uchaguzi.

Hata hivyo, kubatilishwa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu kulikofanywa na Mahakama ya Rufaa kumeharakisha kukamilika kwa zoezi hilo na kuipa muda wa kutosha IEBC kutekeleza wajibu wake kabla ya Agosti 8.

“Kwa kuwa ni taasisi ya umma, inatakiwa umma huo ushirikishwe kwenye suala la utoaji wa zabuni au manunuzi. Ni kama hivyo, nitasema lilikuwa jambo tofauti katika utekelezaji wa shughuli za umma,” alisema Ezra Chiloba.

Mbali ya Kampuni ya Al-Ghurair iliyotoa ofa ya shilingi bilioni 2.5, nyingine zilizokuwa tayari kuchukua zabuni hiyo ni DPS Print Supplies ya Marekani, United Print, Manipal Technologies and KL Hitech Secure Print za India, Tall Security ya Uingereza, Paarl Media ya Afrika Kusini, Ellams Production Limited ya Kenya na Baltijas Banknote.

IEBC ilitakiwa kuchagua kampuni nyingine kuipa zabuni ya kuchapisha karatasi hali ambayo ingechelewesha zoezi zima.

Kwa sasa masanduku ya karatasi za kupigia kura 45,000 yanatarajiwa kupelekwa kwenye vituo mbalimbali.

Tofauti na uchaguzi wa mwaka 2013 ambapo siku mbili kabla ya uchaguzi baadhi ya vifaa vilikuwa havijafika.

Uchaguzi wa mwaka huu vifaa vitawasilishwa mapema. Jumla ya masanduku 45,000 yatapelekwa katika vituo vyote vya kupigia 40,883.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles